TAHARIRI: Wagombeaji wajiepushe na mbinu chafu za uchochezi

TAHARIRI: Wagombeaji wajiepushe na mbinu chafu za uchochezi

NA MHARIRI

WAGOMBEA wa viti mbalimbali jana walimiminika makanisani kwenda kuombewa huku wakiahidi kudumisha amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa kesho Jumanne.

Mgombea urais wa chama cha UDA William Ruto na mpinzani wake mkuu Raila Odinga wa Azimio la Umoja, walikuwa kati ya wawaniaji waliohimiza Wakenya kudumisha amani.

Dkt Ruto alipokuwa akihutubu katika Kanisa la Jesus Teaching Ministry mtaani Kayole, alihimiza Wakenya kudumisha amani kesho na baada ya kutangazwa kwa matokeo.

Wandani wake wakiongozwa na kiongozi wa chama cha ANC Musalia Mudavadi, pia walikariri wito huo wakisema, ‘mtu anayedumisha amani hupata kibali cha kuitwa binti au mwana wa Mungu’.

Naye, Bw Odinga aliyehudhuria ibada katika Jumba la KICC jijini Nairobi, aliahidi kuhakikisha kuwa mrengo wake wa Azimio unadumisha amani.Miito ya amani pia ilitolewa katika maeneo mbalimbali ya nchi na wagombea mbalimbali.

Kwa mfano, wawaniaji sita wa ubunge katika eneobunge la Turbo, Kaunti ya Uasin Gishu, walizika tofauti zao za kisiasa na kushiriki ibada pamoja katika Kanisa la AIC Kiplombe.

Kila uchaguzi unapokaribia wagombea hutoa miito ya aina hii lakini baada ya kuondoka makanisani au majukwaa ya kisiasa wanafanya kinyume.

Wanasiasa hao hao wanaotaka kuwepo kwa amani hufadhili makundi ya vijana kuzua rabsha, kujihusisha na ununuzi wa vitambulisho, kuhonga wapigakura katika foleni, kusambaza vijikaratasi vya chuki na kuhimiza wafuasi wao ‘kulinda kura’.

Licha ya mambo hayo kupigwa marufuku na Sheria ya Uchaguzi, wahusika huwa hawachukuliwi hatua hivyo kuwapa motisha ya kuendelea kukiuka.

Majaribio ya udanganyifu huchangia pakubwa katika kuzuka kwa vurugu na umwagikaji wa damu katika vituo vya kupigia kura.

Vijikaratasi vya chuki husababisha mapigano baada ya kutangazwa kwa matokeo.

Lengo la vyama vya kisiasa kuwa na maajenti ndani ya kituo cha kupigia kura ni kuhakikisha kuwa kuna uwazi.

Hivyo, hakuna haja ya makundi ya vijana wanaofadhiliwa na wanasiasa kungojea nje ya vituo kwa kisingizio kwamba wanalinda kura.

Hivyo, miito ya amani iliyotolewa jana Jumapili na wanasiasa makanisani lisiwe domo – wanasiasa wahakikishe kuwa wanajiepusha na mambo ambayo huenda yakasababisha ghasia nchini.

Kila mgombea ajitayarishe kukubali matokeo ya uchaguzi wa kesho Jumanne kwani asiyekubali kushindwa si mshindani.

Maafisa wa usalama hawana budi kukabiliana na mgombea yeyote atakayevuruga imani bila kuzingatia mrengo wa kisiasa.

  • Tags

You can share this post!

Wavuvi Lamu sasa kushiriki uchaguzi

Mwongozo kusaidia wanahabari wa kike kukabili unyanyasaji...

T L