• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
CHAMBO CHA MBU: Ikiwa husumbuliwa na mbu sana, basi msaliti damu yako

CHAMBO CHA MBU: Ikiwa husumbuliwa na mbu sana, basi msaliti damu yako

Na LEONARD ONYANGO

JE, wewe ndiye pekee unasumbuliwa na mbu usiku huku wenzako mlio kwenye chumba kimoja wamelala usingizi wa pono?

Basi, huenda damu yako ndiyo imekusaliti.

Mbu wa kike ambao hunyonya damu hupendelea zaidi baadhi ya watu na kupuuzilia mbali wengine.

Mbali na aina ya damu, mbu pia hunyemelea harufu ya aina fulani za sabuni au manukato.

Kulingana na wataalamu wa afya, watu wenye damu aina ya ‘O’ hupendelewa zaidi na mbu ikilinganishwa na wenzao walio na damu aina ya ‘A’, ‘B’ au ‘AB’.

Watu wenye damu aina ya ‘O’ huumwa na mbu zaidi ya mara tatu ikilinganishwa na wenzao.

Watafiti, hata hivyo, hawajabaini ni kwa nini mbu hupendelea damu aina ya ‘O’.

Mbali na aina ya damu, watu walio na aina fulani ya kemikali katika ngozi zao pia hupendelewa na mbu.

Wabugiaji wa mvinyo pia huwa kivutio kwa mbu.

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Matibabu cha Toyama nchini Japan ulibaini kuwa mtu anayekunywa chupa moja tu ya bia hugeuka kuwa kivutio cha mbu ikilinganishwa na watu wengine ambao hawajaonja.

Katika utafiti wao, wanasayansi hao walihusisha wanaume 12 wa kati ya umri wa miaka 20 na 58 pamoja na mwanamke mmoja wa umri wa miaka 12.

Wanaume wote walikunywa viwango tofauti vya pombe na mwanamke hakuonja kileo.

Baadaye walipima mbu wa waliotua kumuuma kila mmoja. Walibaini kwamba watu waliokuwa wamekunywa pombe, akiwemo aliyekunywa glasi moja ya mvinyo, waliumwa na mbu mara nyingi zaidi ikilinganishwa na mwanamke ambaye hakuwa amekunywa mvinyo.

Wataalamu wanasema kuwa mbu huvutiwa na gesi aina ya kabon-dioksaidi kutoka umbali wa mita 60.

Unapofanya mazoezi na kutokwa na jasho, kwa mfano, mwili hutoa gesi ya kaboni na kemikali aina ya ‘lactic acid’.

Gesi hiyo pamoja na kemikali hizo ni kivutio kikubwa cha mbu.

Joto jingi

Mwili unapokuwa na joto pia huvutia mbu hao wa kike.

Wataalamu wa afya wanashauri mtu kuoga baada ya kufanya mazoezi au shughuli nzito kabla ya kulala kama njia mojawapo ya kujikinga na mbu.

Wanawake wajawazito wako katika hatari ya kuumwa na mbu maradufu kwa sababu wanatoa gesi aina ya kabondioksaidi kwa asilimia 20 zaidi ikilinganishwa na watu wengine.

Kadhalika, akina mama wajawazito huwa na joto zaidi ambalo ni kivutio cha mbu.

Wataalamu wanashauri kuwa mbali na kutumia neti ya kujikinga na mbu, kuna haja ya kuondoa maji yaliyokwama kando ya nyumba. Maji hayo huwa makao ya kuzaana kwa mbu.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema kuwa malaria huathiri kwa kiasi kikubwa watoto walioko tumboni.

Mwaka jana watafiti wa Taasisi ya Kutafiti Matibabu nchini (Kemri) walivumbua dawa ya kuzuia malaria kudhuru mama na mtoto.

Dawa hiyo iliyofahamika kama dihydroartemisinin-piperaquine (DP), ilibainika kuwa salama zaidi ikilinganishwa na dawa inayotumiwa sasa ya Fansidar.

You can share this post!

MAZINGIRA NA SAYANSI: Kemikali za kuua wadudu hulemaza...

PATA USHAURI WA DKT FLO: Maumivu kooni yanitia wasiwasi

adminleo