TAHARIRI: Wazazi wakomeshwe kupeleka watoto kwa mikutano ya kisiasa

TAHARIRI: Wazazi wakomeshwe kupeleka watoto kwa mikutano ya kisiasa

NA MHARIRI

WAKATI kampeni za siasa za chaguzi kuu zinapoanza humu nchini, huwa mambo mengi yanatiliwa maanani kwa minajili ya kudumisha usalama wa umma.

Ni wakati huo ambapo utapata idara ya uchukuzi wa ndege ikianza kueneza masuala muhimu kuhusu matumizi ya helikopta, huku idara nyingine zikitilia maanani mambo ya kiusalama na kuzuia uchochezi wa umma unaoweza kusababisha ghasia.

Kutokana na vitimbi vingi vinavyoshuhudiwa nyakati hizi, kuna jambo moja muhimu mno ambalo wadau wanaohusika na mambo ya kampeni za kisiasa husahau kuchukulia kwa uzito.

Katika kampeni za wanasiasa tofauti nchini, mara nyingi hutakosa kuona mtu akiwa amewasili hapo na mtoto mdogo, wengine wakiwa ni wachanga mno.

Baadhi ya watu wazima hung’ang’ana ndani ya umati na kusukumana wakitaka kumfikia kigogo wa kisiasa aliyehudhuria mkutano husika ili amsalimie mtoto wake, pengine kwa imani kwamba hatua hiyo itamfanya mtoto kupewa msaada wa aina yoyote ile itakayomwinua maishani.

Kumbeba mtoto hadi katika mkutano wa hadhara wa kisiasa usio na mpangilio bora wa umati, ni jambo ambalo huhatarisha sana maisha ya watoto.

Inavyojulikana, jambo lolote hatari huwa linaweza kutokea katika mikutano aina hiyo iwe ni uwanjani au barabarani.

Si nadra wiki kukamilika bila kupokea habari kuhusu ghasia katika mkutano fulani wa kisiasa, risasi au gesi ya kutoa machozi kufyatuliwa, mkanyagano wa umati miongoni mwa mambo mengine yasiyo salama.

Kimsingi, mazingara yote ya mikutano hii kuanzia wa vipaza sauti, vumbi, upepo na mengineyo huwa si salama kwa afya ya watoto.

Kwa bahati nzuri, kwa sasa hakujaripotiwa madhara mazito kwa watoto wanaopelekwa katika mikutano hii lakini tukumbuke ni busara kuziba ufa kabla ukuta uporomoke.

Tunatoa wito kwa asasi zote zinazosimamia masuala ya haki za watoto kuzinduka, na kuhakikisha haki hizo zote zinalindwa kikamilifu wakati huu wa kampeni za kisiasa.

Yeyote anayeamua kuwapeleka watoto katika mikutano aina hii ya hadhara ya kisiasa bila kuzingatia usalama wao, anastahili kuchukuliwa kama mvunjaji wa sheria zinazolinda haki za watoto Kikatiba.

Mbali na haya, wanasiasa wanaofanya kampeni pia wahakikishe wanazingatia haki za watoto katika mipango yao ya usoni.

Manifesto zinazotolewa zisichukulie tu kwamba elimu pekee ndiyo haki ya watoto inayofaa kuzingatiwa, bali pia wanasiasa waangazie masuala mengine yanayodhuru maisha ya watoto ambayo yanahitaji kusuluhishwa kwa dharura.

You can share this post!

DCI wahoji Sonko kuhusu ghasia wikendi Mombasa

Karua atambuliwa kwa misimamo thabiti kuhusu utawala wa...

T L