TAHARIRI: Wanasiasa wamemaliza yao, uamuzi sasa ni wako

TAHARIRI: Wanasiasa wamemaliza yao, uamuzi sasa ni wako

NA MHARIRI

HATIMAYE, kampeni ambazo zilikuwa zimeteka taifa katika miezi sita iliyopita zimefikia tamati.

Baada ya kukurukakara zilizoanza na kura za mchujo mwezi Aprili, ni wakati wako mwananchi kuamua nani kati ya maelfu ya wagombea viti mbalimbali anatosha mboga kupewa wadhifa huo.

Muhimu zaidi ya yote ni kudumisha amani wakati na baada ya uchaguzi.Katika mikutano yao ya mwisho jana, vigogo wakuu wanaogombea urais, Naibu Rais William Ruto (Kenya Kwanza) na Raila Odinga (Azimio), walitoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanakuwa watulivu hata baada ya uchaguzi mkuu Jumanne.

Itakuwa vyema kwa wafuasi wao na wananchi kwa jumla kufuata wosia huu, na hata kufanya handisheki mmoja kwa mwingine kama alivyoahidi Bw Odinga uwanjani Kasarani, iwapo atashinda au la.

Dkt Ruto naye akizungumza katika uwanja wa Nyayo alihimiza wananchi kukubali matokeo ya kura kama ambavyo atafanya yeye, maana “Kenya iliyo na amani ni bora kwa wote bila kuzingatia utakuwa upande upi wa serikali au dini, rangi ama jamii unayotoka. Amani ndiyo nguzo ya ustawi wa taifa lolote.”

Kumbuka, ni kura yako ndiyo inamfuta kazi ama kumuajiri mwanasiasa; bila wewe hayupo.

Jitokeze kumpiga kura mgombea wako maana hata awe ni mwadilifu na mweledi kiasi gani, ukikosa kushiriki uchaguzi ni sawa na kumpa kura mgombea usiyemtaka.

Yote tisa, ukishapiga kura rudi nyumbani ama mtaani ukunywe chai na jirani yako maana ndiye “ndugu wako wa karibu”.

 

You can share this post!

MKU yakabidhiwa cheti cha ubora kutoka KEBS

JUNGU KUU: Hatari ya Mlima kutengwa na rais

T L