TAHARIRI: Viongozi wetu wachunge ndimi zao

TAHARIRI: Viongozi wetu wachunge ndimi zao

NA MHARIRI

MAJIBIZANO yanayoendelea kati ya viongozi wa kisiasa nchini kuhusu Uchaguzi Mkuu wa 2022, yanahatarisha kuvuruga hali ya amani ambayo imekuwepo miongoni mwa Wakenya.

Viongozi wameanza kukita majibizano yao kwenye masuala ya kikabila, bila kujali athari ambazo midahalo kama hiyo imeleta nchini hapo awali.

Majibizano hayo ambayo yamekuwepo kwa muda mrefu, yalizidi tangu Jumamosi, baada ya cheche za maneno zilizorushwa na wanasiasa katika mazishi ya mamake Kiongozi wa Amani National Congress, Bw Musalia Mudavadi.

Kwenye hafla hiyo, Rais Uhuru Kenyatta alikiri kwamba kati ya viongozi waliohutubu, karibu wote waliangazia siasa badala ya masuala muhimu kama vile maendeleo.

Lakini badala ya kuepuka siasa, naye akajitosa ndani na kutoa matamshi ambayo yalivutia hisia tele kimataifa, kuhusu makabila mawili ambayo yameongoza nchi tangu ilipopata uhuru.

Bila shaka, mwelekeo huu wa majibizano bila kujali athari za matamshi ndio umekuwa ukisababisha ghasia za kisiasa nchini kila baada ya miaka mitano tangu 1992, baada ya Kenya kurudisha mfumo wa vyama vingi vya kisiasa.Ghasia zilishuhudiwa katika miaka ya 1997, 2002, 2007, 2013 na 2017.

Upeo wa ghasia hizo ulikuwa 2007, baada ya Wakenya kugeukiana wao kwa wao kwa misingi ya kikabila.Ni hali iliyowafanya Wakenya sita, miongoni mwao wakiwemo Rais Kenyatta na Dkt Ruto kufunguliwa mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) jijini Hague, Uholanzi.

Ghasia zilizotokea 2017 pia ndizo zilimfanya Rais Kenyatta na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, kubuni handisheki ili kurejesha amani na utulivu wa kisiasa nchini.Ni kinaya kwamba tumeanza kuchukua mkondo huo huo, licha ya matukio ya awali.

Tumesahau yaliyotufika?Uchaguzi mkuu unapozidi kukaribia, wito wetu ni kwa viongozi kuwa waangalifu wanapotoa matamshi yao ili kuhakikisha hawajairejesha nchi kwenye enzi za giza.

Vile vile, wananchi wakome kushangilia matamshi ya matusi na uchochezi yanayotolewa na wanasiasa kila mara.Badala yake, wajizoeshe kufuata wanasiasa wanaojadili masuala ambayo yanaweza kuboresha maisha ya kila mmoja katika taifa hili.

You can share this post!

WANTO WARUI: Kuzuia wanahabari shuleni kunaficha maovu

Tangatanga wamzomea Uhuru kwa matamshi