Makala

TAHARIRI: Wizara ya Afya ichunguze tatizo la Hospitali Kuu ya Kenyatta

March 4th, 2018 2 min read

Waziri wa Afya Bi Sicily Kariuki alipohutubia wanahabari katika Hospitali Kuu ya Kenyatta baada ya madaktari kumpasua kichwa mgonjwa kimakosa. Picha/ Maktaba

TUKIO la hivi punde ambapo madaktari katika Hospitali Kuu ya Kenyatta walimfanyia upasuaji mgonjwa ambaye hakustahili upasuaji huo, ni jambo ambalo limewashangaza wengi na kuibua hisia mseto.

Katika siku za hivi punde matukio kadhaa yamejitokeza katika hospitali hii kuu, ambayo ni pamoja na wizi wa mtoto mchanga pamoja na madai ya wanawake wanaojifungua kubakwa.

Madai haya ni yale ambayo huenda yamefaulu kujitokeza hadharani ila pana uwezekano mkubwa kuwa hospitali hii imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingine tele.

Matukio haya yanahitaji uchunguzi wa kina kuhusiana na utendakazi wa kila mtu aliyeajiriwa hapo na vigezo vyake vya kuhakikisha usalama, sio tu wa wagonjwa bali hata wao wenyewe, vinadumishwa.

Hospitali hii inahudumia idadi kubwa ya wagonjwa na itakuwa vyema kwanza kubainisha ni mambo yepi ambayo huenda yakaelekeza mgonjwa kukosa kutambulishwa vilivyo na kuishia kufanyiwa upasuaji ambao hakustahili.

Hii ni kwa sababu endapo kuna tatizo lazima lichunguzwe na sio kuanzia wakuu pekee kwa sababu kila mmoja amepewa majukumu yake anayostahili kuyatekeleza vilivyo.

Madai ya ubakaji yalipoibuka, hospitali iliongeza walinzi mbali na kuahidi kutekeleza hatua nyinginezo.

Ni muhimu kwa wizara ya Afya kuangalia kwa kina jinsi hospitali hiyo inavyoendesha kazi zake, hasa kwa kuwa imekuwa ikilalamika kuhusu idadi kubwa ya wagonjwa, baadhi ambao wanaweza kutibiwa katika hospitali za kaunti na kutumwa huko tu iwapo kuna hitaji la matibabu maalum.

Hospitali ya Kenyatta inahudumia wagonjwa kutoka Afrika Mashariki na Kati na ni muhimu utendakazi wake uwe wa hali ya juu.

Lakini kwa hilo kufanyika lazima mazingira hayo ya kufanya kazi yaimarishwe pamoja na kutiliwa maanani ili kuhakikisha kuwa watu wanawajibika na kuwa na motisha ya kutoa huduma bora.

Tukio hilo la upasuaji bila shaka limeibua maswali mengi, na wizara badala ya kuwaomba radhi Wakenya inastahili kuwaeleza jinsi inavyolenga kuhakikisha kuwa baadhi ya matukio haya hayataibuka tena.

Serikali lazima iweke mikakati kabambe ya kuimarisha hospitali hii kwa kuhakikisha kuwa inajali maslahi ya wahudumu, wafanyakazi pamoja na kuajiri kulingana na ufaafu wa watu kwa nafasi hizo.

Inastahili pia kufuatilia kwa karibu shughuli zake kwa lengo la kuiboresha na kuitengea pesa za kutosha ili baadhi ya matukio yaweze kuepukwa.