Makala

TAHARIRI: Wanaotuongoza wawe wamesoma

October 30th, 2018 2 min read

NA MHARIRI

KISA cha Jumatatu ambapo Mwakilishi wa Wadi moja katika Kaunti ya Kisii aliwatumia watahiniwa wa mtihani wa darasa la Nane (KCPE) kadi ya kuwafariji akidhani ilikuwa ya heri njema, kinaibua maswali kuhusu viongozi tunaowachagua.

Diwani huyo, japo hatujui kiwango chake cha elimu, anaonyesha ni kwa kiwango gani watu tuliowachagua watulindie maslahi yetu katika ngazi za kaunti hawana unakini katika wanayofanya.

Hata kama ni msomi, kutoangalia kwa makini na kujua kama kadi hiyo ilikuwa ya heri njema au la, ni ishara tosha kuwa hakuwa makini. Kitendo hicho bila shaka kilikuwa cha fedheha na huenda kiliwavunja moyo watahiniwa hao.

Kitendo hicho yafaa kichunguzwe na maafisa wa usalama pamoja na wa wizara ya Elimu, ili ifahamike kama kweli ni ukosefu wa elimu au kilifanywa kimakusudi.

Vyovyote itakavyokuwa, ni muhimu kwa Wakenya kuangaza macho na kujiuliza maswali kuhusu viongozi wanaowataka. Tangu zamani madiwani wamekuwa watu wa kuchaguliwa mashinani, bila kujali misingi yoyote maalum.

Mradi mtu ni Mkenya, mwenye akili timamu na aliyefikisha miaka 18, anachaguliwa kuwakilisha wakazi katika wadi.

Jambo hili limefanya kila mtu kukimbilia uongozi katika wadi, hasa baada ya Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC), kuweka kiwango cha mishahara ya wawakilishi hao kuwa cha juu, kushinda hata madaktari, walimu au wahadhiri.

Pia, ni dhihidirsho kwamba Kenya elimu haithaminiwi. Japokuwa watu huhangaika kulipa karo na kupata masomo mazuri, wanapobahatika kupata ajira hupewa mshahara duni.

Wale walio na ujuzi wa kujianzishia biashara, hukumbana na mazingira magumu kutokana na ushawishi wa wawakilishi wa wadi, ambao siasa zao duni mara nyingi huzalisha magenge ya wahuni wa kuwaandama kila waendapo.

Tunapowaza kufanyia marekebisho Katiba, iwapo hilo litatokea, yatupasa tufikirie upya vigezo vya watu wanaostahili kuchaguliwa kuongoza wananchi.

Haiwezekani kuwa uongozi utahusishwa na pesa au kusema sana mbele za watu. Ni sharti tusisitize viwango vya elimu, ili watu tutakaowapa jukumu la kutuwakilisha wawe wanaweza kusoma na kuandika.

Lengo la uwakilishi ni kuwa na watu wanaoweza kutambua yanayoendela katika uongozi wa kaunti zao. Asuyejua kusoma hawezi kuwa na usaidizi kwa wananchi.