Makala

TAHARIRI: Vijana waufuate ushauri wa Rais

December 8th, 2020 2 min read

KITENGO CHA UHARIRI

KENYA inaelekea kwenye kampeni za kuamua kama nchi inataka mapendekezo ya kurekebisha sheria kupitia BBI au la.

Huu ni muda muafaka kwa kila mmoja wetu kuamua hatima yake, hasa vijana.

Kwa muda mrefu vijana ambao ni zaidi ya asilimia 70 ya Wakenya wote milioni 50, wamekuwa wakiishi kwa kuamini kuwa wao ni ‘Viongozi wa Kesho’. Ni kesho ambayo baadhi wameisubiri kwa zaidi ya miongo mitatu, na hali ilivyo kwa sasa, ni kama haitafika.

Katika kutambua ukweli huo, Rais Uhuru Kenyatta amewataka vijana waamke na kuchukua nafasi yao katika ujenzi wa taifa. Anawataka wajipange na kupigania nafasi za uongozi badala ya kutumiwa na wanasiasa wanaowachochea kupigana na kuwasahau wanapoingia mamlakani.

Hili limekuwa tatizo kubwa miongoni mwa vijana. Wengi unapofika wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, badala ya kubuni sera zao na kuuzia wapigakura, hutaka pesa za haraka kutoka kwa wanasiasa

Mara nyingi wanaopewa pesa hizo baadaye hupewa ulevi au kuingizwa chuki na kuwashambulia viongozi wengine kwenye mikutano ya kisiasa.

Vijana hubebeshwa marungu, mishale, mapanga na wakati mwingine kujihusisha na kurarua makaratasi ya kampeni ya wapinzani wa mabwana zao.

Huku ni kutumika vibaya, ambako husingiziwa umasikini na ukosefu wa ajira.

Wengine, badala ya kuwania, huketi na kusubiri kuteuliwa kuwa mawaziri au makatibu. Katiba inasema hakuwezi kuwa na mawaziri zaidi ya 24. Kenya ina zaidi ya vijana 30 milioni. Ni kigezo kipi kitakachotumiwa kuwateua angalau 12 kwenye Baraza la Mawaziri?

Isitoshe, marekebisho ya Katiba tunayopendekeza yanataka mawaziri watoke Bungeni na wachache wawe wataalamu kutoka nje. Rais hataweza kuteua kijana yeyote kuwa waziri. Ni sharti awe na utaalamu fulani, ambao lazima uandamane na uzoefu. Kwa mfano, itakuwa rahisi kwa kijana aliyejianzishia biashara ndogo na kuiendeleza, kuteuliwa waziri wa Biashara kuliko yule aliyeketi chini ya miti au kando ya barabara akisubiri msaada.

Kwa kujiunga na uongozi kupitia kura, vijana watakuwa na nafasi bora zaidi ya kuwa mawaziri na pia kuunda sera na sheria zitakazobadili mwelekeo wa nchi kiuchumi, kisiasa na kijamii.