TAHARIRI: Vijana wasitumiwe na viongozi kuzua fujo

TAHARIRI: Vijana wasitumiwe na viongozi kuzua fujo

KITENGO CHA UHARIRI

KISA ambapo msafara wa Kiongozi wa ODM Raila Odinga ulishambuliwa na vijana wanaodaiwa kukodiwa na wanasiasa hasimu katika mtaa wa Githurai wiki hii ni cha kuogofya mno.

Kadri joto na misimamo mikali inavyoanza kujitokeza kuhusu mchakato wa Marekebisho ya Katiba kupitia mpango wa maridhiano wa BBI ndivyo joto la kisiasa linapanda nchini. Ni wazi kwamba katika mchakato huu kutakuwa na pande mbili; mmoja unaounga na mwingine unaopinga.

Zipo dalili kwamba wakati ambapo kundi la Handsheki linaloongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM liko katika mstari wa mbele kupigia debe marekebisho ya Katiba, mrengo wa pili unaoongozwa na Naibu Rais William Ruto unapinga mpango huu.

Licha ya kutangazwa marufuku ya mikutano ya kisiasa kama njia mojawapo ya kukabili ueneaji wa maradhi ya Covid-19, wanasiasa wametoka mafichoni na sasa wanaonekana katika pembe mbalimbali za nchi wakichapa siasa. Mapuuza haya huenda yakatosa taifa katika wimbi la tatu la msambao mbaya zaidi wa corona kisha tujutie matendo ya sasa.

Jiji la Nairobi ndilo limeonekana kuwa kivutio kikuu kwa wanasiasa. Katika siku za hivi karibuni, Naibu Rais William Ruto na Kinara wa ODM Raila Odinga wameonekana kuzidisha mikutano ya kuonyeshana ubabe.

Majuma machache yaliyopita Raila alizuru soko maarufu la Burma na hapo Jumatano Naibu Rais alielekea huko kama mbinu ya kufuta yote yaliyosemwa na Raila. Maadamu Raila siku ya Jumatano alizuru maeneo ya Githurai na Roysambu, haitakuwa ajabu tumwone naibu Rais akielekea huko kuenda kukosoa alichosema Raila.

Hali ikiendelea hivyo, cha kutia hofu ni visa vya ghasia ambavyo vimeanza kuonekana wakati mibabe hawa wa siasa wanapopimana nguvu. Kushambuliwa kwa msafara wa Raila eneo la Githurai huenda kukachochea wafuasi wa Raila kumshambulia Ruto atakapozuru ngome ya Odinga.

Ongezeko la visa hivi litasababisha taharuki na kuzidisha chuki kati ya wafuasi wa vigogo hawa wa kisiasa. Hii ndiyo maana inawapasa viongozi hawa kuonyesha ukomavu wao kwa kukashifu visa vya ghasia na hasa wawashauri wafuasi wao wakome kushambulia misafara ya mahasimu wao.

Tahadhari kuu inafaa kuchukuliwa na vyombo vya usalama kuwanyaka wanaozua fujo ili ufikapo uchaguzi wa 2022 taifa hili lisitumbukie katika machafuko ya kisiasa.

You can share this post!

Mwendwa aidhinishwa kuwania nafasi ya haiba katika Baraza...

Bomba lililochakaa lasababisha uhaba wa maji Pwani