TAHARIRI: Visasi na chuki ni vikwazo kwa nchi kuendelea

TAHARIRI: Visasi na chuki ni vikwazo kwa nchi kuendelea

NA MHARIRI

UONGOZI ni jukumu kubwa ambalo viongozi hutwikwa na wananchi.

Punde baada ya uchaguzi, huwa jukumu la waliochaguliwa kushirikiana serikali ya kitaifa pamoja na za kaunti, ili kufanikisha maendeleo kwa wananchi.

Maendeleo haya hupatikana tu iwapo watu watalenga mbele kama nchi moja, badala ya baadhi ya watu kuendelea kuuguza hisia kali.

Ni kweli kwamba kuna sehemu kubwa ya Wakenya ambao hawakufurahishwa na uamuzi wa Mahakama ya Upeo kuhusu matokeo ya urais.

Viongozi wakuu wa Azimio walieleza zaidi ya mara moja kuwa ingawa walitii uamuzi huo, hawakubaliani nao.

Pia ni kweli kwamba kuna maafisa wa umma waliokuwa na msimamo mkali dhidi ya Rais William Ruto na viongozi wa Kenya Kwanza kwa jumla.

Baadhi ya maafisa wa Utawala kama machifu na wakuu wa kaunti walikuwa mstari wa mbele kupigia debe kiongozi wa Azimio Raila Odinga.

Maafisa hao walikuwa tu wakifuata maagizo ya wasimamizi wao.

Kwa hivyo taarifa kwamba kuna maafisa wanaohangaishwa na wanasiasa wanaoegemea chama cha United Democratic Alliance (UDA) kwa kudhaniwa kuunga mkono mrengo fulani wa kisiasa kuelekea uchaguzi wa Agosti 9 ni za kuvunja moyo.

Chama cha Watumishi wa Umma Nchini (UKCS), kinadai kuwa maafisa wanaolengwa zaidi ni wa utawala. Maafisa hao kuanzia naibu chifu, chifu, naibu kamishna wa kaunti na makamishna katika kaunti, ni watu wanaotoa huduma muhimu kwa umma.

Kuwahangaisha na kuwawekea mazingira magumu ya kufanya kazi, kunaweza kuchangia utoaji duni wa huduma.

Wanasiasa na serikali huja na kuenda lakini watumishi wa umma husalia kama kiungo muhimu katika utekelezaji wa sera na utoaji huduma kwa umma.

Kwa hivyo, wafanyakazi wa umma hawafai kuhangaishwa na wanasiasa kwani hatua hiyo itawazuia kutekeleza majukumu yao ya utoaji huduma kwa wananchi.

Alipokula kiapo katika uwanja wa michezo wa kimataifa wa Moi, Kasarani, Rais Ruto alitangaza hadharani kwamba serikali yake haitakuwa ya kulipiza kisasi.

Kuwaandama maafisa wa serikali ambao hawakuunga mkono UDA ni kwenda kinyume na kauli ya rais.

Dkt Ruto anapaswa kuwakanya wanasiasa wanaowatisha watumishi wa umma.

Upande wa upinzani pia unapaswa kujua kwamba wakati wa siasa uliisha. Iwapo rais atahudhuria maeneo ya nchi kwa lengo la kujadili maendeleo, ni ishara nzuri wakijitokeza.

Kitendo cha jana Jumapili cha viongozi wakuu wa Homa Bay kuhepa ziara ya Rais Ruto ni mfano mbaya.

Hata kama hakuna sheria inayomlazimu kiongozi kuungana na rais, kuhudhuria ziara zake katika maeneo yao ni ishara ya ukomavu wa kisiasa.

You can share this post!

Mpira wa Vikapu: Kenya yaambulia patupu mashindano ya Red...

Ruto alenga ngome ya Raila kwa minofu

T L