TAHARIRI: Makanisa mengine nao waige mfano kanisa la ACK

NA MHARIRI

MSIMU wa siasa huwa muda wa wanasiasa kufanya lolote. Ndio wakati ambao utawaona masokoni, matangani, harusini, na hata makanisani.

Kutokana na kanuni za kuzuia maambukizi ya corona, serikali ilipiga marufuku mikusanyiko ya watu kwenye viwanja na kumbi mbalimbali.

Maeneo pekee ambako bado watu wanapatikana kwa wingi, ni katika makanisa.Si ajabu kwamba ghafla wanasiasa wanaomezea mate kumrithi Rais Uhuru Kenyatta mwaka ujao, wamekuwa waumini wakuu kila Jumapili.

Jana Kinara wa chama cha ODM, Raila Odinga na mwenzake wa Amani National Congress (ANC), Musalia Mudavadi walikuwa kanisani Butere, Kakamega.

Kanisa la Kianglikana (ACK) lilikuwa likimtawaza Askofu wa Dayosisi ya Butere, Rose Okeno.Ingawa hafla hiyo ilikuwa ya kihistoria kwa kuwa Bi Okeno ni mwanamke wa kwanza kuchukua wadhifa huo, kuhudhuria kwa wanasiasa hao kulikuwa na lengo tofauti.

Ndio maana Askofu Mkuu Jackson Ole Sapit alipotangaza kwamba hawangeruhusiwa kuhutubu, waliondoka mmoja baada ya mwengine.Kwa kawaida, wanasiasa huwa wanatumia mialiko katika hafla za makanisa na ibada zinazohudhuriwa na watu wengi, kuuza sera zao, hasa wakati huu wa kampeni za uchaguzi mkuu.

Vigogo hao wa kisiasa huwa wanaandamana na wabunge na madiwani, na hugeuza hafla za kidini kuwa mikutano ya kampeni za kisiasa.

Bila aibu wanasiasa wanapopokea vipaza sauti, husahau kuwa wako mahali patakatifu. Hugeuza fursa ya kuzungumza kuwa nashambulizi dhidi ya wapinzani wao.

Askofu Ole Sapit aliwaambia wazi wanasiasa kote nchini kwamba wasitarajie kupatiwa nafasi ya kuzungumza wakihudhuria ibada katika makanisa ya ACK.

Kwamba kila mmoja anakaribishwa kanisani, lakini altari ni ya viongozi wa kidini pekee.Msimamo huu wa Askofu Ole Sapit kwamba kanisa la Kianglikana (ACK) hakitawapa nafasi wanasiasa kuzungumza, ni mzuri. Unafaa kuungwa mkono na Wakenya wote.

Viongozi misikitini wamekuwa na msimamo huu tangu zamani. Hata uwe nani, unaswali kwenye mikeka kama watu wengine. Swala ikiisha, unaondoka na kuendelea na shughuli zako.Lakini wanasiasa wamekuwa wakiotea majukwaa ya makanisa kuongea.

Wangekuwa wanazungumza mambo ya kuwajenga raia kiuchumi na kimaendeleo, hakungekuwa na sababu ya kuwa na wasiwasi.

Wengi wakipewa nafasi ya kuzungumza, huonyesha wazi kuwa hawana sera. Badala ya kueleza ni vipi wanapanga kubadili maisha ya vijana, akina mama, wazee na watu wengine, huanza kushambulia wenzao na kuvuruga heshima ya madhabau. Tabia hii si katika makanisa pekee.

Wanasiasa wamekuwa wakiotea matanga. Badala ya kuwafariji waliofiwa, hugeuza matanga hayo kuwa majukwaa ya matusi na fitina. Kwa hivyo Wakenya wengine yafaa waige hatua zilizochukuliwa na ACK.

Ole Sapit aitaka serikali isambaze PPE kwa hospitali zinazosimamiwa na makanisa

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Kanisa la Anglikana Nchini (ACK) Askofu Mkuu Jackson Ole Sapit ametoa wito kwa serikali kusambaza vifaa vya kujikinga (PPE) katika hospitali zinazosimamiwa na makanisa wakati huu wa janga la Covid-19.

Alisema hatua kama hiyo itahakikisha wahudumu wa afya katika hospitali hizo pia wanakingwa dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona wanapowahudumia wagonjwa.

“Vifaa vya kujikinga vinavyotolewa kwa serikali na wahisani au kununuliwa kwa fedha zinazokusanywa visambazwe kote nchini katika hospitali za umma na zinazosimamiwa na makanisa,” Ole Sapit akasema wakati wa ibada ya Jumapili katika Kanisa la All Saints Cathedral, Nairobi.

Ibada hiyo ilipeperushwa kupitia runinga na mitandao kwani serikali imepiga marufuku ibada za kawaida kama sehemu ya mikakati ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Askofu Ole Sapit pia aliitaka serikali kusambaza pesa zinazotolewa na wahisani kama msaada wa kufadhili vita dhidi ya janga hilo kwa hospitali hizo ambazo zinakabiliwa na changamoto ya uhaba wa pesa wakati huu ambapo watu wengi hawaendi huko kwa matibabu.

“Unyanyapaa unaohusishwa na ugonjwa wa Covid-19 umechangia watu wengi kuogopa kwenda hospitalini. Hali hii imesababisha hospitali za makanisa kukosa fedha za kuwalipa wahudumu wao,” akasema.

Askofu Ole Sapit aliitaka serikali kuondoa ushuru unaotozwa vifaa vya PPE ili bei yavyo ishuke wakati huu ambapo vinahitajika kwa wingi.

Raila asifu Sapit kwa kupigana na ufisadi kanisani

Na RUSHDIE OUDIA

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga amemiminia sifa Kiongozi wa Kanisa la Anglikana (ACK) Jackson Ole Sapit kwa kupiga marufuku michango ya fedha kutoka kwa wanasiasa.

Bw Odinga alisema hatua ya Askofu Mkuu Sapit inasaidia katika kukabiliana na ufisadi ambao umekolea nchini.

Kumekuwa na mjadala kuhusiana na mamilioni ya fedha yanayotolewa na wanasiasa makanisani huku Bw Odinga na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Hajji wakiamini kuwa michango hiyo inaendeleza wizi wa fedha za walipa ushuru.

Bw Odinga alidai kuwa wanasiasa wa kundi la Tangatanga linalounga mkono Naibu wa Rais William Ruto linatumia fedha kujitafutia umaarufu nchini.

Bw Odinga alikuwa akizungumza katika Kaunti ya Siaya wakati wa hafla ya kusherekea kustaafu kwa Askofu wa Parokia ya Maseno Magharibi Dkt Joseph Otieno Wesonga.

Alisema uchumi wa Kenya umedorora kutokana na ufisadi.

“Wanasiasa sasa wanawahonga viongozi wa kidini ili wawaalike kanisani kufanya mchango. Fedha hizo zinatokana na ufisadi na wanazitumia kununua watu wa kuwaunga mkono,” Bw Odinga.

“Hata wafanyabiashara maarufu kama vile Vimal Shah na Manu Chandaria ambao wamekuwa wakisaidia jamii hawawezi kutoa mamilioni ya fedha kila wikendi,” akasema.

Suala kuhusu harambee kanisani limekuwa likiibua mjadala mkali, lakini Dkt Ruto husisitiza ataendelea kutoa michango hiyo kwa kuwa ni shukrani yake kwa Mungu.

Raila apongeza kanisa la ACK kwa kukataa pesa za ufisadi

Na Victor Raballa

KINARA wa ODM Raila Odinga amepongeza kanisa la ACK kwa msimamo wake dhidi ya kutumiwa vibaya na viongozi wafisadi.

Bw Odinga alisisitiza kuwa kanisa halifai kutumiwa kama pahali pa kutakasa pesa za ufisadi na wanasiasa wasiotaka kufichua wanakotoa pesa za michango yao kanisani.

“Nyingi ya pesa zinazotolewa makanisani ni za ufisadi kwani zilikuwa zimepangiwa kwa ujenzi wa vifaa muhimu kama hospitali, barabara, shule na kuzalisha chakula cha kutosha kwa Wakenya,” alisema.

Kigogo huyo aliyekuwa akizungumza Siaya,lihimiza viongozi wa kidini wanaotii wito wao wasihofu kutilia shaka chimbuko la mamilioni ya pesa zinazotolewa kama michango makanisani mwao.

Bw Odinga alieleza: “Askofu Mkuu wa kanisa la Kianglikana Jackson Ole Sapit ndiye kiongozi wa kwanza wa kidini kusimama wima kuwakashifu wanasiasa wanaozunguka nchi kwa lengo la kuwahadaa Wakenya kuelekea siasa za 2022.

“Inashangaza mtu anayepokea mshahara wa Sh1 milioni kwa mwezi kutoa michango ya hadi Sh30 milioni kila mwezi.”

 

Waumini wa ACK wakataa uteuzi wa viongozi wapya jimbo la Kitale

Na OSCAR KAKAI?

MZOZO katika kanisa la Anglikana katika kaunti ya Pokot Magharibi unaendelea kutokota huku baadhi ya waumini wakipinga viongozi wapya kwa madai ya uongozi mbaya.

Haya yanajiri siku tatu baada ya kanisa la ACK kumteua Dkt Emanuel Chemetich kuwa kasisi wa jimbo la Kitale mwaka jana.? Kwa zaidi ya miaka 25, kumekuwa na mizozo hiyo na kuchangia mgawanyiko kati ya wakristo katika kanisa hilo.

Mwaka jana, dayosisi ya Kitale iligawanyika kutokana na mizozo kati ya waumini wa kanisa hilo huku zaidi ya waumini elfu kumi kutoka kaunti ya Pokot Magharibi wakiamua kujiondoa kutoka kwenye dayosisi hiyo.

Baadhi ya wakristo hao kutoka kaunti ndogo zote nne katika kaunti ya Pokot Magharibi walijiondoa kutoka dayosisi ya Kitale na kuzindua rasmi dayosisi ya Kapenguria na kuanza shughuli zao wakiwasiliana na eneo la mkoa chini ya askofu mkuu wa kanisa hilo nchini, Jackson Ole Sapit.

Mizozo hiyo imeleta migawanyiko kati ya wakristo na hata kulemaza shughuli za dayosisi asili ya Kitale.

Wakiongea na wanahabari mjini Kapenguria, Wakristo hao walipinga askofu Chemetich kuwa aliteuliwa bila kufuata utaratabu na kumtaka askofu mkuu kuwapa dayosisi.?Kundi moja linataka kubuniwa kwa dayosisi mpya ya Kapenguria huku jingine likitaka kusalia ile ya Kitale.

Mzozo wa uongozi kati ya waumini umeendelea kushuhudiwa huku wakristo zaidi ya elfu kumi wakijiondoa kutoka kwa dayosisi ya Kitale na kuzindua rasmi doyosisi ya Kapenguria na kuanza shughuli zao wakiwasiliana na eneo la mkoa chini ya askofu mkuu wa kanisa hilo nchini, Jackson Ole Sapit.

Tutaendelea kupokea pesa za wanasiasa, Askofu aapa

Na NDUNGU GACHANE

ASKOFU wa Kanisa la Kianglikana (ACK) amewashutumu vikali viongozi wa kisiasa ambao wamekuwa wakiyakashifu makanisa kwa kupokea fedha zilizopatikana kwa njia ya ufisadi, akisema yataendelea na mtindo huo hadi pale mahakama itakapowapata na hatia viongozi wanaodaiwa hupora pesa kisha kuzitoa kanisani.

Askofu Timothy Gichere wa Dayosisi ya ACK Mlima Kenya ya Kati, alisema hakuna mwanasiasa anayefaa kudai mwenzake anatoa pesa za wizi kwa makanisa ilhali vyombo vya sheria havijampata anayerejelewa na hatia ya kushiriki ufisadi.

Bw Gichere vilevile alisema kanisa halina mbinu ya kutambua iwapo fedha zinazotolewa kwenye michango ya harambee zimeibwa na akawataka wanaokashifu makanisa kuviruhusu vyombo vya sheria kutekeleza wajibu wao badala ya kuingiza siasa kwenye suala hilo.

“Viongozi wanapofika kanisani na kuchangisha fedha, hatuwezi kukataa kwa sababu hatuna njia za kutambua iwapo fedha hizo ni za ufisadi au la. Kanisa haliwezi kuwaita watu wafisadi au waporaji kwa sababu hilo ni jukumu la mahakama.

“Naomba tuache sheria ichukue mkondo wake bila kuingiza siasa ili wafisadi wakamatwe na kufikishwa mahakamani,” akasema Bw Gichere. Askofu huyo aliyekuwa akizungumza katika Gereza la Murang’a alipoongoza Waumini wa ACK kuadhimisha Pasaka na wafungwa, alisema kanisa hilo linaunga mkono vita dhidi ya ufisadi ila akawataka viongozi kukoma kutatiza vita hivyo kwa kuingiza siasa.

Vilevile aliwaonya wanasiasa dhidi ya kutumia majukwaa kanisani kuhubiri chuki na ukabila akisema wanafaa kufika kanisani kupokea mafunzo ya kidini badala ya kushiriki siasa.

“Si vyema kwa wanasiasa kutumia muda wanaopewa kanisani kuhubiri chuki na kufanya kampeni. Wanafaa kuhudhuria ibada ili kulishwa chakula cha kiroho badala ya kutumia muda wao wa kuhutubu kuwashambulia wanasiasa wenzao,” akaongeza Askofu huyo.

Matamshi ya Bw Gichere yanakuja siku chache tu baada ya kinara wa upinzani Raila Odinga kuwashtumu baadhi ya viongozi wa kidini kwa kupokea fedha kutoka kwa wanasiasa waliobobea katika uporaji wa mali ya umma.

Bw Odinga alidai pesa nyingi zinazotolewa makanisani kila wikendi na baadhi ya viongozi hupatikana kwa njia za ufisadi na akataka makanisa kuchunguzwa kwa kutumiwa na wanasiasa kama vituo vikuu vya ulanguzi wa fedha.

“Kuna baadhi ya viongozi wa kidini ambao wanazingatia maadili ya Kristo lakini wengine hawafanyi hivyo. Tunafaa kuuliza kunakotoka mamilioni yanayotolewa makanisani kila wikendi. Inakuaje mtu hulipwa mshahara wa Sh1 milioni ilhali anatoa mchango wa Sh20 milioni kila mwezi?” akauliza Bw Odinga.

Kasisi Mkenya achaguliwa askofu wa Kianglikana New Zealand

CHARLES WASONGA na MASHIRIKA

KASISI Mkenya, Steve Maina, amechaguliwa kuwa Askofu Mpya wa Kanisa la Kianglikana katika jiji la Nelson, nchini New Zealand.

Maina alitawazwa kuwa kasisi mnamo mwaka wa 2004 baada ya kuhudumu katika matawi kadha ya Kianglikana katika Kaunti ya Nairobi.

Kwenye taarifa iliyochapishwa kwenye vyombo vya habari nchini New Zealand, maaskofu wakuu wa Kanisa la Kianglikana katika madayosisi ya Aoteorea na Polynesi waliommiminia sifa Bw Maina walimtaja kama mtumishi ambaye amekuwa akihudumu kwa bidii na kujitolea.

“Steve analeta huduma yenye mwelekeo katika nyanja zote na anaheshimiwa kwa bidii na kujitolea kwake kuendeleza injili,” wakasema Maaskofu hao wakuu.

Waliongeza kuwa uongozi wake uongozi wa Maina amewasaidia vijana na watu wengi ambao amewahi kuwahudumia.

“Steve analeta moyo wa utumishi na fikra nzuri katika yale yote anayofanya katika kanisa hili, wakasema.

Maina ambaye alizaliwa mnamo 1970 atachukua mahala pa Richard Ellena, atakapotawazwa rasmi.

“Nimefurahi kwa kuchaguliwa kwa wadhifa huu na ninaukubali kwa unyenyekevu,” akasema.

“Je, mtoto wa Afrika anaweza kuchaguliwa? Mtu kutoka Kenya? Niko na hamu ya kuhudumu,” Bw Maina akaendelea kusema.

Askofu aitaka NASA ikubali Uhuru Kenyatta ni Rais halali

Na SAMMY LUTTA na VALENTINE OBARA

Kwa Muhtasari:

  • Askofu Sapit asema kipindi cha kampeni kilikamilika 2017 na nchi inahitaji utulivu
  • Awataka Wakenya kusubiri hadi 2022 uchaguzi mwingine wa urais utakapoandaliwa
  • Mashauriano ya kisiasa yanafaa yawe kuhusu jinsi sheria za uchaguzi zinaweza kurekebishwa
  • Kiongozi huyo aonya Kenya itabaki nyuma kimaendeleo na kiuchumi hali ya kisiasa nchini ikizidi kushuhudiwa

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Anglikana la Kenya (ACK), Bw Jackson ole Sapit, Jumatatu alisema Muungano wa NASA unafaa kusubiri hadi mwaka wa 2022 ili ushiriki kwenye uchaguzi wa urais kwani Rais Uhuru Kenyatta yuko mamlakani kihalali.

Askofu Sapit alisema kipindi cha uchaguzi kilikamilika 2017 na nchi inahitaji utulivu ili kuleta maendeleo na huduma kwa wananchi baada ya serikali kuundwa.

“Tunahitaji kukomesha siasa na tusubiri hadi 2022 kwani wakati huyo ndio viti vya kisiasa vitakuwa wazi kikatiba na wale wanaotaka kuwa wagombeaji wataruhusiwa. Ninaomba walio serikalini na katika upande wa upinzani washauriane kuhusu jinsi ya kuleta umoja kwa Wakenya ambao kwa sasa wamegawanyika kisiasa,” akasema.

Alikuwa akizungumza na wanahabari katika kanisa la St Paul’s ACK, parokia ya Lodwar baada ya kuzindua lango jipya na maduka yaliyojengwa.

 

Uchumi utayumba

Kiongozi huyo wa kidini alisema Kenya itabaki nyuma kimaendeleo na kiuchumi kama hali ya kisiasa itazidi kushuhudiwa kwa muda mrefu huku upande wa upinzani ukitaka mmoja wao awe rais.

Alisema kanisa linaomba kila mmoja nchini akumbatie uwiano na uvumilivu wa kisiasa ili kuwe na amani huku akiongeza kuwa serikali iliyopo inafaa kuwa katika mstari wa mbele kueneza umoja wa kitaifa.

Bw Sapit alisema mashauriano ya kisiasa yanafaa yawe kuhusu jinsi sheria za uchaguzi zinaweza kurekebishwa ili kuhakikisha Uchaguzi Mkuu wa 2022 utafanywa kwa njia bora zaidi.

“Hatuhitaji mashauriano kuhusu jinsi Kenya inaweza kupata rais mpya hivi sasa kwa kuwa nchi tayari ina Rais Uhuru ambaye aliapishwa mamlakani baada ya ushindi wake kukubaliwa na Mahakama ya Juu,” akasema na kusisitiza kuwa nchi haiwezi kuwa na marais wawili kwa wakati mmoja.

 

Msimamo sawa na mabalozi 

Msimamo wake ni sawa na uliotolewa na mabalozi wa nchi za magharibi ambao walimtaka Bw Odinga atambue uhalali wa uongozi uliopo kabla kuwe na mashauriano kuhusu mabadiliko anayotaka.

Bw Odinga alikashifu mabalozi hao 11 na kusema hawana haki ya kuamulia wananchi wa Kenya kuhusu uongozi wanaotaka kwani walionyesha ubaguzi wao wakati wa uchaguzi wa urais mwaka uliopita.

Mshauri wa kiongozi huyo wa Chama cha ODM, Bw Salim Lone, pia alikosoa mabalozi hao na kusema msimamo wao unaweza kufanya pande zote mbili zizidi kuwa na misimamo mikali.

Kulingana naye, Bw Odinga amekuwa mvumilivu kwa muda mrefu na hata aliepuka wito wa wafuasi wake mara nyingi walipomtaka ajiapishe kuwa rais, na hatimaye akajiapisha tu kuwa ‘rais wa wananchi’ na wala si wa Jamhuri ya Kenya.