Makala

TAHARIRI: Watumiao barabara wawe waangalifu

November 30th, 2020 2 min read

KITENGO CHA UHARIRI

IDARA ya Utabiri wa Hali ya Hewa imetahadharisha kwamba mwezi wa Desemba unaoanza kesho utakuwa wa mzizimo.

Kwamba katika maeneo mengi ya nchi, kutakuwa na mvua inayotarajiwa kuendelea kwa muda. Mvua hii, katika baadhi ya maeneo huenda itaandamana na mafuriko. Hali hii husababisha maji kujaa kwenye mashimo barabarani.

Aidha, maji ya mafuriko yanaweza kukata barabara au kusomba madaraja. Hali ya ukungu hujitokeza kunaponyesha na kuwatatiza madereva kuona vizuri wanakoenda.

Kwa hivyo, ijapokuwa Desemba huwa msimu wa shamrashamra, iwapo itaandamana na mvua jinsi ambavyo mambo yameanza kuonekana, itabidi kila mmoja wetu achukue tahadhari.

Takwimu ya Mamlaka ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA) zinaonyesha kuwa zaidi ya watu 3,000 walifariki kwenye ajali, ambalo ni ongezeko la karibu asilimia sita. Mbali na magari, waliofariki barabarani walijumuisha waendeshaji bodaboda na watu waliovuka barabara kwa miguu.

Kunaponyesha hivi, huwa kuna utelezi au mitaro hujaa maji. Katika miji mingi kuna maeneo maalumu kwa abiria kuvuki. Nairobi, Mombasa na baadhi ya miji kuna madaraja yaliyojengwa ili watu wanaotembea kwa miguu wayatumie. Madaraja haya huokoa maisha, hasa wakati wa mvua.

Wananchi wanaotembea kwa miguu wanapaswa kuchunga maisha yao kama watu binafsi, kwa kutumia madaraja hayo. Ni afadhali mtu achelewe lakini avuke barabara akiwa mzima, badala ya kuchukua njia za mkato na kuishia kujeruhiwa au hata kufa.

Kwa madereva, Desemba huwa na Krismasi ambapo miaka ya nyuma, watu wengi walikuwa wakikimbilia magari ya usafiri wa umma ili kwenda kwao mashambani. Katika kutaka kubeba abiria wengi, wahudumu wa matatu wamekuwa wakiwajaza watu na kuendesha kwa kasi.

Jambo hili huhatarisha maisha ya watu. Wakati huu ambapo Disemba itakuwa yenye mvua, madereva wanapaswa kuwa waangalifu na kuendesha magari wakijua kwamba wanabeba binadamu.

Kuwepo kwa maambukizi na vifo kutokana na janga la Corona, ni makosa kuwajaza watu kwenye magari hayo. Polisi wanapaswa kuanza mapema kufanya misako ya magari yatakayokiuka kanuni za Wizara ya Afya.

Usalama wa abiria ni muhimu zaidi kushinda faida kidogo ambayo wahudumu hao wanajitafutia.