• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
BAHARI YA MAPENZI: Bosi wa kijakazi mume au mke?

BAHARI YA MAPENZI: Bosi wa kijakazi mume au mke?

SIZARINA HAMISI Na BENSON MATHEKA

WANASEMA ukitaka kuishi vizuri na mkeo ama mumeo, elewa yale yanayomhusu na yale pia yasiyomhusu.

Kwamba wanandoa wanapoanza maisha ya pamoja ni vyema kuweka bayana majukumu na wajibu wa kila mmojawao katika ndoa.

Katika makubaliano haya ni vyema pia kuweka wazi kuhusu suala la msaidizi wa shughuli za nyumbani ambaye siku hizi amekuwa ni sehemu kubwa ya maisha ya wanandoa. Mara nyingi katika familia, mwenye jukumu la usimamizi wa shughuli za nyumbani ni mke, naye ndiye husimamia utekelezaji wa yale ya muhimu pale.

Kwa upande mwingine, mume pia anaweza kutaka ashirikishwe katika maamuzi ya yule anayepatiwa jukumu la kazi za nyumbani. Mara nyingi waume huwaachia jukumu hili wake zao kwa maelewano kwamba ndio wenye mamlaka ya kuajiri ama kufukuza, mradi shughuli za nyumbani na maisha ya wahusika yasitetereke.

Changamoto kubwa ambayo wake wamekuwa wakikutana nayo katika uajiri wa hawa wasichana wa kazi ni kwamba wakati mwingine mume naye anakuwa na malengo yake binafsi ambayo huenda asiyaweke wazi, bali anaweza kuyatenda. Na mara nyingi hili ni jambo ambalo wake hulizingatia pale msaidizi wa shughuli za nyumbani anapoajiriwa.

Wanasema mtu aliyeumwa na nyoka akiona unyasi atashtuka. Kumekuwa na habari nyingi za waume kuwachangamkia wasichana wa kazi na kuwageuza wake wa pili. Ndiposa katika hali hii wanapokuwa mstari wa mbele kutaka kujua ni msichana gani anaajiriwa na kuamua ni yupi aajiriwe na yupi asiajiriwe, ni wazi kwamba kunakuwa na ukakasi katika shughuli hii ya uajiri.

Tumewasikia waume ambao msichana wa kazi anapoajiriwa, basi mwelekeo wao wote unageuka kwa msichana. Chakula kikipikwa vizuri anamsifia msichana na kusahau mkewe ndiye anayepanga na kuweka utaratibu huko jikoni. Wapo wale ambao wanafikia hatua ya kudai wafanyiwe shughuli fulani na wasichana wa kazi na kusahau kwamba mke ndiye ambaye anatakiwa ashirikishwe katika yale masuala yanayomhusu.

Katika hili wapo pia wasichana wa kazi ambao wanakuja kwa makusudi maalum ya kupindua serikali na kuteka hisia na mapenzi ya baba mwenye nyumba. Na zipo ndoa zilizovunjika sababu yao. Na ndio maana linapokuja suala hili, ni vyema kumuachia mke ashike usukani kwani anaweza kunusa hiyana ikiwa kilomita hamsini na akajua nia ya msichana wa kazi iwapo ni kutafuta kibarua ama mengineyo.

Wapo wasichana ambao ni washirikina, wanaingia katika nyumba za watu kwa malengo ya kutenda matendo ya kiibilisi na mara nyingi mke ni rahisi kung’amua kwani mengi yanayotendeka nyumbani huwa yanaeleweka zaidi na mama mwenye nyumba.

Hivyo pale mkeo anapoamua kumtimua msichana ama kumuajiri, ni vyema kuelewa na wakati mwingine kumuachia jukumu hilo, kwani huenda anaelewa na anaona mengi kuliko unavyoweza kung’amua.

Muhimu ni kushirikiana katika maamuzi na majukumu, lakini wakati mwingine kumuachia mke atimize yale yanayomhusu.

[email protected]

MAJUZI nilishuhudia mzozo mkali kwa jirani yangu akimlaumu mkewe kwa kuajiri wafanyakazi ‘wachafu’ wa nyumbani.

Ni mzozo uliovutia majirani wengine na kuaibisha wanandoa hao ambao walianika siri zao kwetu.

Hali hii haingetokea iwapo mume hangeingilia chaguo la mkewe la mfanyakazi wa nyumbani au kama mkewe angesikiliza ushauri wa mumewe kuhusu mfanyakazi huyo ambaye sisi kama watazamaji wa kioja hicho, tulikubaliana kwa kauli moja hakuwa ‘mchafu’ ilivyodaiwa.

Baadaye tulibaini kwamba mke wa jirani alikuwa amekataa mwanadada ambaye mumewe alitaka awe kijakazi wao.

Katika ndoa kuna majukumu ambayo hata kama mume ni kichwa cha familia hafai kushughulika nayo moja kwa moja. Haya ni majukumu ambayo mkewe anahusika nayo moja kwa moja kama ya jikoni, na anachoweza kufanya mwanamume kamili ni kutoa ushauri na kuacha mkewe kufanya uamuzi. Hapa ndipo suala la kuajiri wafanyakazi wa nyumbani linapoibuka.

Katika baadhi ya familia, suala hili limekuwa likizua utata na hata ugomvi ilivyokuwa kwa jirani yangu pale mume na mke wanapotofautiana kuhusu anayefaa kuajiriwa. Hasa, ugomvi huzuka mume anapokosoa chaguo la mkewe la mfanyakazi wa nyumbani kwa sababu moja au nyingine. Mume anaweza kuchukia kijakazi anayeajiriwa na mkewe na kuamua kuchukua jukumu la kuajiri anayetaka hata kama anayechukiwa ni mchapa kazi na ana nidhamu.

Niseme wazi kwamba wanaume wanaofanya hivyo huwa na nia fiche kwa kuwa umuhimu wa kijakazi ni kazi anayofanya na sio mtindo wake wa mavazi au sura yake jinsi baadhi yao wanavyodai. Na sisemi wawe wachafu hata kama wanachapa kazi.

Ukweli ni kwamba wanaume hawafai kujitwika jukumu la kuajiri wafanyakazi wa nyumbani wa kike na ikiwezekana, wake hawafai kuajiri wafanyakazi wa nyumbani wanaume. Kuna wanaoweza kunipura mawe kwa msimamo wangu huu hadi pale watakapogundua hekima iliyopo kwa kuachia wanawake jukumu la kuajiri vijakazi na wanawake kuachia waume jukumu la kuajiri ‘house boy’, ‘shamba boy’ na walinzi.

Kumekuwa na malalamishi mengi ya wanaume kubadilisha vijakazi kuwa mipango ya kando au hata kuajiri mipango yao ya kando kuwa wafanyakazi wa nyumbani. Wanawake pia wamekuwa wakiajiri wa pembeni kuwa wafanyakazi wa nyumbani. Ili kuepuka hali hii, waume wanafaa kuachia wake zao jukumu la kuajiri na kufuta kazi vijakazi. Hii itadumisha amani katika boma.

Hata hivyo, hakuna makosa wanandoa kushauriana kuhusu mfanyakazi anayefaa hasa ikiwa kuna watoto. Kupitia mashauriano, mke anaweza kupatia mumewe ruhusa ya kumsaidia kutafuta mfanyakazi wa nyumbani lakini mume asifanye kosa la kumlazimisha mkewe kuajiri chaguo lake. Mkeo akikataa unayependekeza, heshimu uamuzi wake.

Makosa mengine ambayo wanaume hufanya ni kuwalipa wafanyakazi wa nyumbani moja kwa moja ingawa huwa wameajiriwa na wake zao.

Mwanamume anayefanya hivi huwa anaalika balaa. Lipa wafanyakazi wengine wote na hata ulipe karo ya shule moja kwa moja lakini busara inahitaji kwamba upitishie mshahara wa mfanyakazi wa nyumbani kwa mkeo ambaye ndiye bosi wake.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

PENZI LA KIJANJA: Ashiki ni kama pombe, ukilewa...

Brentford yaduwaza Man-City katika EPL ugani Etihad

T L