Makala

TAHARIRI: Vijana wajihadhari na uraibu wa kamari

July 4th, 2020 2 min read

Na MHARIRI

MNAMO Jumanne wiki hii, Rais Uhuru Kenyatta alirejesha tabasamu kwenye nyuso za kampuni za kamari ya spoti alipofutilia mbali ushuru wa asilimia 20 ambao ulikuwa unazua mgogoro mkubwa wa kibiashara baina ya mashirika hayo na serikali.

Kuondolewa kwa kodi hiyo kunaweza kufasiriwa kama hatua ya serikali kuzikaribisha tena kampuni za kamari ya spoti zilizokuwa zimefunga biashara zao humu nchini kama vile SportPesa na Betin.

Kampuni hizo zilifunga biashara zikilalamikia aina nyingi za ushuru unaotozwa sekta hiyo ya bahati-nasibu zikisema hitaji hilo la serikali linazinyima faida.

Hatimaye Rais amesikiliza kilio cha kampuni hizo japo raia hawajajua kiini cha kuchukua hatua hiyo. Labda ni kwa sababu alitaka serikali ipate ushuru uliotoweka baada ya kampuni hizo kufunga biashara zayo mwaka 2019.

Ama yamkini kiongozi huyo wa nchi anazitaka kampuni hizo zirejee na udhamini wa michezo mbalimbali zilizokuwa zikitoa kwa sekta ya michezo kabla ya kujiondoa katika biashara hiyo.

Bila kujali nia ya Rais, ichukuliwe kuwa ana kusudio zuri kwa taifa lake.

Muhimu zaidi ni kutambua madhara ya kamari na kuwakinga raia wake hasa vijana dhidi ya kujitumbukiza ndani yake.

Mojawapo ya madhara ya mchezo huo ni kwamba ni rahisi sana kumpata mchezaji akigeuka mraibu.

Anapogeuka mraibu, mhusika huharibu pesa nyingi kwa kucheza akitarajia kuangukia bahati ila aghalabu huwa anapoteza.

Pesa hizo zinazopotea wakati mwingine huwa ni za kutunza familia. Kwa hivyo, anapozipoteza mafarakano hutokea katika familia.

Madhara ya pili ni visa vya kujiua na kutamauka maishani. Hili hutokea baada ya mchezaji kupoteza pesa, hasa kiasi kikubwa katika harakati ya kujaribu bahati. Kabla ya mashirika hayo kufunga biashara, visa vya kujiua vilikuwa vingi mno nchini.

Tatu ni kuwa vijana wanapojiingiza katika uraibu huo, huwa wanakosa kufanya kazi zinazoleta pesa kwa kutoa jasho na badala yake kupotelea kwenye pata-potea. Mwishowe taifa ndilo huhasirika maadamu nguvu za vijana hao zinahitajika katika kukuza uchumi.

Kwa sababu hizo kuu na nyingi nyinginezo, ni ushauri wetu kuwa kamari hii inaporuhusiwa kurejea, tuchunge raia wetu hasa vijana dhidi ya kuzama zaidi katika uraibu huu hatari.