Makala

TAHARIRI: Walinzi wote wakaguliwe kabla ya kupewa bunduki

February 4th, 2019 2 min read

NA MHARIRI

WALINZI wa kibinafsi wanatekeleza jukumu muhimu la kulinda mali hapa nchini.

Katika nyumba za makazi, biashara na shughuli nyingine muhimu, walinzi hawa huwa wanahakikisha kuwa wahalifu hawaibi au kusababisha hasara.

Afisi nyingi mijini na vijijini hulindwa, hasa nyakati za usiku wenye mali wanapokuwa wamelala raha mstarehe.

Kumekuwa na matukio mbalimbali ambapo wezi na wahalifu wanapovamia maeneo kama vile shule, benki au makazi ya watu, huwafunga walinzi kwa kamba kabla ya kutekeleza wizi. Wakati mwingine walinzi hao huuawa.

Kwenye tukio la majuzi katika hoteli ya Dusit jijini Nairobi, walinzi waliokuwa wakishika doria waliuawa na magaidi.

Punde baada ya tukio hilo , kulizuka hoja kuhusu iwapo maafisa hao wanastahili kupewa bunduki au la. Mwenyekiti wa bodi ya Kusimamia walinzi wa Kibinafsi, Bw Fazul Mohamed, alitoa rai kuwa walinzi hao wa kibinafsi wapewe silaha sawa na maafisa wa polisi.

Walinzi kama hao wamekuwa wakipewa silaha katika mataifa mengi, ikiwemo nchi jirani ya Uganda. Hata hivyo, umeibuka mjadala kuhusu iwapo hapa Kenya wananchi watakuwa salama mikononi mwa walinzi hao.

Sababu kubwa inayofanya wengi kupinga jambo hilo, ni tabia ya Wakenya kupenda kutumia nguvu kujipatia riziki. Walinzi wengi wa kibinafsi wanafanya kazi katika mazingira duni, baadhi wakiwa hawana hata vibanda ambapo wanaweza kujikinga mvua au jua.

Wengi wao au karibu wote, hupokea mshahara duni, kiasi kwamba hawana uwezo wa hata kukidhi mahitaji yao muhimu.

Ikizingatiwa kuwa jamii yetu imekuwa na watu wengi walio na upungufu wa maadili, kuwapa walinzi hao silaha kunapingwa na wengi. Ikiwa baadhi ya polisi wamehusishwa na kukodisha silaha zao kwa majambazi, sembuse walinzi hawa?

Pendekezo la kuwapa silaha huenda likawa na manufaa kwa walinzi hao kujilinda dhidi ya majambazi, lakini pia yafaa wapigwe msasa na Idara ya Jinai (DCI), ili kufahamu rekodi zao kuhusu uhalifu.

Bali na kuwapiga msasa, walinzi hao yafaa wapewe mafunzo maalum ya kijeshi, ili wawe wanaweza kukabiliana na hatari wakati wowote.