Makala

TAHARIRI: Wabunge wajue umma umechoka

July 13th, 2019 2 min read

Na MHARIRI

ILIKUWA wiki iliyosheheni mihemko mingi hasa kutoka kwa wabunge ambao, kwa mara nyingine, wameamua kujiongezea marupurupu yao.

Katika kile kilichoacha Wakenya wengi mdomo wazi, watungaji sheria hao wamebuni marupurupu mapya; ya kulala jijini Nairobi wanapokuwa katika shughuli za kikazi, jambo lililokashifiwa vikali kwa kutofikiria jinsi marupurupu hayo yatakavyokuwa mzigo mzito kwa umma.

Kuna shida mbili katika mapendekezo ya marupurupu haya ambayo Wabunge wamekuwa wakifanya katika siku za hivi punde

Moja na ya wazi ni kwamba Katiba inasema nyongeza yoyote ya marupurupu au mishahara ya wabunge inafaa kuanza kutekelezwa kwa wabunge wajao, wala sio waliopo.

Kwa maana kwamba, mapendekezo wanayofanya sasa hayapaswi kuanza kulipwa moja kwa moja bali ni baada ya bunge jipya kuchaguliwa uchaguzi mkuu ujao.

Tatizo la pili ni kwamba taifa linapitia wakati mgumu mno kiuchumi.

Biashara nyingi zimeathirika na wengi wanasaka kazi ambazo hazipatikani huku mamilioni wakitapata wakati mgumu hata kupata chakula cha kila siku.

Takribani kila mtu amefunga mshipi kujaribu kutumia raslimali chache zilizopo.

Iweje viongozi hao hawahisi wala kutambua ugumu huu wa maisha?

Baadhi ya waliotetea hatua hiyo ya kujiundia marupurupu mapya wamesema kwamba wanasumbuliwa na wakazi katika maeneo wanakotoka, kwamba wakazi wanawasimamisha njia kila mara wakiomba pesa au misaada mbalimbali.

Walisema tabia ya Wakenya kuombaomba huwaacha wakiwa hawana hata peni mfukoni.

Ni kweli, hulka hiyo haipingiki.

Na kadri uchumi utakavyoendelea kuzorota ndivyo wakazi wengi watakita kambi katika makazi ya viongozi waliowachagua.

Kile wabunge wanachofumbia macho ni kwamba mojawapo ya sababu ya kuzuka kwa ombaomba hao ni tatizo lile lile la uchumi ulio mbaya, uliosababishwa na ufisadi usiomithilika na sera mbovu ambazo wao kama watetezi na waangalizi wa umma wamekosa kushughulika ipasavyo kukabili.

Umefika wakati kwa viongozi hao waliochaguliwa na umma kuketi chini na kufikiria kwa kina nchi ambayo wanataka kuiunda kwa sababu jinsi wanavyoendelea na juhudi za kujiletea manufaa ya kibinafsi tutashtukia nchi imeliwa ikaisha.