Makala

TAHARIRI: Wadau washirikiane kufanikisha mitihani

October 9th, 2018 2 min read

NA MHARIRI

KAULI ya Wizara ya Elimu kwamba wazazi ndio watakaowajibika ikiwa wanao watapatikana wakijihusisha na udanganyifu wa mitihani ya kitaifa ya Darasa la Nane (KCPE) na Kidato cha Nne (KCSE) ni ya kuridhisha.

Ni tangazo linalopaswa kuungwa mkono na kila mmoja, ikizingatiwa kwamba kwa muda mrefu wanafunzi wamekuwa wakibebeshwa mizigo ambayo si yao. Wale ambao huwasaidia kujihusisha vitendo vya udanganyifu aghalabu huwa wanasazwa katika mchakato wa utoaji adhabu kwani wanafunzi husika ndiyo huwajibika.

Wizara pia imetangaza kwamba wakati wa mitihani hiyo, wazazi hawataruhusiwa kuwatembelea wanao- hasa wanaosomea katika shule za mabweni. Kimsingi, hii ni hatua nzuri katika kukabili visa hivyo, ila pia pana haja ya mashauriano zaidi.

Kwanza, kuwazuia wanafunzi kuonana na wazazi ama walezi wao huenda isiwe hatua ya busara kwani kuna baadhi ya hali ambazo hutokea na huhitaji uwepo wao. Katika muda huo wa mitihani, baadhi ya wanafunzi huugua au huhitaji dharura fulani maalum ambazo mzazi ama mlezi wake ndiye pekee anazielewa.

Baadhi ya wanafunzi pia hukumbwa na maradhi ya ghafla kama kifafa, hali ambazo usimamizi wa shule wanamosomea huenda ukashindwa kuelewa. Kwa hali kama hizo, si busara kwa Waziri wa Elimu Amina Mohamed kutoa uamuzi huo bila ushirikishi ufaao wa wadau husika.

Hofu kuu inatokana na hali kwamba si mara moja tumesikia visa vya wanafunzi waliougua na kufariki katika hali tatanishi, baada ya uongozi wa shule wanamosomea kutoshughulikia hali zao za kiafya.

Katika baadhi ya matukio, wanafunzi hufikishwa hospitalini wakiwa wamechelewa au hata kupewa dawa zisizofaa, hivyo kuhatarisha hali zao zaidi.

Ili kuepuka matukio kama hayo, wizara inapaswa kulegeza kamba kuhusu agizo lake ili kutoa mwanya wa kushughulikia hali maalum zitakazowakumba wanafunzi. Mojawapo ya mikakati inayopaswa kuwekwa ni wizara kuwaagiza maafisa wake wanaosimamia shule mbalimbali ama vituo vya mitihani kunakili wanafunzi ambao watahitaji hali zozote za dharuta mitihani hiyo ikiendelea.

Hilo litabuni ushirikiano mzuri ambao utahakikisha kuwa pande zote mbili zinashirikiana kwa manufaa ya wanafunzi, ila si kuwaumiza.