• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 7:50 AM
Ahadi feki za Ruto kuhusu mahindi 

Ahadi feki za Ruto kuhusu mahindi 

NA SAMMY WAWERU

MALENGO ya Rais William Ruto kuhusu kiwango cha mavuno ya mahindi 2023 yameonekana kutofautiana pakubwa na kauli ya wataalamu. 

Huku kiongozi wa nchi akitangaza kutarajia magunia milioni 66, wataalamu wa masuala ya kilimo wanahoji kupata magunia milioni 33 itakuwa mchongoma – kibarua.

Akizungumza mnamo Jumapili, Agosti 13, 2023 katika Kanisa la Faith Evangelistic Ministry, Karen, Dkt Ruto alielezea imani yake kuwa taifa litatinga kiwango alichotaja.

“Mwaka huu tunapania kuvuna magunia milioni 66 ya mahindi, ikilinganishwa na milioni 44 tuliyovuna mwaka uliopita, 2022,” akasema.

Hata ingawa serikali yake inaendeleza Mpango wa Ruzuku ya Mbolea, Rais hata hivyo, alikiri ongezeko hilo limechochewa na kiwango kikubwa cha mvua kilichopokewa 2023.

Ruto, aidha, alisema mvua ya mwaka huu imekuwa bora ikilinganishwa na ya miaka ya awali, hasa kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Matarajio ya Rais, hata hivyo, yanaonekana kukinzana pakubwa na ya wataalamu wa kilimo na Wanasayansi.

Kulingana na Dkt James Karanja, kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo cha Mimea na Uimarishaji Mifugo (Kalro), kituo cha Kabete, kufikisha zaidi ya magunia milioni 35 itakuwa kibarua.

Kauli ya mtaalamu huyo, anasema uzalishaji nafaka nchini umelemewa na mdudu hatari na mharibifu aina ya stalk borer.

“Mwaka huu, 2023 haitakuwa rahisi Kenya kuvuna zaidi ya magunia milioni 35 kwa sababu ya kero ya stalk borer. Ni mdudu hatari na mharibifu kwa mihindi,” afisa huyo akasema.

Nchi inapoteza mazao mengi kutokana na mdudu huyo, Dkt Karanja akidokeza kwamba amepunguza uzalishaji mahindi hadi chini ya magunia 23 ya kilo 90 katika kila ekari.

Mwanasayansi huyo pia alitaja kero ya viwavijeshi kama changamoto nyingine inayozingira uzalishaji mahindi Kenya.

“Shabaha inapaswa kuwa magunia 42 kwa kila ekari, lakini stalk borer ndio kizingiti kikuu.”

Mbali na takwimu za Rais Ruto kutofautiana na za Kalro, pia zinakinzana na za Wizara ya Kilimo, iliyotangaza awali kwamba taifa linatarajia kuvuna magunia milioni 44 mwaka huu.

Mwaka 2021, Kenya ilivuna magunia milioni 36.7 ya mahindi.

Kiwastani, nchi inahitaji kati ya magunia milioni 50 hadi 52 kutosheleza ulaji kila mwaka.

Kwa muda mrefu, Kenya imekuwa ikiagiza mahindi kutoka nje ya nchi kuziba gapu iliyopo ya uzalishaji.

  • Tags

You can share this post!

Ruto ahimiza wakulima kugeukia Mungu kupata mazao tele  

Najib Balala alaumiwa kwa kuangusha hoteli za kifahari Nyeri

T L