TAHARIRI: Wanaotoa chanjo watoe habari zote

TAHARIRI: Wanaotoa chanjo watoe habari zote

NA MHARIRI

WATU 789 wapya waliripotiwa kuambukizwa virusi vya corona na kufikisha jumla ya maambukizi kuwa 220,727. Maambukizi ya jana ni asilimia 14.

Idadi hiyo ya watu laki mbili inatokana na watu 2,253,457 pekee waliopimwa, kwenye nchi iliyo na karibu watu milioni 50.

Serikali inasema upimaji umekuwa wa chini kutokana na kukosekana kwa vifaa muhimu katika kaunti mbalimbali.

Aidha, inawapima tu waliolengwa au wanaojiwasilisha hospitalini.Kwa sababu hii, kuna hatari ya kuwa mamilioni ya watu wana virusi vya corona, wakati ambapo sekta mbalimbali za uchumi zinafunguliwa.

Wiki jana sekta ya uchukuzi wa umma iliruhusiwa kubeba abiria kwenye viti vyote vya matatu na mabasi. Ina maana kwamba kinga pekee ni watu kupata chanjo kwa wingi na kuendelea kuvaa barakoa.

Wizara ya Afya imethibitisha kwamba walimu na maafisa wa usalama ni kati ya watumishi wa umma wachache zaidi kupata chanjo. Kiwango cha upeanaji chanjo kiko chini, na hili linaeleweka.

Kumekuwa na kila aina ya propaganda na habari za kutisha kwenye mitandao ya jamii kuihusu chanjo yenyewe.

Serikali haijatumia maafisa wake wa mawasiliano kutengeza jumbe maalumu zinazoweza kuwaondoa hofu wananchi.Lakini baadhi ya maafisa wanaochanja watu ni kama hawajaelewa kanuni za kumpa mteja maelezo yote kikamilifu.

Awali serikali ilipoingiza nchini chanjo ya AstraZeneca kwa mara ya kwanza mnamo Aprili, wauguzi na maafisa waliochanja watu waliwapa maelezokikamilifu.

Kwa mfano waliwataka wafahamu kuwa kama mtu ana dalili fulani, huenda akawa ana corona tayari na kudungwa wakati huo huenda iwe si salama.

Watu walielekezwa kujaza maelezo yao yote kikamilifu kabla ya kutafutwa ushauri kama walikuwa tayari kuendelea na chanjo au la.

Lakini sasa baadhi ya wanaochanja watu hawatoi maelezo yoyote. Mtu akiingia kwenye chumba cha chanjo anaulizwa jina, nambari ya simu na mtu wa karibu naye. Kisha papo hapo hutakiwa aonyeshe mkono wa kushoto na kuchanjwa.

Huu huenda ukawa ukiukaji wa haki ya mteja kupata maelezo. Iwapo mtu atadhurika kiafya kwa kutoshauriwa ipasavyo, kuna uwezekano jamaa zake wa karibu wakatishika na kususia chanjo hii muhimu.

You can share this post!

WANTO WARUI: Serikali iwape vijana mazingira bora kuundia...

Lungu adai kura ya urais ilijaa dosari mpinzani akiongoza