• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
AU, UN zaunga jeshi la EAC kukabili waasi DRC

AU, UN zaunga jeshi la EAC kukabili waasi DRC

NA THE EAST AFRICAN

KINSHANSA, DRC

MPANGO wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kutaka kuunda jeshi litakalokabiliana na waasi katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) umeungwa mkono na Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa (UN).

AU na UN pia waliunga juhudi za kutaka kupatanisha serikali ya DRC na makundi ya waasi ambayo yamekuwa yakihangaisha raia katika nchi hiyo yenye utajiri wa madini.

Mwenyekiti wa Tume ya AU Moussa Faki Mahamat alisema kuwa anaunga mpango huo uliopitishwa na viongozi wa mataifa ya EAC walipokutana jijini Nairobi wiki iliyopita.

Faki pia alihimiza majirani za DRC kuendelea kutekeleza mkataba wa 2013 ambapo nchi za Angola, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Congo, Rwanda, Afrika Kusini, Sudan Kusini, Tanzania, Uganda na Zambia ziliafikiana kutotoa maficho kwa waasi na wahalifu wa kivita.Nchi hizo jirani pia ziliafikiana kusaidia DRC kuimarisha taasisi zake.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ambaye ni mwenyekiti wa EAC, wiki iliyopita, aliongoza kikao cha viongozi wa nchi za Afrika Mashariki ambapo waliafikiana kuunda jeshi la pamoja kupambana na waasi nchini DRC.

Mkutano huo ulihudhuria na marais Kenyatta, Yoweri Museveni wa Uganda, Felix Tshisekedi wa DRC na Evariste Ndayishimiye wa Burundi na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Rwanda Vincent Biruta aliyewakilisha Rais Paul Kagame.

Waliafikiana kuwa serikali ya DRC ianze kwa kufanya mkutano na makundi ya waasi.

Kenya ilijitolea kuwa mwenyeji wa mazungumzo hayo.

“Makundi yote ya waasi nchini DRC yajitokeze kufanya mazungumzo na serikali bila masharti ili kero zao zitatuliwe. Kundi litakalokosa kushiriki mazungumzo hayo litachukuliwa kuwa adui na litakabiliwa vikali na jeshi la pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki,” ikasema taarifa iliyotolewa baada ya kikao hicho cha viongozi wa nchi za EAC.

Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres alisema kuwa anaunga mkono juhudi za mataifa ya Afrika Mashariki kutaka kurejesha amani nchini DRC.

Guterres alitoa hakikisho hilo alipokuwa akizungumza na Rais Kenyatta kwa njia ya simu.Serikali ya DRC imekataa kushiriki mazungumzo na kundi la waasi wa M-23 baada ya kuendeleza mashambulio katika eneo la Bukasa, Kivu Kaskazini.

Kulingana na serikali ya DRC, washambuliaji wa M-23 wanaotekeleza mashambulio katika eneo la Kivu Kaskazini wamejificha katika nchi jirani ya Uganda.

Lakini kundi la M-23 lilidai kuwa lilitekeleza mashambulio baada ya kuchokozwa na wanajeshi wa DRC.

Makundi 15 ya waasi yamekuwa yakifanya mazungumzo ya amani na wawakilishi wa serikali ya DRC tangu Ijumaa, wiki iliyopita.

Makundi ya waasi yanayoshiriki mazungumzo hayo ni Gumino, Raia Mutomboki, FPDC, Twiraneho, UPSP na makundi mengine matatu yaliyojitenga kutoka kwa M-23.

Makundi mengine tisa yanatarajiwa kujiunga na mazungumzo hayo.

  • Tags

You can share this post!

Liverpool wapepeta Villarreal katika mkondo wa kwanza wa...

GWIJI WA WIKI: Heman Gitaa Angwenyi

T L