Makala

TAHARIRI:Tutafakari kuhusu mageuzi ya Katiba

October 8th, 2018 2 min read

NA MHARIRI

HATUA ya Naibu Rais William Ruto kubadili msimamo wake kuhusu kura ya maamuzi, huenda sasa inaashiria umuhimu wa kila mmoja kutafakari vyema kile kinachohitajika katika marekebisho hayo.

Kwa muda mrefu sasa, ubishani kati ya wanaounga mkono marekebisho ya katiba na wale wanaopinga umefanya kuwe na hali ambapo suala hilo limechukuliwa kisiasa.

Ilifikia kiwango ambapo marekebisho ya katiba yalikuwa yanachukuliwa kama jambo linalohusu ubabe wa kisiasa kati ya Bw Ruto na Kiongozi wa Upinzani, Bw Raila Odinga.

Hali hii ilikuwa imeanza kuibua taharuki nchini kwani kama ilivyo kawaida, misimamo mikali kuhusu masuala aina hii husababisha mgawanyiko wa wananchi kwa mirengo tofauti ya kisiasa katika hali inayoweza kuathiri utulivu wa nchi.

Wakati huu kutokana na kuwa pande zote zimekubali kwamba katiba inahitaji marekebisho, hakuna haja tena ya ushindani bali ushirikiano utakaoleta manufaa kwa kila mwananchi wa taifa hili.

Viongozi wote wanahitaji kupatanishwa, kuwe na mashauriano katika mandhari tulivu, na wote waelewane kuhusu marekebisho yanayofaa. Lakini ikumbukwe hili si suala linalohusu viongozi pekee, kwani katiba ni mwongozo muhimu zaidi wa jinsi taifa linavyosimamiwa na linavyoendesha shughuli zake zote.

Kwa msingi huu, mashauriano yajumuishe wadau wote, wakiwemo viongozi wa kijamii na wananchi ndipo tupate katiba itakayokubaliwa na kila mmoja wetu. Kwa wananchi, ni vyema wote wawe macho wasipotoshwe na viongozi ambao huenda wakataka kutumia marekebisho ya katiba kujitakia makuu kibinafsi.

Marekebisho yoyote yatoe kipaumbele kwa mahitaji ya mwananchi, kwa mfano, kwa kuondoa nafasi za uongozi ambazo hazihitajiki au zile zisizotoa mchango wowote wa maana katika uongozi bora wa taifa.

La muhimu zaidi ni kwamba inapaswa tutilie maanani hali ya kiuchumi inayotukumba kwa sasa.

Mchakato mzima wa kurekebisha katiba usiwe kwa hali ambayo itasababishia mwananchi gharama zaidi kwani sasa tayari wengi wao wanalalamikia hali ngumu ya kimaisha.

Kila pendekezo liwekwe wazi, lizingatiwe na kupigwa msasa ndipo tusonge mbele kwa pamoja kama taifa moja bila migawanyiko isiyo na maana.