Makala

TAHARIRI: Waziri wa Elimu awe na msimamo rasmi

January 7th, 2019 2 min read

NA MHARIRI

WANAFUNZI wanapojiunga na shule za upili Jumatatu, maswali yanazidu kuibuka kuhusu jinsi ya kuwasajili.

Katika kipindi cha siku tatu zilizopita, kumekuwa na kauli moja baada ya nyingine, huku Wizara ya Elimu ikionekana kutokuwa na msimamo halisi wa serikali katika usajili huo.

Awali, kulikuwa na tahadhari kwa walimu wakuu wa shule za upili kuwa wasithubutu kuwasajili wanafunzi, isipokuwa katika shule walizopewa kupitia mitambo ya kompyuta. Baadaye waziri Amina Mohamed alibadili kauli na kusema wanaweza kuwasajili wanafunzi.

Kugeuka huko kwa msimamo wake huenda kulisababishwa na kelele za baadhi ya wazazi, waliodai kuwa watoto wao walikuwa wameitwa kujiunga na shule za upili ambazo hawakuchagua, au hawakupewa nafasi ya kupata shule ‘nzuri kulingana na alama walizopata’.

Ingawa serikali inasisitiza kwamba lazima kila mwanafunzi asajiliwe kwenye mfumo wa kuweka kumbukumbu za wanafunzi, maarufu kama NEMIS, njia inayotumia kuwasiliana na umma haifai.

Wizara ya Elimu ina washauri wengi ambao wananchi wanatarajia kuwa wanaweza kutoa mwelekeo kwa waziri na katibu wake, kuhusu namna ya kujieleza.

Ingawa Kenya ina bahati ya kuwa na utumizi wa hali ya juu wa mtandao, si kweli kwamba kila mzazi anajua jinsi ya kutumia kompyuta.

Kusisitiza kwamba lazima kila mzazi apate nakala ya usajili wa mwanawe kutoka kwa wavuti wa wizara ya Elimu, kwanza ni kuwatia wananchi gharama ya ziada.

Kwenda kwenye mkahawa unaotoa huduma za inatenti kunahitaji fedha na wakati. Kwa nini wizara haikusema mambo haya mapema na kuacha kubadili misimamo?

Pili, kutumia kompyuta kunahitaji mtu kuwa na elimu ya kiwango fulani. Hivi waziri Amina na Katibu Dkt Belio Kipsang wanafahamu kuwa idadi kuwa ya wazazi wa wanafunzi wanaotaka kujiunga na kidato cha kwanza huenda walisoma, lakini hawana uwezo wa hata kuikaribia kompyuta?

Si vizuri kufananisha usimamizi wa idara serikalini, lakini ilivyo sasa, ni kama wizara ya Elimu chini ya Bi Amina inakumbwa na tatizo la kukosekana msimamo halisi wa serikali.

Hali ya sasa inatukumbusha wizara hiyo ilipokuwa ikisimamiwa na Dkt Jacob Kaimenyi, ambapo alikuwa akitangaza sera nyingi ambazo hazikuwa zikilingana na kanuni wala sheria za usimamizi wa elimu.