Maoni

TAHARIRI: Walioathiriwa na majeshi ya Uingereza wapewe haki

May 30th, 2024 2 min read

NA MHARIRI

KAMATI ya Bunge kuhusu Ulinzi, Ujasusi na Masuala ya Kigeni inapoendelea kuchukua maoni ya wakazi wa kaunti za Samburu na Laikipia ili kuamua kuhusu kurefusha mpango wa majeshi ya Uingereza kuendesha mafunzo kwa miaka mingine mitano nchini, suala la haki na fidia linafaa kupewa kipaumbele.

Visa vya unyanyasaji na ukiukaji umeripotiwa kushuhudiwa maeneo hayo vikidaiwa kusababishwa na majeshi hayo ya Uingereza na kufikia sasa, waathiriwa hawajapata fidia.

Kuna madai kwamba, kando na wale wanaouguza makovu ya majeraha waliyopata, kuna wale wanaodaiwa kupoteza maisha yao mikononi mwa wageni hao.

Mojawapo ya matukio hayo ni mauaji ya msusi Agnes Wanjiru ambaye anadaiwa kuuawa mwaka wa 2012 na mwanajeshi wa kigeni aliyekuwa akipokea mafunzo.

Kuna kisa kingine cha moto ambao ulichoma ranchi ya Lolldaiga, Laikipia mwaka 2021 na baadhi ya wakazi kupata maradhi kutokana na athari za moshi.

Linaloshangaza ni kwamba, licha la matukio hayo kuwafika wahanga hao, serikali bado haijasema lolote kuhusu fidia au haki za Wakenya hao walionyanyaswa.

Ingawa familia ya Wanjiru inaendelea kusononeka, miaka 12 baadaye hakuna lolote ambalo limefanyika.

Inasikitisha kwamba mwenye ranchi ya Lolldaiga alifidiwa huku wakazi walioathirika wakipuuziliwa mbali na kusahaulika. Jambo hili linadhihirisha maantiki ya wenye nguvu mpishe na ‘mnyonge hana haki’ imani ambazo zinafaa kulaaniwa kwa vinywa vipana.

Kinaya ni kwamba, ingalikuwa maovu hayo yalitendewa wageni hao nchini mwao adhabu ingalikuwa kubwa na ya kifani kisichomithilika.

Wabunge sasa wana nafasi nzuri ya kusikiliza na kutathmini maoni, kilio cha wakazi hao wanaoshi maeneo ya Doldol na Archers Post ambao kwa hakika wanajua fika ukweli kuhusu matukio wanayopitia kila siku na kabla ya kurefusha mpango mwingine wa miaka mitano kwa wanajeshi hao wa kigeni.

Ingawa mwenyekiti wa Kamati hiyo Newton Koech ametoa hakikisho kwamba familia ya Wanjiru itapewa haki kabla ya mkataba mwingine wa ushirikiano kati ya Uingereza na Kenya, utekelezwaji unafaa kuonekana ukianza mara moja, isiwe ni ahadi hewa za maneneo matupu bila matendo.