Makala

TAHARIRI: Waliohamia shuleni wasaidiwe kuondoka

December 30th, 2019 2 min read

Na MHARIRI

HUKU ikiwa imesalia wiki moja kabla shule zifunguliwe, imebainika kuna shule nyingi ambazo bado ni makao ya watu waliohama wakati wa mafuriko yaliyotanda mwezi mzima Desemba.

Wakati wa msimu wa mvua iliyopitiliza Desemba, maelfu ya watu walipoteza makao yao wakalazimika kutafuta maeneo salama.

Wengi wao walihamia katika shule pembe tofauti za nchi walizogeuza kuwa makao yao ya muda.

Kufikia sasa, bado mvua inazidi kunyesha na kuhangaisha wananchi sehemu tofauti za nchi, huku wale walioathirika awali wakiwa bado hawajapata misaada ya kutosha.

Kando na mafuriko, kuna pia wale ambao walilazimika kuhama kufuatia maporomoko ya ardhi ambayo yaliharibu maboma yao na hata kusababisha maafa.

Ijapokuwa awali kulikuwa na wahisani wengi waliojitokeza kusaidia waathiriwa hao, ripoti zinaonyesha wangali wapo wengi wanaohitaji makao mapya.

Kuna wale ambao wanahitaji tu kuwezeshwa kifedha au wapewe vifaa vya ujenzi kurejea kwao, na pia kuna wale ambao bado hawaezi kurudi kwao kwa vile hali ya hewa ingali mbovu.

Inafaa idara husika za masuala ya majanga zijitokeze kusaidia watu hawa haraka iwezekanavyo.

Wanaohitaji vifaa vya ujenzi wapewe, na wale ambao bado wanaona ni hatari kurudi nyumbani watafutiwe sehemu mbadala za kuishi kwa muda.

Shule zitakapofunguliwa wiki ijayo, haitakuwa vyema wanafunzi kupata kuna watu wanaoshi katika sehemu wanazotegemea kimasomo.

Hayo si mandhari mazuri ya kuendeleza elimu kwa watoto wetu.

Kando na hayo, usalama wa watoto unastahili kulindwa wakati wote na hivyo basi kila anayekuwa shuleni wakati wa muhula anafaa kuwa mtu anayefahamika vyema kwa wasimamizi wa shule husika.

Kila mwaka huwa tunasikia jinsi mamilioni ya pesa au hata mabilioni yanavyotengewa masuala ya kushughulikia majanga.

Hili sio tu katika serikali kuu bali pia katika serikali za kaunti.

Licha ya haya, huwa tunazidi kuona wananchi wakiteseka kila mara janga linapotokea, na tunabaki kushangaa pesa zinazotengwa huwa zinafanyiwa nini.

Tungependa kuona serikali kuu na za kaunti zikichukua hatua za haraka wiki hii.

Hazina za kutoa misaada wakati wa majanga zifunguliwe, na wote waliohamia shuleni wasaidiwe kuhama kabla shule zifunguliwe kwa muhula wa kwanza 2020.