Makala

TAHARIRI: Uwakilishi wa jiji katika baraza la mawaziri wafaa

September 11th, 2020 2 min read

Na MHARIRI

HATUA ya Rais Uhuru Kenyatta kumruhusu Mkurugenzi Mkuu wa Halmashauri ya Usimamizi wa Jiji la Nairobi (NMS), Mohamed Badi, kuanza kuhudhuria vikao vya Baraza la Mawaziri ni nzuri endapo itaboresha hali ya utoaji wa huduma jijini.

Bila shaka, ni hatua inayoashiria kwamba serikali imejitolea kuona Nairobi imerejesha hadhi yake kama jiji kuu la Kenya na mojawapo ya miji mikubwa zaidi katika eneo la Afrika Mashariki na Kati.

Alhamisi, Jenerali Badi alikula kiapo cha kuweka siri, ambacho ni hitaji la kila mmoja anayehudhuria vikao hivyo.

Mnamo Machi, Rais Kenyatta alibuni halmashauri hiyo na kumteua Jen Badi kuiongoza, kwenye juhudi za kumsaidia Gavana Mike Sonko kuliendesha jiji.

Hatua ya Rais ilionekana kuchochewa na malalamishi ya wananchi wengi, kwamba hadhi ya Nairobi kama mji mkuu ilikuwa ikididimia kutokana na ongezelo la taka jijini, barabara mbovu, ongezeko la wahalifu kati ya mengine.

Kwa wenyeji wa Nairobi ama yeyote ambaye hufika jijini mara nyingi kwa shughuli zake, utendakazi wa halmashauri hiyo umeanza kuonekana.

Baadhi ya dalili zake ni barabara nzuri na uokotaji taka, hali ambayo imeanza kurejesha taswira ya Nairobi kama jiji linalosifika kwa mandhari yake ya kuvutia.

Lakini licha ya juhudi hizo zote, baadhi ya wadau, hasa Bw Sonko amekuwa akilalamikia kutengwa kwenye uendeshaji wa ajenda muhimu zinazohusu taratibu za uongozi wa jiji hili.

Ingawa Rais Kenyatta aliingilia kati na kusuluhisha baadhi ya tofauti zilizokuwepo kati ya Bw Sonko na Jen Badi, hali bado haijaonekana kulainika.

Bw Sonko angali analalamika kuwa shughuli zimenyakuliwa kutoka kwake kinyume cha sheria.

Kwa msingi huu, ni vyema serikali itafute jinsi ya kusuluhisha mapengo ya kisheria ambayo yanaweza kuifanya iendelee kuonekana kama utawala usiojali kuheshimu sheria za nchi.

Wito wetu ni kwa washikadau wote kujumuishwa kwenye harakati za kufufua jiji kuu, kwani hatua zote zinazochukuliwa zinawaathiri wakazi moja kwa moja na kukiwa na mizozo pia ni wakazi wanaoumia.

Lengo la viongozi lisiwe kujitafutia sifa kuhusu aliyefanikisha ustawi wa jiji dhidi ya aliyeshindwa, bali kuwe na lengo moja la kuboresha hadhi ya Nairobi.