Makala

TAHARIRI: Wadau wafanye hima kuiokoa voliboli nchini

March 30th, 2019 2 min read

Brackcides Agala (kulia) na Evelyne Makuto wakiichezea Kenya Pipeline . Picha/ Maktaba

Na MHARIRI

MATOKEO duni yaliyosajiliwa na wawakilishi wa Kenya katika kampeni za kuwania umalkia wa Klabu Bingwa Afrika (CAVB) zilizokamilika jijini Cairo, Misri wiki jana yanavunja moyo.

Fahari ya pekee katika fainali hizo ni kwamba refa Lucy Chege kuingia katika mabuku ya historia kwa kuwa mwamuzi wa kwanza wa kike kutoka Kenya kuwahi kupuliza kipenga katika mapambano ya Klabu Bingwa barani.

Kwa upande mwingine, ni fainali ambazo zilifichua jinsi ambavyo viwango vya mchezo wa voliboli vinashuka kwa kasi humu nchini.

Kenya Prisons na wanabenki wa KCB waliambulia pakavu katika kivumbi hicho huku Kenya Pipeline ambao walitia fora zaidi, wakizidiwa maarifa kwenye hatua ya nusu-fainali.

Vipusa hao wa kocha Margaret Indakala walitwaa nishani ya shaba baada ya kuwachabanga GSP ya Algeria kwa seti 3-0 kwenye mchuano wa kutafuta mshindi wa nafasi ya tatu na nne. Miamba wa Misri, Al Ahly walifanikiwa kulitetea taji hilo baada ya kuwazidi maarifa Carthage kutoka Tunisia kwa seti 3-1 (21-25, 25-15, 25-11,25-19).

Chini ya mkufunzi Japheth Munala, KCB iliyowachabanga Revenue Authority ya Rwanda seti 3-0 (25-15, 25-13, 25-11) iliambulia nafasi ya tisa huku Prisons iliyobanduliwa kwenye makundi ikikokota nanga mkiani katika nafasi ya 17.

Tunahisi kwamba ipo haja kwa Shirikisho la Voliboli Nchini (KVF) kukutana na makocha na wachezaji wa zamani wa mchezo huo ili kubuni mikakati kabambe itakayorejesha Kenya kwenye ramani ya voliboli kimataifa.

Ilivyo, huenda ikawa vigumu kwa vikosi vya voliboli hapa Kenya kufikia viwango vya wapinzani wao kutoka Kaskazini na Magharibi ya Afrika iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa na vinara wa KVF kwa ushirikiano na wakufunzi wa voliboli.

Timu za Afrika Kaskazini zina mbinu bora zaidi za kuwanolea wachezaji wao. Pia zinajivunia vifaa vya kila sampuli ambavyo vimewezesha vikosi vya sehemu hizo kuwatamalaki wapinzani wao kwingineko barani.

Upekee wa timu hizo ni mfumo wao wa kushirikisha kasi katika mechi zao na kuwazima wapinzani haraka iwezekanavyo kabla wajipange mchuanoni.

Huu ni mkakati ambao unastahili pia kuandamwa na timu za voliboli kutoka humu nchini.

Licha ya Pipeline kuridhika na medali ya shaba, mwanavoliboli wao Esther Mutinda alionekana kutia fora, na anapigiwa upatu kushirikiana vilivyo na Janet Wanja ili kuwatambisha vipusa wa timu ya taifa Malkia Strikers katika kampeni zijazo za kufuzu kwa Olimpiki za Tokyo, Japan mnamo 2020.

Ingawa hakushiriki mechi nyingi, Esther alidhihirisha sifa za kuwa miongoni mwa wanavoliboli wa haiba kubwa kuwahi kutokea humu nchini katika siku zijazo.

Aidha, Sharon Chepchumba wa Pipeline alitawazwa Mfungaji Bora mwishoni mwa kampeni hizo za CAVB jijini Cairo, Misri. Mvamizi huyo wa kushoto alibanduka kambini mwa Prisons mapema mwaka 2019.