HabariSiasa

Taharuki ndani ya serikali

June 28th, 2019 2 min read

BENSON MATHEKA Na MWANGI MUIRURI

WAKENYA wameingiwa na wasiwasi kuhusu hali ya nchi kufuatia tofauti ambazo zimeigawanya serikali.

Migawanyiko hii imeonekana kuanzia kwenye urais wenyewe ambapo Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto wamekuwa wakivutia pande tofauti tangu mwaka 2018.

Katika hotuba zake Rais Kenyatta amekuwa akionyesha hasira kali dhidi ya Dkt Ruto kundi la Tangatanga la upande wa Dkt Ruto, ambalo limekaidi maagizo yake ya kuwataka wakomeshe kampeni za mapema za 2022.

Japo tofauti kati ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto zimekuwa wazi tangu mwaka jana, wadadisi wanasema kuhusishwa kwa Baraza la Mawaziri, makatibu wa wizara na wakuu wa idara kwenye tofauti hizi ni hatari kwa nchi.

Wachanganuzi wanasema madai ya Dkt Ruto kuwa baadhi ya mawaziri wanakula njama ya kumuua ni kilele cha uadui kati ya mirengo tofauti ndani ya serikali.

Kulingana na wakili Ahmednasir Abdullahi, Rais Kenyatta anafaa kuvunja baraza lake la mawaziri na kuteua jipya.

“Kufuatia madai ya Ruto kwamba wanawachama wanne wa baraza la mawaziri walipanga kumuua, Rais ni lazima avunje baraza lake la mawaziri na kuteua wapya,” alisema Bw Abdullahi.

Baadhi ya wadadisi wanasema katika hali ya sasa itakuwa vigumu kwa maafisa wa serikali ambao wanalaumiana kila uchao kutekeleza majukumu kwa manufaa ya taifa.

Dkt Ruto aliwalaumu mawaziri Peter Munya (Biashara), Sicily Kariuki (Afya), Joe Mucheru (Tekinolojia) na James Macharia (Uchukuzi) kuwa wanashirikiana na Katibu na Wizara ya Usalama wa Ndani, Dkt Karanja Kibicho kuandaa mikutano wa kupanga kummaliza.

Naibu Rais amekuwa akimlaumu Bw Kibicho kwa kuhujumu kazi yake kwa kuagiza makamishna wa kaunti na makamanda wa polisi kutohudhuria hafla anazoandaa mashinani.

Ingawa mawaziri waliodaiwa kupanga njama za kumuua Dkt Ruto walisema walikutana kujadili maendeleo katika eneo la Mlima Kenya, Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri ambaye anatoka eneo hilo, alijitenga nao jambo ambalo wadadisi wanasema linaonyesha tofauti kubwa katika serikali.

Mchanganuzi wa siasa Martin Andati anasema madai ya kupanga kumuua Dkt Ruto yataathiri pakubwa ajenda za serikali ya Jubilee.

“Madai hayo yataathiri shughuli za serikali pakubwa. Ruto ni kiongozi wa pili mwenye mamlaka makuu katika serikali. Atawezaje kuketi katika baraza moja na watu anaowashuku kupanga kumuua,” alisema Bw Andati.

Anasema pia itakuwa vigumu kwa Dkt Ruto kushirikiana na mawaziri hao katika shughuli za wizara wanazosimamia akitumwa na rais kumwakilisha.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa MutahiNgunyi matukio yanayoshuhudiwa yanaweza kutumbukiza nchi pabaya.

“Nchi inaelekea njia mbaya. Tuombe mambo hayataharibika zaidi,” Bw Ngunyi alisema.

Wachanganuzi wanamlaumu Rais Kenyatta kwa migawanyiko hiyo wakisema ameshindwa kuweka nidhamu miongoni mwa wadogo wake.

“Rais ndiye ametupatia mfano wa kuiga kwa kulalamika hadharani, kutoa vitisho, kuahidi bila kutimiza na hata kuzomea viongozi hadharani pasipo nia ya kuandaa vikao na kuwapa mwongozo ufaao,” asema mhadhiri wa somo la Sayansi ya Siasa, Gasper Odhiambo.

Aongeza: “Wakati serikali haina mwongozo thabiti wa kushughulikia masuala nyeti, kila mtu akiwa na lake la kutangaza anakimbia mitaani na kupayuka. Rais akiwaongoza kufanya hivyo, nao lazima wafuate nyayo zake.”