Utalii, uwekezaji kuimarika Pwani – Wadau

Na KNA

KUZINDULIWA kwa Bandari ya Lamu pamoja na ujenzi wa barabara za kisasa kutaimarisha sekta ya utalii katika ukanda wa Pwani.

Kulingana na wadau katika sekta hiyo, kufunguliwa kwa bandari, kuboreshwa kwa barabara na kupanuliwa kwa uwanja mdogo wa ndege wa Manda kutainua hadhi ya kisiwa cha Lamu kama eneo la utalii na uwekezaji.

“Uboreshaji wa miundomsingi huchangia mno kuimarisha sekta za utalii na uchukuzi,” akasema Bw Said Swabu, ambaye ni mkurugenzi mkuu wa mkahawa wa Betlysalam Resort.

Bw Swabu alisema eneo hilo litafaidika pakubwa kiuchumi kutokana na uboreshaji wa barabara na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Manda.

Aliisifu serikali kwa kuwekeza pakubwa katika ujenzi wa barabara mpya, kuimarisha zilizopo na kuboresha shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.

“Kaunti hii sasa itakuwa eneo la kipekee la kitalii na uwekezaji, na litapata utambulisho maalum kote duniani,” akasema Bw Swabu.

Hata hivyo, aliongeza kuwa kaunti hiyo bado inakumbwa na changamoto nyingi za uhaba wa maji na matatizo ya umeme.

Hivyo, aliziomba serikali ya kitaifa na ile ya kaunti kutatua suala hilo.