• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 6:50 PM
Barca 16-bora kwa nyanyaso za Messi

Barca 16-bora kwa nyanyaso za Messi

Na MASHIRIKA

BARCELONA, Uhispania

LIONEL Messi alihakikisha kuwa mechi yake ya 700 akiwa mwanasoka wa Barcelona inakuwa ya kihistoria alipopachika bao lake la 613, huku miamba hao wa Uhispania wakichabanga Borussia Dortmund 3-1 na kuingia raundi ya 16-bora ya kabumbu ya Klabu Bingwa Ulaya, Jumatano.

Messi alisherehekea mchuano huo kwa kupachika bao la pili pamoja na kumega pasi zilizofungwa na Luis Suarez na Antoine Griezmann uwanjani Camp Nou.

“Alikuwa stadi,” alisifu kocha wa Barcelona, Ernesto Valverde. “Mchezo wake ulituwezesha kujikatia tiketi ya kusonga mbele.”

Muingereza Jadon Sancho alipatia Dortmund bao la kufutia machozi dakika za lala-salama, lakini wageni hao ambao hawakuridhisha kwa kipindi kikubwa, sasa wako katika vita vya kufa kupona dhidi ya Inter Milan kuamua nani kati yao ataungana na Barca kutoka Kundi F.

Dortmund itatumai kupepeta Slavia Prague uwanjani Westfalenstadion wiki mbili zijazo na pia itategemea Barcelona isipigwe uwanjani San Siro ili iingie mduara wa 16-bora.

“Kwa maoni yangu, tulitiwa katika kundi ngumu sana katika mashindano haya,” alisema Valverde. “Tumeingia mduara wa 16-bora tukisalia na mechi moja, kama washindi wa kundi hili, na kwa wachezaji ni kitu muhimu sana.”

Huku Real Madrid ikionekana kuamka wakati huu, Barca imekuwa ikichechemea, ingawa imebahatika kupata matokeo mazuri kwenye Ligi Kuu ya Uhispania. Mkombozi wa Barca kwa kiwango kikubwa amekuwa Messi, ambaye sasa ameona lango mara 10 katika mechi tisa, huku tuzo ya kifahari ya mwanasoka bora duniani ya Ballon d’Or ikinukia.

Mbali na kutikisa nyavu mara 613, Messi amechangia pasi 237 katika mechi 700 za Barca.

Kwa Barcelona, kilichoitia wasiwasi ni Ousmane Dembele kutoka uwanjani akichechemea katika kipindi cha kwanza. Dembele huenda akakosa gozi la Clasico dhidi ya Real Madrid mnamo Desemba 18.

“Tumefuzu, ingawa habari za kuvunja moyo ni kuwa Dembele ameumia.”

Dembele alikuwa akitegemewa kuliko Griezmann, ambaye alijaza nafasi yake, huku Ivan Rakitic akipata kuanzishwa mechi kwa mara ya kwanza tangu Septemba 21.

Rakitic alianza mechi vibaya alipopoteza mpira na kupatia Dortmund fursa yake nzuri ya kwanza katika dakika ya kwanza. Hata hivyo, beki Samuel Umtiti na kipa Marc-Andre ter Stegen waliepushia Barca madhara walipoondosha hatari hiyo.

Rakitic pia alipata fursa ya kupachika bao, lakini ngome ya Dortmund ikazuia shuti lake. Messi alimegea Suarez pasi, ambayo raia huyo wa Uruguaya alifunga, lakini akapatikana amerombeza.

Hata hivyo, walishirikana tena vyema kuzalisha bao la kwanza pale pasi ya Suarez kwa mchezaji Junior Firpo ilirejea kwa Messi. Messi kisha alipasia Suarez mpira murwa na mshambuliaji huyo akamwaga kipa Roman Burki na kuweka Barca bao 1-0 juu dakika ya 29.

Messi alifanya mabao kuwa 2-0 baada ya Suarez kummegea pasi safi kabla ya Griezmann kuimarisha uongozi huo dakika ya 67 alipopokea pasi kutoka kwa Messi.

Sancho, ambaye alijaza nafasi ya Nico Schulz mapema katika kipindi cha pili, alifungia Dortmund bao la kujifariji dakika ya 77.

You can share this post!

Mshukiwa wa tatu mauaji ya mwanamke na wanawe wawili...

Joshua Kipkorir na Priscah Cherono ni miongoni mwa...

adminleo