MakalaSiasa

TAHARIRI: Wabunge warudishe mamilioni waliyomumunya Amerika

August 12th, 2019 1 min read

NA MHARIRI

KAMA alivyosema gavana wa Machakos, Dkt Alfred Mutua, wabunge hawana budi kushinikizwa kurejesha fedha za umma walizotumia katika ziara ya Amerika.

Idadi kubwa ya wabunge walioelekea nchini Amerika ni ithibati kwamba walikuwa wameenda likizo.

Ziara hizo zisizokuwa na manufaa kwa walipa ushuru ndizo zimefanya gharama ya kuendesha mabunge ya kaunti kuwa juu.

Awali serikali ilikuwa imepiga marufuku idadi kubwa ya watu kuhudhuria kongamano moja na hasa nje ya nchi kutokana na gharama ya usafiri na marupurupu wanayolipwa.

Kuna sera ya serikali inayodhibiti idadi ya watu wanaofaa kuhudhuria kongamano moja.

Lakini hata baada ya serikali za kaunti kuandikiwa barua zikitakiwa zisitume zaidi ya watu watatu katika kongamano, bunge linatuma watu 100.

Mbali na wabunge, wengine waliosafiri ni maseneta, madiwani na wafanyakazi wa bunge.

Inakadiriwa kuwa Wakenya walipoteza zaidi ya Sh100 milioni katika ziara hiyo na hilo ni jambo la kutamausha kwa kweli kwa sababu zigo la kulipa ushuru limewaelemea raia wengi, hasa wenye mapato ya chini na ambao wana utashi mkubwa wa huduma bora kutoka kwa serikali.

Haya yanajiri wakati ambapo gumzo lililotanda kote nchini ni kuhusu gonjwa hatari la saratani linaloendelea kuangamiza Wakenya kila uchao.

Badala ya mabunge kuyapa kipaumbele maswala kama haya wanajipa raha wao kwa safari zisizomfaa mwananchi wa kawaida.

Viongozi wanapaswa kuiga baadhi ya magavana wanaotumia mgao wa pesa za kaunti zao kuimarisha afya ya wakazi na huduma nyinginezo.

Tayari Wakenya wana matatizo ya kutosha na sasa ni wakati mwafaka wa serikali kuchukua hatua kuhakikisha inadhibiti ulafi wa wabunge.

Tusipoziba ufa tutaujenga ukuta na itakuwa gharama ya juu zaidi kwa vizazi vijavyo, ambavyo maisha yatakuwa magumu sana kwao.