TAHARIRI: Yafaa tuwaruhusu mashabiki viwanjani

TAHARIRI: Yafaa tuwaruhusu mashabiki viwanjani

KITENGO CHA UHARIRI

WIZARA ya Michezo inafaa iwaruhusu mashabiki wa soka warejee uwanjani wakati huu ambapo maambukizi ya corona yanapungua.

Mechi za Ligi Kuu nchini (KPL) zimekuwa zikiendelea tangu mwezi Novemba, japo mashabiki hawajaruhusiwa kufika uwanjani kushangilia timu zao.

Tangu ligi kuanza klabu zimewapima wachezaji corona huku pia dawa ikinyunyizwa uwanjani kama njia ya kudhibiti virusi hivyo.

Ni jambo zuri kuwa hakujawahi kuripotiwa maambukizi ya corona miongoni mwa wachezaji na japo matokeo ya vipimo hivyo huwa hayawekwi hadharani, ukweli ni kuwa kurejelewa kwa mchezo wa soka haujachangia ongezeko la maambukizi mengine nchini.

Mwanzo, viwanja ambavyo huandaa mechi za ligi huwa vina uwezo wa kuwasitiri mashabiki kiasi fulani.

Kwa mfano uga wa Kasarani ina uwezo wa kuwasitiri mashabiki 60,000 na ule wa Nyayo, 45,000. Iwapo wizara itawaruhusu mashabiki 5,000 ambao wataketi umbali wa mita moja unusu na kuzingatia masharti yote, litakuwa jambo jema kwao. Vile viwanja vidogo vidogo navyo vinafaa viruhusiwe viwe na angalau mashabiki 1,500 pekee.

Klabu za kijamii kama Gor Mahia na AFC Leopards ambazo zinajivunia ufuasi mkubwa pia hutegemea ada zinazotozwa langoni kuwalipa wachezaji na kugharamia masuala mengine. Iwapo mashabiki kiasi wataruhusiwa, Gor na AFC ambazo kwa sasa zinakabiliwa na uchechefu wa fedha, angalau zitapata hela kidogo baada ya kipindi kirefu.

Inasikitisha kuwa klabu hizi ziliambulia patupu katika Debi ya Mashemeji wikendi iliyopita kutokana na marufuku inayoendelea dhidi ya mashabiki viwanjani.

Ni kinaya kuona mashabiki wakinyimwa burudani ilhali wanasiasa huandaa mikutano ya halaiki ambapo masharti yaliyowekwa kuhusu corona hayazingatiwi kabisa.

Hapo kesho, Gor Mahia itakuwa inacheza mechi ya Kombe la Mashirikisho Afrika dhidi ya Napsa ya Zambia. Mashabiki huwashaajisha wachezaji ili wajitume na ingekuwa vyema iwapo wangekuwa uwanjani ili kuipa K’Ogalo sapoti inayohitajika ili kuwabwaga vijana hao wa Zambia.

Serikali iangazie suala hili kwani mataifa mengi yameanza kuwaruhusu mashabiki uwanjani.

Hata Cameroon ambayo ilikuwa mwenyeji wa dimba la Chan pia iliwaruhusu mashabiki uwanjani hadi mechi ya fainali kati ya Morocco na Mali.

You can share this post!

MUTUA: Valentino: Tutahadhari tunapoiga mila za kigeni

Uhuru aomba talaka