Makala

TAHARIRI: Uvamizi ni ithibati ugaidi bado tisho

November 22nd, 2018 2 min read

NA MHARIRI

Kisa cha hivi majuzi ambapo magaidi wa Al-Shabaab walivamia eneo la Chakama katika kaunti ya Kilifi na kumchukua mateka Bi Syllvia Constance, raia wa Italia ni ukumbusho kwamba, magaidi hao wangali tishio kwa usalama wa nchi hii licha ya juhudi nyingi za kuwadhibiti.

Mojawapo ya sababu zilizochochea Serikali kuwapeleka wanajeshi wetu nchini Somalia ni visa vya uvamizi vya mara kwa mara vilivyotekelezwa na wahalifu hao waliovizia watalii na wenyeji, hasa sehemu za mpakani.

Hali hiyo iliathiri pakubwa sekta ya utalii. Hivyo basi, wakati juhudi nyingi zilizofanywa na raslimali nyingi kutumika kufufua sekta hiyo zinapoonekana kuanza kuzalisha matunda, yamkini magaidi hao wanataka kuzua hofu tena kwa lengo la kuisambaratisha sekta hiyo.

Kama tulivyowahi kutaja kwenye safu hizi, Al-Shabaab hawatambui mazuri wala hawafurahii kuona raia wenzao wakiishi kwa utulivu. Ndio maana wanalenga wahudumu kama Bi Constance ambao mchango wao kwa wasiobahatika katika jamii ni mkubwa.

Wakati umewadia kwa serikali na hasa wakuu jeshini kubadili mkakati wa kuzima makali ya genge hili. Kwa mfano, tunaamini ingekuwa bora zaidi iwapo wanajeshi hao wangeimarisha usalama katika sehemu za mpakani ili kuzima wahalifu hao wasiothamini maisha ya binadamu kuingia nchini.

Ilivyo kwa sasa ni kwamba, sehemu kubwa ya mpaka kati ya Somalia ambayo ni ngome ya magaidi hao na Kenya, iko wazi na magaidi hao, huweza kuvamia vijijini na kuzua taharuki bila vikwazo vyovyote. Hali hii ni lazima ikomeshwe.

Vile vile, tungependa kutaja hapa kwamba, uvamizi wa juzi ni thibitisho tosha kwamba, magaidi hao wangali tishio kwa usalama wa nchi hii licha ya wanajeshi wetu, kwa ushirikiano na kikosi cha wa Umoja wa Afrika pamoja na wenzao wa Amerika kuimarisha juhudi za kuwaangamiza.

Kwa msingi huo, tunahimiza Wakenya wote kumakinika popote pale walipo ili magaidi hao wasifanikiwe kusababisha umwagikaji wa damu ya raia wasio na hatia.

Idara ya polisi inapasa kurejesha tena kampeni ya kutoa uhamasisho kwa Wakenya kuhusu manufaa ya kukaa chonjo kama walivyofanya mbeleni, hasa mwanzo mwanzo wa mashambulizi hayo.

Ni kwa kufanya hivyo wahalifu hao wanaweza kudhibitiwa bila maafa yoyote kutokea.