Makala

TAHARIRI: Wafisadi wasipewe masharti magumu

October 24th, 2019 2 min read

Na MHARIRI

SIKU ya Jumanne Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Bw Noordin Haji alikuwa mjini Kisumu ambapo alidokeza kuwa watu maarufu wanaohusishwa na ufisadi wameomba wakiri makosa ili warejeshe mali.

Miongoni mwa watu hao, wapo waliokuwa maafisa wa umma waliotumia vibaya mamlaka yao na kujilimbikizia mamilioni ya pesa za mlipa ushuru.

Kupitia mpango huo, watuhumiwa watakiri makosa, waombe radhi kisha waandikishiane na afisi ya DPP kuhusu jinsi wanavyopanga kurejesha pesa hizo.

Huu ni mpango mzuri ambao sio tu utawavutia washukiwa wengi, bali pia utakuwa na faida kwa mwananchi, ikizingatiwa kuwa mtu anapofungwa, kwa njia moja au nyingine, serikali haifaidiki kivyovyote.

Lakini mpango huu sharti utekelezwe kwa njia ya uwazi na uwajibikaji mkuu.

Kwa kuwa mali yaliyoibwa ni ya umma, afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma inalazimishwa na Katiba kutekeleza uwazi. Yapaswa itangaze majina hayo hadharani, iseme ni akina nani waliojitokeza kutaka msamaha ili warejeshe waliochoiba. Kisha makubaliano yao pia yafaa kuwekwa wazi, ili iwapo wataamua kuwa hawalipi kama walivyokubaliana, mwananchi ajue.

Afisi ya DPP inashikiliwa kwa niaba ya umma. Litakuwa jambo la busara iwapo itafanya shughuli zake kwa kuuhusisha umma, kwa njia ya taarifa zenye maelezo ya kina.

Uwazi pekee hautoshi. Wakenya wanatarajia kuona uwajibikaji wa hali ya juu. Mtu anaweza kujitokeza na kudai kuwa yupo tayari kulipa mali aliyoiba ilia pate msamaha nje ya mahakama.

Atakapokubaliwa, yafaa kuwe na njia ya kufuatilia na kuhakikisha kwamba anatimiza ahadi yake kulingana na makubaliano.

Isitoshe, kusema kwamba mbali na kurudisha mali kuna adhabu ya kifungo kisichopungua miezi sita, kunaweza kuwafanya watu wengi walioiba mali ya umma waogope kujitokeza.

Iwapo serikali kufikia afisi ya DPP inatarajia kupata ufanisi katika kurejesha mali ya umma iliyoibwa, kuna haja ya kuangalia upya kanuni za msamaha huo, ili atakayerejesha asamehewe bila ya pingamizi zozote. Kwa kufanya hivyo, watu wengi watakuwa tayari kutafuta msamaha huo na kurudisha walichojipatia kwa njia isiyo halali.

Afisi ya DPP pia yapaswa kutafuta ushauri wa mara kwa mara kutoka kwa wadau wengine, ambao huenda wakawa na maelezo yanayoweza kuidadiai kutekeleza jukumu hili kwa uadilifu.