Taharuki watu watatu wakiuawa Kenol

Taharuki watu watatu wakiuawa Kenol

Na MWANGI MUIRURI

Wakazi wa mji wa Kenol ulioko Kaunti ya Murang’a Jumatatu wameamkia kisanga cha watu watatu kuuliwa kinyama na kisha miili yao kutupwa ovyo mtaani.

Mwili mmoja ulikuwa una kamba shingoni na kufungwa kwa mti ulio karibu na makao makuu ya Naibu Kamishna wa Murang’a Kusini njama ikiwa ni kuzuke taswira ya mtu aliyejinyonga.

Lakini waliojitokeza kutazama mwili huo walihoji ni jinsi gani angeweza kujinyonga kutoka kwa urefu mdogo kuliko aliokuwa nao.

“Hawezi akajinyonga akiwa amekanyanga chini…huyu ni kufungwa tu amefungwa hapo na wanaojua kilichomuua,” akasema mwanamke mmoja.

Miili mingine miwili ikiwa katika mduara wa kilomita moja, yote yakiwa na majeraha ya kuuawa kinyama, ilionekana na kuzidisha hasira za wenyeji walioitaka serikali kiuchukulia suala hilo kwa uzito.

Mshirikishi wa masuala ya Kiusalama eneo la Kati Bw Wilfred Nyagwanga alitaja kisa hicho kuwa cha kugadhabisha akiwataka maafisa wa kiusalama eneo hilo wachunguze visa hivyo ili ukweli ubainike na waliohusika wawajibishwe mkondo wa sheria ya haki.

Mwili wa pili ukionekana kuwa wa mwendeshaji pikipiki ulikuwa umedungwadungwa vibaya usoni kwa kifaa butu na kando ya alikokuwa ameiagia dunia kulikuwa na kipande cha bao kilichokuwa na misumari iliyojichomoza hivyo basi kugeuzwa kuwa silaha.

Kipande cha bao kilichojaa damu na ambacho kinaaminika ni mojawapo ya silaha butu zilizotumika kutekeleza mauaji ya vijana watatu Mjini Kenol. Picha/ Mwangi Muiruri

Kipande hicho kilionekana kilitumika kutekeleza mauaji hayo kwa kuwa kilikuwa kiimejaa alama za damu.

Mwili wa tatu pia nao ukiwa na majeraha ya kushambuliwa kwa vifaa butu ulionekana katika eneo la Githanja—hali zote zikiwa na sadifa ya kuwa ni miili ya vijana wa rika moja.

Kwa mujibu wa Bw James Kiama ambaye ni mkazi katika boma moja lililo karibu na makao makuu ya Kaunti ndogo ya Murang’a Kusini, “haya ni mauaji ambayo yalitekelezwa mwendo wa saa tisa usiku.”

Aliambia Taifa Leo kuwa alisikia milio ya mbwa usiku “na nikaamka kujua kulikoni katika mtaa wetu. Niliangalia saa yangu na ilikuwa mwendo was aa tisa na nusu. Ndipo nilisikia mayoe nje na nikaelekea kwa dirisha kuchungulia. Sikuona kitu lakini kulikuwa na nduru zilizosikika zilikuwa za watu watatu…Halafu ghafla kukanyamaza na kukazuka mgurumo wa gari pamoja na wa pikipiki. Zikaondoka na kukanyamaza. Asubuhi ndio tumesikia kwamba kuna miili mitatu imepatikana na ninahisi kwamba kuna uhusiano wa tukio hilo la usiku na pia miili hii kupatikana hapa kwetu.”

Bw Nyagwanga alisema kuwa hicho ni kisa ambacho kinafaa kuchunguzwa kwa kina, baadhi ya wenyeji wakibashiri kuwa “haya ni mauaji ambayo kuna uwezekano mkuu kwamba waliuawa katika sakata ya wizi wa mananasi katika shamba moja eneo hili.”

Kunao waliashiria kuwa kumekuwa na ukatili tele eneo hilo ambao hutokana na vijana wengi kujihusisha na wizi wa mananasi hayo na kisha kuyauza katika masoko kadha ya eneo hilo, Kenol ikiwa ni mojawapo ya soko la sakata hiyo.

Katika siku za hivu punde, ukatili huo wa walinzi na vijana wanaosaka riziki kupitia wizi huo kushambuliana na kuzua mauti umekuwa ukiombwa na wenyeji utafutiwe suluhu.

Hata hivyo, Bw Nyagwanga alisema kuwa suala hilo linachunguzwa kwa kina “na tutakuwa na jibu kuhusu ni nini hasa kilifanyika ndio ikaishia miili hiyo kupatikana hapa Kenol.”

You can share this post!

Wakazi waikejeli serikali kusitisha usambazaji wa maji

Serikali yaonya wanaopandisha nauli kiholela