Habari Mseto

Taharuki KDF kuua watu 3 kwa risasi kabla ya kujiangamiza

April 30th, 2019 1 min read

TITUS OMINDE na WYCLIFFE KIPSANG

MWANAJESHI aliyekuwa akifanya kazi katika kambi ya KDF ya Lanet, Nakuru Jumanne aliwaua watu watatu na kisha akajiangamiza kwa kutumia bunduki katika mtaa wa Jua Kali, Eldoret.

Kwenye kisa hicho cha saa kumi na moja alfajiri kilichozua taharuki, Haron Tiony alipagawa na kumpiga risasi mpenzi wake wa kike, Dorcas Lorinyo, ambaye pia ni mwanajeshi katika katika chuo cha mafunzo ya kijeshi RTS mjini Eldoret.

Kisha aliwaua shangazi yake Bi Rose Sang wa umri wa miaka 60 na mjombake Bernard Muge.

Kabla ya tukio hilo mwanajeshi huyo alishinda akinywa pombe na marafiki wake katika baa mbalimbali mtaani humo.

Inadaiwa kuwa marehemu alimpiga shangazi yake risasi pale alipokuwa akijaribu kumzuia kumuua rafiki yake wa kike nyumbani mwake.

Afisa mkuu wa polisi Eldoret Magharibi Bw Zacharia Bittok ambaye alizuru eneo la mkasa alisema chanzo cha mauaji hayo bado hakijabainika.

“Uchunguzi wa awali umebaini kuwa marehemu alimpiga shangazi yake risasi pale alipojaribu kumzuia kumpiga rafiki yake wa kike ambaye alikimbilia usalama nyumbani mwa shangazi wa mwanajeshi huyo pale kulitokea mvutano kati yake na mwanamke huyo,” alisema Bw Bittok

Bw Bittok alisema polisi walipata bunduki aina ya M4 ambayo ilitumika katika uhalifu huo.

Baadhi ya majirani na marafiki ambao walizungumza na wanahabari walisema kulitokea msukumano kati ya mwanajeshi huyo na rafiki yake wa kike.

Mamake mlezi ambaye alipoteza mzee wake wakati wa uvamizi huo alisema tangu utoto wake marehemu alikuwa mtu mwenye hasira.

Flora Muge ambaye mume wake ni miongoni mwa watu ambao waliua kwa risasi.