Taharuki yatanda mpakani watu 3 wakiuawa

Taharuki yatanda mpakani watu 3 wakiuawa

Na Oscar Kakai

TAHARUKI imetanda katika mpaka wa Kaunti za Pokot Magharibi na Elgeyo Marakwet baada ya watu watatu kuuawa kwenye uvamizi uliotekelezwa na majangili eneo la Chesegon wikendi.

Watatu hao walipigwa risasi eneo hilo ambalo ni nusu kilomita kutoka Marakwet Mashariki, Kaunti ya Pokot Magharibi. Kamanda wa Polisi wa Pokot Magharibi Jackson Tumwet alisema watatu hao walikuwa kwenye pikipiki kutoka soko la Lomut wakielekea Sokouto ndipo wakapigwa risasi na majangili hao wanaoaminika wanatoka Marakwet Mashariki.

Tukio hilo lilitendeka saa kumi kasorobo mchana. Majangili hao walivuka hadi upande wa Pokot kisha kuwapiga risasi watatu hao.

“Walinda usalama kutoka Sigor na Lomut wamefika katika eneo la tukio na wakaokoa watu wengine waliojeruhiwa,” akasema Bw Tumwet.

Chifu wa Cheptulel James Kapeyon alifichua kuwa kando na kuwaua watatu hao pia waliiba simu zao za mikononi.

“Miili hiyo imesafirishwa hadi hifadhi ya maiti ya hospitali ya Kapenguria. Kuna taharuki na watu wameanza kuishi kwa hofu,” akasema.

Viongozi wa eneo hilo wakiongozwa na mbunge wa Sigor Peter Lochakapong wamekashifu tukio hilo, wakisema hali ya usalama ilikuwa imezorota sana.

Bw Lochakapong alishangaa kwa nini majangili kutoka Pokot Magharibi, Elgeyo Marakwet na Tiaty hawajakamatwa ilhali wenyeji wamekuwa wakifikisha majina yao kwa polisi.

Mbunge huyo hata hivyo, alitoa wito kwa wenyeji wasilipize kisasi huku akitoa wito kwa maafisa wa usalama wahakikishe mauaji hayo hayatokei.

You can share this post!

Kenya yazidi kuteleza Olimpiki za Walemavu

Korti yaruhusu kaunti izike miili iliyotelekezwa kwa zaidi...