Makaka kuzikwa Jumamosi kijijini Imukhonje

Na JOHN ASHIHUNDU

SALAMU za pole ziliendelea kumiminika kufuatia kifo cha ghafla cha mchezaji raga, Allan Makaka aliyeaga dunia kwenye ajali barabarani mwishoni mwa wiki jana.

Rambirambi hizo ni pamoja na za kocha Paul Murunga wa Homeboyz RFC ambaye walicheza naye katika kikosi cha Ulinzi mnamo 2000.

Risala zingine zilitoka kwa aliyekuwa kocha wa timu ya taiufa, Edward Rombo pamoja na wachezaji wastaafu, Innocent Simiyu, Sydney Ashioya, Dennis Mwanja waliomtaja kama mchezaji aliyekuwa na bidii na kasi ya kutisha uwanjani.

Makaka ambaye alifariki usiku wa kuamkia Jumapili katika ajali ya gari kwenye barabara ya Mombasa Road alikuwa mchezaji wa timu ya taifa ya kikosi cha Shujaa na pia klabu za Ulinzi RFC na Kenya Harlequines kabla ya kustaafu mnamo 2008 kutokana na jeraha la goti.

Kulingana na babake mzazi, Macdonald Makaka, marehemu zamani mwanafunzi wa Musingu High na Chuo Kikuu cha USIU atazikwa Jumamosi katika kijiji cha Imukhonje, Isukha Magharibi, tarafa ya Shinyalu katika Kaunti ya Kakamega.

Makaka aliyefariki akiwa na umri wa miaka 37 alikuwa katika kikosi cha Shujaa kilichoshiriki katika Kombe la Dunia la (World Cup Sevens) 2005 Hong Kong, pamoja na Michezo ya Madola ya 2006 nchini Australia.

Aliicheza timu ya taifa mara 57 na kuifungia mabao 28.

Aliisaidia Harlequins kutwaa ubingwa mnamo 2005, 2006 pamoja na taji la Kenya Cup mnamo 2008.

Makaka alikuwa meneja wa kitengo cha uuzaji cha HOT 96 FM cha shirika la utangazaji la Royal Media Services kwa miaka minane.

TANZIA: Nyota wa zamani wa timu ya taifa raga Allan Makaka afariki

Na GEOFFREY ANENE

KENYA imeamkia habari za kuhuzunisha Jumamosi baada ya kumpoteza nyota wake wa zamani wa timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande Allan Makaka Shisiali katika ajali mbaya ya barabarani iliyotokea saa sita usiku.

Makaka, ambaye alipeperusha bendera ya Kenya katika Kombe la Dunia 2005 mjini Hong Kong na Jumuiya ya Madola 2006 mjini Melbourne nchini Australia, alikuwa katika gari ndogo alipogonga lori lililokuwa limesimama kwenye barabara ya Mombasa Road kutoka nyuma.

Mchezaji huyu wa zamani wa klabu za Ulinzi na Kenya Harlequin alizaliwa mnamo Juni 28 mwaka 1982.

Alisomea katika Shule ya Msingi ya Mumias Boys kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya Musingu katika Kaunti ya Kakamega na kisha kupata digrii katika Chuo Kikuu cha USIU katika eneobunge la Kasarani katika Kaunti ya Nairobi.

Wakati wa kifo chake, Makaka ambaye alichezea Kenya jumla ya mechi 57 na kuifungia miguso 28 kwenye Raga ya Dunia, alikuwa meneja katika Shirika la Habari la Royal Media Services.

Mwili wake umepelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Montenzuma kusubiri mazishi.