Makala

TAHARIRI: Usawa wahitaji suluhu la kudumu

September 22nd, 2020 1 min read

Na MHARIRI

PENDEKEZO la Jaji Mkuu David Maraga kwa Rais Uhuru Kenyatta kuvunja bunge Jumatatu lilipokewa kwa hisia mseto.

Pendekezo hilo ambalo msingi wake ni kuwa bunge limeshindwa kutekeleza usawa wa jinsia kikatiba lilisifiwa na wengi huku likikashifiwa na wengine wengi vile vile.

Jukumu la iwapo bunge litavunjwa au la, sasa limo mikononi mwa Rais Kenyatta.

Bila shaka, Rais anatarajiwa kufanya maamuzi yake kwa kufuata ushauri wa wataalamu wa sheria na pia masuala ya uongozi waliomzingira.

Huo hautakuwa uamuzi rahisi kufanya, kwani kwa upande mmoja, Rais anafaa aonekane anaheshimu katiba inayotaka kuwe na usawa wa jinsia bungeni.

Kwa upande mwingine, kuna masuala kama vile gharama itakayosababishwa na uamuzi wa kuvunja bunge kwa taifa.

Gharama hiyo haihusu masuala ya kifedha pekee bali pia shughuli muhimu zitakazovurugwa.

Haya yote yanadhihirisha kuwa hili ni suala zito lisilofaa kufanyiwa mzaha.

Hivyo basi, itakuwa vyema kama taifa litajihoji na kuamua kutafuta suluhisho ya kudumu kuhusu usawa wa jinsia.

Haitakuwa busara kama maamuzi yatakayotolewa sasa yatakosa kuleta tofauti yoyote katika miaka ijayo kisha tujipate tukirudia makosa yale yale ya awali.

Baadhi ya wadadisi husema janga la uongozi linalotokana na ukiukaji wa katiba bungeni kwa kukosa kutimiza usawa wa jinsia, linaweza kuepukwa kupitia marekebisho ya sheria ambayo yatapitishwa na wabunge wenyewe.

Huu ni wakati mwafaka sasa kwa taifa zima kuweka kando tofauti zao na kutafuta jinsi ya kutatua tatizo hilo lililopo.

Endapo Rais ataamua kuepuka kuvunja bunge, atoe nafasi kwa wadau wote kushirikiana ili tupate sheria ambayo itatekeleza usawa wa jinsia bila vikwazo wala kuongezea mwananchi gharama ya ushuru.

Hatua zozote zitakazochukuliwa zisiwe na malengo ya kibinafsi bali zitilie maanani mahitaji ya kulinda na kuboresha maisha ya kila mwananchi.