Makala

TAHARIRI: Wapi Matiang'i matatu zikituua?

August 6th, 2019 2 min read

NA MHARIRI

WAZIRI wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i anaonekana kuanza kulemewa na majukumu yake, tangu alipopewa mamlaka ya kusimamia shughuli za serikali katika Baraza la Mawaziri.

Waliomzoea Dkt Matiang’i alipokuwa waziri wa Elimu, wanashangazwa na kukosekana makali yake, tangu aipoongoza msako wa kutekeleza sheria mpya za trafiki.

Huenda uamuzi wa kuondoa Halmashauri ya Uchukuzi Barabarani (NTSA) kutoka kwa wizara ya Uchukuzi haukuwa sahihi. Madereva, makondakta na wamiliki wa magari ya usafiri wa umma wana jeuri na kiburi kiasi ya kwamba, hakuna mtu anayeweza kuwatisha.

Kwa mfano usiku wa Ijumaa katika eneo la Gilgil, madereva wa malori waliunda mistari miwili na kujaza barabara, mistari yote ikielekea Nakuru.

Abiria, waliokuwa na watoto au wagonjwa, walibaki kwenye msongamano huo hadi saa mbili za asubuhi ya Jumamosi, ilhali kuna maafisa wanaosimamia trafiki kaunti ya Nakuru.

Kubwa zaidi sasa hivi ni mtindo wa wenye matatu kurusha watu kutoka kwenye magari yakiwa yanaenda. Kisa cha punde zaidi ni cha kijana Gerald Kamotho Wachira aliyerushwa kutoka nje ya basi asubuhi ya Ijumaa.

Alikorofishana na kondakta eneo la Roysambu, akarushwa nje na kufariki papo hapo. Polisi wa Kasarani walikamata basi, lakini dereva akaachiliwa baada ya kulipa bondi ya polisi ya Sh60,000.

Polisi wa kituo cha polisi cha Kasarani wanasema kwa sababu sheria inaruhusu dhamana ya polisi, hata watu wanaohusishwa na mauaji wana haki ya kupata dhamana hiyo. Je, Dkt Matiang’i huo ndio msimamo wa wizara yako?

Kinachoudhi ni kwamba, basi lililohusika Ijumaa ni lile lile yenye nambari za usajili KCC 021 A ambalo mwaka jana lilihusika na kisa kingine cha kumrusha nje Doreen Kinyamwiti, aliyekuwa mwanafunzi wa Nairobi Institute of Business Studies (NIBS).

Maswali ambayo Wakenya wanajiuliza ni haya: Je, ni nani mmiliki wa basi hilo? Ni kwa nini hata watu wa NTSA wameshindwa kukamata basi badala ya waendeshaji? Mbona hata Dkt Matiang’i hajasema chochote kuhusu visa vya watu kurushwa nje ya magari? Kwani usalama wa abiria si usalama wa nchi?

Kinachoudhi zaidi ni kuwa, kisa hiki kimejiri mwezi mmoja tu baada ya kingine ambapo Florence Wanjiru alirushwa nje ya gari la kampuni ya Kileleton. Sasa ni lazima serikali ichukue hatua. Wakenya hawatakubali unyama huu dhidi ya raia wasio na hatia.