Makala

TAHARIRI: Viongozi wachuje wasemayo vikaoni

September 9th, 2020 2 min read

Na MHARIRI

MNAMO Desemba 14, 1974, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio maalumu ambalo lengo lake lilikuwa kuwalinda akina mama na watoto wakati wa makabiliano na majanga.

Kimsingi, azimio hilo lilielezea wazi kwamba, wanawake na watoto hawapaswi, katika hali yoyote ile, kudhulumiwa au kukandamizwa iwe ni wakati wa vita au kwenye msukosuko wa aina yoyote.

Ni katika muktadha huo ambapo tunaungana na Wakenya wengine kukemea matamshi ya Mbunge wa Kipseret, Oscar Sudi, ambayo yalionekana kumshushia hadhi mamake Rais.

Kimsingi, hatulaani matamshi hayo kwa sababu mhusika ni mamake kiongozi wa taifa. La hasha. Tunakerwa na hatua ya Mbunge huyo kumhusisha mamake Rais kwenye malumbano ya kisiasa ambayo tunaamini mama huyo si mshirika kamwe.

Nchi hii imewahi kukumbwa na makabiliano ya kikabila, hali iliyochochewa na cheche za matusi na matamshi ya kuumbuana kama tuliyoona kwenye mitandao ya kijamii juzi.

Huenda Bw Sudi na wanasiasa wengine wakawa na sababu za kukerwa na hatua ya Rais kuonekana kumtenga naibu wake katika masuala ya uongozi wa nchi. Lakini hiyo kamwe si njia ya kuwasilisha malalamishi yao.

Wakati umewadia kwa Rais Kenyatta, Naibu Rais William Ruto na Kiongozi wa ODM, Raila Odinga, kuwaonya washirika wao dhidi ya kutoa matamshi ambayo yanaweza kupandisha joto la kisiasa na hatimaye kuzua mafarakano ya kikabila.

Inashangaza kwamba, miaka karibu miwili na nusu kabla ya uchaguzi mkuu kuandaliwa, wanasiasa wako mbioni kupiga kampeni za kisiasa kana kwamba kiti cha urais kiko wazi.

Yote hayo yanaendelea licha ya kwamba, maelfu ya Wakenya hawana kazi, wengi wamekosa chakula huku maafisa wachache serikalini wakiendelea na uporaji wa mali ya umma.

Isitoshe, viwango vya umaskini nchini vimefikia hatua ya kutisha na viongozi waliotwikwa jukumu la kutafuta suluhu kwa changamoto hizo wanapapurana hadharani. Hali hii haifai kamwe.

Siasa za chuki na matusi ni kiungo kikuu cha uhasama na hatimaye mapigano ya kijamii.

Hivyo basi, viongozi wote wanapasa kutafakari maneno wayatoayo vinywani mwao ili kuepusha hali ambapo taifa linaweza kuzama tena katika vurugu.