• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
ANC kusajili wanachama wapya

ANC kusajili wanachama wapya

Na CHARLES WASONGA

SENETA wa Kakamega Cleophas Malala amesema Jumapili chama cha Amani National Congress (ANC) kitaanzisha usajili wa wanachama wapya kote nchini kama sehemu ya matayarisho yake kwa uchaguzi mkuu ujao.

Amesema shughuli hiyo itaendeshwa kwa njia ya mtandao wa Intaneti na mitandao ya kijamii kutokana na masharti yaliyowekwa kuzuia kuenea kwa Covid-19.

Bw Malala amesema usajili huo wa wanachama wapya unalenga kuvumisha chama hicho ambacho amesema kimeelekeza “macho yake yote kwa uchaguzi mkuu wa 2022.”

“Kwa sababu vyama vyote vinajiandaa kwa uchaguzi mkuu ujao, sisi kama ANC hatutaki kuachwa nyuma. Hii ndio maana hivi karibuni tutazindua mchakato wa usajili wa wanachama wapya kote nchini japo kwa njia ya mitandao,” akasema alipohudhuria ibada ya Jumapili katika Kanisa la Jeshi la Wokovu, eneo la Majengo, Mombasa.

Vile vile, Bw Malala amesema muungano wa “One Kenya Alliance” unaowaleta pamoja kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi, kiongozi wa KANU Gideon Moi, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang’ula unalenga kuendelea siasa zinazoshirikisha watu wote.

“Kwa hivyo, natoa wito kwa magavana Hassan Joho (Mombasa), Salim Mvurya (Kwale) na Amason Kingi, wanaohudumu mihula yao ya pili na ya mwisho kujiunga na muungano huu wetu,” akasema Seneta huyo wa Kakamega.

Wiki jana, Bw Malala aling’olewa kutoka wadhifa wa Naibu Kiongozi wa Wengi ambao ameushikilia kwa zaidi ya mwaka mmoja. Hii ni baada ya maseneta wa ODM kudai kuwa Seneta huyo alimkosea heshima kiongozi wa chama hicho Raila Odinga katika uchaguzi mdogo eneobunge la Matungu uliofanyika Machi 4, 2021.

You can share this post!

Watu 13 waangamizwa na corona

Wito serikali ipige jeki sekta ya juakali