Makala

TAHARIRI: Wakati wa kuwalinda wanahabari ni sasa

October 18th, 2018 2 min read

NA MHARIRI

KATIKA siku za hivi majuzi, visa vya kusikitisha ambapo wanahabari wamekuwa wakishambuliwa vimekithiri zaidi humu nchini.

Kisa cha karibuni zaidi kilijiri mnamo Jumanne katika bunge la Kaunti ya Nyandarua ambapo wanahabari wanne walishambuliwa na maafisa wa usalama wa bunge hilo na kujeruhiwa.

Mwezi Septemba, itakumbukwa vyema nusra mwanahabari wa Nation Media Group (NMG) auawe katika eneo la Kisumu akijaribu kufuatilia sakata ya mapenzi iliyohusisha kigogo wa kisiasa katika mkoa wa Nyanza.

Muda si mrefu sana tangu wanahabari wa Nation wavamiwe na hata kutupwa ndani na polisi walipokuwa wakijaribu kufuatilia kisa cha unyakuzi wa ardhi ya umma ufuoni ili kujenga hoteli katika eneo la Mombasa.

Kwa ufupi hakuna mwezi unaopita bila kusikia visa vya wanahabari kuvamiwa, kujeruhiwa na hata kuuawa wanapotekeleza majukumu yao kitaalamu.

Sharti wadau wote wahusika wakiwemo serikali, vyama vya wanahabari, vyama vya wafanyakazi, watunga sera, watetezi wa haki za kibinadamu na umma kwa jumla wachukue hatua ya kuzuia dhuluma hizi dhidi ya wanahabari maadamu bila wataalamu hawa kupewa uhuru wao, wananchi hawatapata haki yao ya kuzipata habari hasa zile muhimu zinazogusa maisha yao kwa njia ya moja kwa moja.

Imebainika kuwa wahuni wanaotekeleza unyama huo huwa wana njama fiche ambayo hawataki umma au mkono wa sheria kuifahamu.

Lakini cha kusikitisha hata zaidi ni kwamba baadhi ya uhayawani wanaotendewa wanahabari hufanywa na maafisa wa polisi au walinda usalama wengineo.

Ni wakati muafaka wa serikali kwa ushirikiano na mashirika ya habari pamoja na vyama vya wanahabari kubuni mkakati wa kuwalinda wanahabari wanaoonekena kuwa katika hatari ya kuumizwa kila wanapotekeleza wajibu wao.

Sharti vyombo vya habari vihakikishe kuwa wafanyakazi wao wenye majukumu ya kufichua sakata au wanaohusika na upelelezi wanapewa ulinzi wa kutosha ili wasije wakadhurika na watu wenye hila.

Wale wanaoumizwa na watu wanaoweza kujulikana kwa urahisi wasaidiwe kuwatambua wenye hila ambao wanastahili kushtakiwa na kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria.