Makala

TAHARIRI: Wakulima wapewe mawasiliano kisasa

November 24th, 2020 2 min read

KITENGO CHA UHARIRI

KWA muda mrefu sasa, kumekuwa na aina tofauti za uvumbuzi wa kitekinolojia zinazolenga kusaidia wakulima katika njia mbalimbali.

Mojawapo ya uvumbuzi ambao unaendelea kupata umaarufu kote nchini ni kuhusu utumizi wa tekinolojia za mawasiliano kupata mashauri ya kitaalamu kuhusu kilimo.

Licha ya haya, bado kuna wakulima katika pembe tofauti za nchi ambao hulalamika kukosa ushauri wa wataalamu katika shughuli zao wa kilimo na ufugaji.

Mfano ni katika Kaunti ya Mombasa, ambapo imebainika kuna wakulima wanaolalamika kutopata ushauri wa maafisa wa kilimo wa serikali.

Mbinu hiyo ya kusubiri maafisa wa serikali kutembelea shamba moja hadi nyingine ili wachunguze mashamba na kutoa ushauri bado ni muhimu, lakini imepitwa na wakati.

Katika enzi hizi, inafaa wakulima wahamasishwe kuhusu tekinolojia zilizopo ambazo nyingine hata hazihitaji ujuzi mwingi kutumia kupata ushauri wowote wa kitaalamu wanaohitaji.

Changamoto mbalimbali ambazo zilikumba mbinu ya jadi ya kusubiri washauri kutembelea mashamba ndizo zilisababisha watu na mashirika kuvumbua mbinu za kisasa, ambazo nyingi zinahitaji tu mtu kuwa na simu ya rununu.

Mojawapo ni kuwa, ongezeko la watu limefanya idadi ya wakulima kuongezeka na hivyo basi ni vigumu kupata maafisa wa kutosha wa serikali kutembelea kila shamba mara kwa mara.

Pili, idadi ya maafisa wanaohusika katika kazi hiyo imeendelea kupungua kadri na jinsi miaka inavyosonga.

Kutokana na kuwa kilimo ni jukumu ambalo liko chini ya serikali za kaunti kwa mujibu wa katiba, itakuwa vyema kama serikali hizo zitawekeza katika uvumbuzi wa tekinolojia za mawasiliano kwa wakulima, au ziwekeze katika kuwezesha wakulima kutumia tekinolojia zilizopo.

Baadhi ya tekinolojia hizo ziko chini ya mashirika ya serikali kuu kwa hivyo huenda ikawa kinachohitajika ni hamasisho kuzihusu kwa wakulima.

Wakati wadau wanapozungumzia kilimo cha kisasa wasiweke mawazo yao kwa mbinu za uzalishaji pekee bali pia watilie maanani tekinolojia hizi ambazo ni muhimu sana kwa wakulima.

Kwa kutumia mbinu za kisasa kupokea ushauri, mkulima huwa na uwezo wa kupata ushauri wa wataalamu tofauti wa kuaminika kuhusu masuala mengi kwa muda mfupi.