TAHARIRI: Usimamizi wa soka umedorora

TAHARIRI: Usimamizi wa soka umedorora

KITENGO CHA UHARIRI

MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya Soka (KPL) unaanza hii leo ukigubikwa na sintofahamu kubwa jinsi ligi itafadhiliwa, baada ya kampuni ya Odibet kuwa ya hivi punde kuondoa udhamini wake.

Wiki hii Odibet ilitangaza rasmi kuagana na Shirikisho la Soka Nchini (FKF) kwa kile kinachosemekana ni kutoridhishwa na juhudi za shirikisho kukuza soka mashinani.

Kampuni hiyo ya kamari ilikuwa ikitoa ufadhili wa Sh127 milioni katika mkataba wa miaka mitatu uliotangazwa Desemba 2019. Ufadhili huo ulikuwa kwa Ligi ya Kitaifa Daraja ya Kwanza, Ligi ya Kitaifa Daraja ya Pili na Ligi ya Kaunti.

Madhumuni yalikuwa kuimarisha kandanda mashinani ili kuwa na timu thabiti zinazokuza chipukizi watakaowika kesho na mtondogoo.

Kujiondoa kwa Odibet kunakujia miezi kadha baada ya wafadhili wa Ligi Kuu, Betking, kukatiza uhusiano wake na FKF kuelekea mwisho wa msimu jana Agosti.

Betking, kutoka Nigeria, ilikuwa imetoa ufadhili wa Sh1.2 bilioni katika mkataba wa miaka mitano kuanzia Julai 2020.Kwa sasa ni kampuni moja pekee iliyosalia ya Betika, inayofadhili Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL).

Hata huko mambo ni hatihati huku kukiwa na minong’ono kwamba pia inawazia kuondoa ufadhili wake wa Sh45 milioni kwa miaka mitatu, ulioanza Novemba 2019.

Ni wazi kwamba wafadhili hawana imani tena jinsi Rais Nick Mwendwa anavyosimamia soka ya Kenya.Kinara huyo amejawa na kiburi, haambiliki hasemezeki. Hataki kuwajibikia mabilioni ya fedha ambazo FKF inapokea kuendesha soka.

Isitoshe, amekuwa kama dikteta – alilazimisha klabu za soka kutia saini mkataba wa kupeperusha mechi kupitia Star Times, la sivyo zinyimwe posho la ufadhili wa Betking.

Akajipata katika mvutano na vigogo wa soka nchini, Gor na AFC, kuhusu Sh3 milioni za kombe la Betway Cup ilhali siku chache tu alizindua mnara wa KPL la Sh5 milioni.

Juzi aliibuka na jipya alipotangaza kocha mpya wa timu ya taifa Harambee Stars kwa mkataba wa miezi miwili! Ni matukio ya kushangaza jinsi usimamizi wa soka unavyozidi kudorora kila uchao. Je, nani atawaondolea mashabiki madhila haya?

Wanachama wa Baraza Simamizi la Kitaifa (NEC) ndio wenye kuamua jibu la swali hili. Wako na uwezo wa kupiga kura ya kumuondoa Mwendwa ofisini kwani hatokubali kubanduka. Wataweza?

Tunasubiri kuona iwapo watatimiza wajibu huo ipasavyo ili kuokoa soka ya Kenya.

You can share this post!

Upasuaji waonyesha daktari alikufa kwa sumu

Walimu Nairobi kula marupurupu ya juu ya nyumba