TAHARIRI: Wakati wa serikali mpya kuinusuru soka ni sasa

TAHARIRI: Wakati wa serikali mpya kuinusuru soka ni sasa

NA MHARIRI

MATUKIO yaliyoshuhudiwa wiki hii yametumbukiza wadau wa soka nchini katika giza, mtafaruku, mashaka na hofu kuu kuhusu ni upi ndio mwelekeo na hatima ya spoti hii maarufu zaidi duniani.

Mnamo Jumanne, Rais wa Shirikisho la Soka Nchini (FKF) Nick Mwendwa, alirejea kwenye ofisi yake na kutoa ahadi kwamba atarejesha mchezo wa kandanda katika hali inayofaa kwa kuzungumza na Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) ili iweze kuondoa marufuku yake kwa nchi ya Kenya.

Vivyo hivyo, aliahidi kwamba, atakutana na wasimamizi na wadau wa Ligi Kuu ya Taifa (KPL) ili kurejesha na kuzindua msimu mpya karibuni.

Hata hivyo, rais huyo aliweka wazi kwamba FKF haitambui matokeo ya mechi ambazo haikusimamia tangu iondolewe kwenye usukani mwezi Novemba 2021. Kwa ufupi Mwendwa alimaanisha kuwa ataendeleza spoti hii kutoka mahali alikoiachia kwa kuwa yeye bado ndiye aliyekuwa rais hasa kwa sababu hakuna yeyote aliwahi kuchukua nafasi hiyo tangu aondolewe ofisini.

Kabla ya matamshi ya Mwendwa kutulia vichwani mwa Wakenya, siku hiyo hiyo waziri wa Michezo Amina Mohamed alijibu kwa kusema kwamba Rais huyo kamwe hakuwa na ruhusa kirasmi kurejea ofisini humo kwa kuwa Kamati ya Mpito bado ndiyo ilikuwa ikisimamia shughuli za soka nchini.

Na katika hali hii ya vuta nikuvute, siku iliyofuata Vuguvugu la Klabu zinazoshiriki ligi ya KPL lilitangaza wazi kwamba hazitashiriki mechi zozote hadi marufuku ya Fifa yaondolewe.

Kwa ufupi, kundi hili lilielekea kumaanisha kwamba halitafuata maagizo yoyote kutoka kwa uongozi wowote hadi mzozo kuhusu marufuku ya Fia uondolewe kabisa.

Ingawa ombi la vuguvugu hili lilionekana kupata jibu kutoka kwa Rais Mwendwa kwa kuzingatia ahadi zake alizokuwa ametoa siku iliyotangulia, mambo yaligeuka kuwa mazito zaidi Mwendwa aliposhtakiwa upya na kutakikana afike katika mahakama ya Kiambu Jumatatu.

Hii ni baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali ombi lake la kuzima hatua ya DPP kumshtaki kuhusiana na wizi.Fahali wawili wapiganapo nyasi ndizo huumia kama Waswahili walivyonena.

Tumesema mara kadha kuwa vijana a nchi hii ndio wanaumia kwenye mivutano hii ya kila mara.

Hili kuondolea chipukizi mahasla hali hii ya kutamausha, Rais Williama Ruto anafaa kutimiza ahadi yake kwa wanamichezo iliyoko kwenye manifesto yake na kulainisha spoti hii bila kusita.

Kwa dharura Rais amteue waziri wa michezo mwenye maono atakayeteua au kurejesha Rais wa FKF ambaye atazungumza na Fifa faraghani ili kumaliza mzozo huu ili vijana wetu wapate amani katika ukuzaji wa talanta zao katika soka.

You can share this post!

DOUGLAS MUTUA: Tamaa ya kutajirika haraka imevuruga sifa...

Vinono bungeni vyapasua ODM

T L