Makala

TAHARIRI: Usalama shuleni usibahatishwe

December 2nd, 2020 2 min read

KITENGO CHA UHARIRI

RIPOTI kwamba wanafunzi 78 wa shule ya upili walitoroka ili kushirikia zoezi la upashaji tohara ni tukio la kufadhaisha.

Imeripotiwa kwamba wanafunzi hao wa kidato cha Nne kutoka Shule ya Wavulana ya Kisanana, Kaunti ya Baringo walihepa shuleni saa saba usiku huku wakiacha wenzao 23 pekee kwenye taasisi hiyo.

Ingawa mkurugenzi wa elimu katika eneo hilo amesema kwamba kiini cha watoto hao kutoroka haijabainika, kuna maswali kadha ambayo yamejitokeza moja kwa moja kuhusiana na kisa hiki.

Je, wanafunzi hawa waliweza kutoroka vipi? Usalama wa kutosha katika taasisi hii upo? Bawabu wa shule, mwalimu mkuu na mwalimu wa zamu walikuwa wapi kisa hiki kikitendeka? Mwalimu mkuu wa shule ameweka mikakati gani kuhakikishia watoto na wafanyakazi wa shule usalama wa kutosha?

Jukumu la usalama katika shule hasa ya bweni ni la mwalimu mkuu kwa ushirikiano wa bodi ya usimamizi katika taasisi husika.

Kila mzazi anapopeleka mtoto shuleni, hitaji la kimsingi analohitaji ni usalama kwa mtoto wake. Endapo shule limekosa usalama basi halifai kuruhusiwa kuendesha shughuli za masomo kwa kukwa hazikwezi kufanikiwa.

Kuna suala lingine linalojitokeza katika kisa hiki kwamba, huenda jamii inayozunguka shule hii imechangia pakubwa katika kitendo cha wanafunzi kutoroka. Hii ni kwa sababu, kuna uwezekano mkubwa kuwepo wahusika waliopasha wanafunzi hawa kuhusu zoezi la kupasha tohara hasa siku, wakati na mahali ambapo lingefanyika. Si ajabu kwamba hata baadhi ya wazazi wa watoto hawa walihusika katika kuwashauri au kuwatorosha wanafunzi ili washiriki katika zoezi hilo la kitamaduni. Bila shaka chifu wa eneo hilo ana jukumu la kuzuia matukio kama haya kuendelezwa kwani yanaathiri masomo ya watoto wakiwa shuleni.

Walimu pia walifaa kufanya uchunguzi wa mapema kuhakikisha tukio kama hili lingezuiwa kwa kuwa inawezekana watoto hawa walikuwa wakihepa mtihani ambao ungefanyika Ijumaa ijayo. Aidha wangetumia viranja wa wanafunzi kupata habari mapema.

Kwa ufupi, hiki ni kisa ambacho kingezuilika. Walimu wakuu nchini wanafaa kujua kwamba ni jukumu lao kuhakikishia kila mwanafunzi usalama wa kutosha shuleni. Wanafaa kushirikiana machifu na wakuu wa vituo vya polisi kufanikisha hili. Aidha wanafaa kuwa na ushirikiano bora na wazazi na viranja wa wanafunzi kukamilisha usimamizi wao.