Walioingia mitini

WANDERI KAMAU na LEONARD ONYANGO

KUSAMBARATIKA kwa Mpango wa Kubadilisha Katiba (BBI) na sintofahamu kuhusu mwelekeo wa siasa za 2022, imefanya baadhi ya wanasiasa waliokuwa watetezi wa kufa kupona wa vigogo wakuu wa kisiasa nchini, kunyamaza.

Idadi kubwa ya wanasiasa hao walikuwa watetezi sugu wa Rais Uhuru Kenyatta, kiongozi wa ODM, Raila Odinga na Naibu Rais William Ruto.

Wengi wa wanasiasa hao wameingia ‘mafichoni’ katika siku za hivi karibuni na wamekuwa wakikwepa kuandamana na Bw Odinga au Dkt Ruto ambao wameimarisha kampeni zao wakijiandaa kwa kinyang’anyiro cha urais Agosti 9, 2022.

Katika kambi ya Rais Kenyatta na Bw Odinga, baadhi ya watetezi wao waliofyata midomo ni Naibu Mwenyekiti wa Chama cha Jubilee David Murathe, Mbunge Maalum Maina Kamanda, mwanasiasa Peter Kenneth, wabunge Jared Okello (Nyando), Joshua Kutuny (Cherengany), Alfred Keter (Nandi Hills), Naisula Lesuuda (Samburu Magharibi), Mpuru Aburi (EALA), Peter Kaluma (Homa Bay Mjini), Florence Mutua (Busia) kati ya wengine.

Miongoni mwa waliokuwa watetezi sugu wa Dkt Ruto ambao wameamua kusalia kimya ni Seneta wa Tharaka Nithi Kithure Kindiki, wabunge John Paul Mwirigi (Igembe Kusini), Owen Baya (Kilifi Kaskazini), Khatib Mwashetani (Lungalunga), Vincent Musyoka ‘Kawaya’ (Mwala), Patrick Makau (Mbooni) kati ya wengine.

Baadhi ya wanasiasa pia wameamua kunyamaza baada ya kubaini kwamba viongozi wao wa vyama wana uhusiano wa karibu na wapinzani wao.

Ingawa baadhi yao wanadai “kujishughulisha kuwahudumia wananchi” au kujiendeleza kimasomo, Taifa Jumapili imebaini misimamo ya wengi wao imechochewa na hali ya kutotabirika kwa siasa zinazoendelea nchini.

“Huu ni wakati muhimu sana kwa wanasiasa kufanya uamuzi utakaohakikisha hawajipati kwenye baridi ya kisiasa baada ya uchaguzi mkuu wa 2022. Licha ya kuwa watetezi wa vigogo wakuu wa kisiasa, lazima wahakikishe hawapotezi ushirikiano wao na wananchi,” asema Bw Dismus Mokua, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Kimya cha Prof Kindiki hata kuhusu siasa za Kaunti ya Tharaka Nithi kimewakanganya wanasiasa wanaomezea mate kiti cha ugavana.

Seneta Kindiki katika miezi ya hivi karibuni amejitenga na Dkt Ruto na amekuwa akizunguka kutoka kijiji kimoja hadi kingine katika Kaunti ya Tharaka Nithi lakini hajatangaza atawania kiti kipi mwaka 2022.

“Niliamua kurudi nyumbani kutangamana na wenyeji wa Tharaka-Nithi ili kufahamu matatizo yanayowakabili. Baada ya kupokonywa wadhifa wa Naibu Spika wa Seneti, niliamua kurejea nyumbani kutumia muda wangu mwingi kuingiliana na wenyeji,” akasema Prof Kindiki huku akisisitiza kuwa angali anaunga mkono Dkt Ruto.

Kabla ya kimya chake cha ghafla, Bw Murathe ndiye alikuwa akionekana kama ‘sauti’ ya Rais Kenyatta na Bw Odinga, hasa wakati wa kampeni za kuipigia debe BBI.

Semi zake ziligeuka kuwa ‘utabiri’ wa kisiasa, ambao mara nyingi ulitimia wiki ama siku chache baadaye.

Alikuwa akifanya mahojiano na vyombo tofauti vya habari, huku kauli zake zikiutikisa sana mrengo wa ‘Tangatanga’ ambao humuunga mkono Dkt Ruto.

Baadhi ya utabiri wake uliotimia ni kufurushwa kwa maseneta sita ‘waasi’ kutoka Chama cha Jubilee (JP).

Bw Murathe pia ‘alitabiri’ kufurushwa kwa mbunge Caleb Kositany (Soy) kama Naibu Katibu Mkuu wa chama.

Alijijengea ushawishi mkubwa kiasi kwamba Dkt Ruto alianza kumtaja moja kwa moja kwenye hotuba zake, kama miongoni mwa watu waliochangia kusambaratika kwa JP.

“Bw Murathe na (Katibu Mkuu) Raphael Tuju ndio sababu kuu za kuvurugika kwa Jubilee,” alidai Dkt Ruto.

Wengine waliojijengea ushawishi huo ni Bw Kamanda. Kabla ya kutupwa kwa BBI na korti, mbunge huyo Maalumu alikuwa akiandamana na Bw Odinga katika maeneo mbalimbali nchini ukiwemo ukanda wa Mlima Kenya, akisisitiza kuwa kinyume na awali, eneo hilo litamuunga mkono kikamilifu kutokana na ushirikiano ambao amempa Rais Kenyatta kupitia kwa handisheki.

Bw Kamanda amewahi kunukuliwa akisema kuwa BBI ndiyo ilikuwa imeweka pamoja Rais Kenyatta na Bw Odinga na kutupwa kwake lilikuwa pigo kubwa.

Mbunge Keter anadai kimya chake kinatokana na hatua yake ya kurejea katika chuo kujiendeleza kimasomo.

“Niliondoka kwenye ulingo wa siasa kwa muda kuangazia masomo yangu. Ninasomea shahada ya uzamili kuhusu Masuala ya Usimamizi wa Biashara (MBA) katika Chuo Kikuu cha Nairobi,” akasema kwenye mahojiano.

Bw Keter, hata hivyo, ameonyesha nia ya kuelekea mrengo wa Dkt Ruto huku akilenga kuwania ugavana wa Nandi.

Mbunge Mwirigi naye anasema kwamba ameamua kurudi nyumbani kuwa karibu na wenyeji, kwani ndio “mabosi wake.”

Wadadisi wa siasa wanasema kuwa wanasiasa wengi walikuwa na matumaini kwamba wangepata nyadhifa mbalimba serikalini endapo BBI ingepita.

“Baada ya BBI kusitishwa na mahakama, wengi waliona kwamba njia ya pekee ambayo wataweza kujiokoa kisiasa ni kurejea walikochaguliwa ili kutopoteza nyadhifa zao. Tutaendelea kushuhudia mwenendo huu kadri uchaguzi unapokaribia,” asema Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Murathe sasa apotosha bunge kuhusu wizi wa mabilioni ya corona

Na LEONARD ONYANGO

NAIBU mwenyekiti wa Jubilee David Murathe Alhamisi alijaribu kupotosha kamati ya Bunge inayochunguza sakata ya wizi wa mabilioni pesa katika Shirika la Kusambaza Dawa (KEMSA).

Hii ni baada ya Bw Murathe kudai kuwa kampuni ya Kilig Limited, ambayo ni moja ya zinazodaiwa kulipwa mabilioni ya sakata ya Kemsa, inamilikiwa na washirika wa Naibu Rais William Ruto.

Lakini alipoitwa baadaye na kamati hiyo, mmoja wa waanzilishi wa Kilig Limited, Wilbroad Gachoka alikanusha madai hayo ya Bw Murathe akisema: “Mimi sina uhusiano wa aina yoyote na Ruto.”

Bw Murathe aliwadhamini wasimamizi wa Kilig Limited na Entec wakati kampuni hizo zilipotuma maombi ya kandarasi kwa Kemsa. Baadaye Kilig Limited ilipata kandarasi ya Sh4 bilioni.

“Hatukuwa na mkataba wowote tuliotia saini na Kilig Limited, bali nilikubali kuwa mdhamini wake kirafiki kwa sababu tunajuana,” akasema Bw Murathe.

Naibu mwenyekiti huyo wa Jubilee na ambaye ni mwandani wa karibu wa Rais Uhuru Kenyatta, alidai amekuwa akiwasimamia watu wengi ambao wamekuwa wakiomba kandarasi, wakiwemo hata wabunge.

“Sijawahi kujihusisha katika biashara au shughuli za kampuni ya Kilig Limited au Entec. Vilevile, sikuwa na uwezo wa kushinikiza Kemsa kulipa kampuni hizo baada kusambaza vifaa vya matibabu ya corona.

“Mimi si Mkurugenzi wa Kilig. Sina mkataba wowote na Kemsa na wala sikuletea mamlaka hiyo kitu chochote. Nilisimamia kampuni hizo lakini sikunufaika na chochote na wala hatukuwa tumeafikiana wanilipe,” akajitetea Bw Murathe.

Stakabadhi za kiapo zilizowasilishwa mbele ya PIC zinaonyesha kuwa Bw Murathe aliacha kuwa mfadhili wa Kilig Limited mnamo Agosti 2020 baada ya Kemsa kufuatilia mbali barua ya makubaliano ya kandarasi.

Wiki iliyopita, Mbunge wa Wajir Mashariki Rashid Amin alisema kuwa ufichuzi kwamba Bw Murathe alikuwa na uhusiano na kampuni ya Kilig Limited ilikuwa ishara kwamba uchunguzi unaoendelea kuhusiana na sakata ya Kemsa imeanza kuzaa matunda.

Raila chaguo la Uhuru 2022 – Murathe

Na WANDERI KAMAU

KUNA uwezekano wa Rais Uhuru Kenyatta kumuunga mkono kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, kuwania urais 2022, licha ya tashwishi ambazo zimeonekana kukumba handisheki katika siku za hivi karibuni.

Kulingana na Naibu Mwenyekiti wa Jubilee, Bw David Murathe, Bw Odinga ndiye mwanasiasa pekee mwenye uwezo, ushawishi na ufuasi mkubwa kisiasa kumkabili Naibu Rais William Ruto, kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

Bw Murathe ni miongoni mwa washirika wa karibu zaidi wa Rais Uhuru Kenyatta na kauli zake zimekuwa zikifasiriwa kuwa “sauti” ya rais.

Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni Jumapili usiku, Bw Murathe alipuuzilia mbali muungano wa One Kenya Alliance (OKA), akisema wanachama wake hawana ushawishi ufaao kisiasa kumkabili Dkt Ruto.

Muungano huo unawashirikisha kiongozi wa ANC, Bw Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka (Wiper), Maseneta Moses Wetang’ula (Ford-Kenya) na Gideon Moi (Kanu).

“Lengo letu ni kuhakikisha (Dkt Ruto) hashindi urais hata kidogo 2022. Kwa mkakati huo, mwanasiasa pekee mwenye uwezo kutimiza hilo ni Bw Odinga. Ana ufuasi katika karibu nusu ya nchi. Huwezi kumpuuza kisiasa hata kidogo,” akasema.

Kauli yake inajiri wakati kumekuwa na tashwishi miongoni mwa washirika wa Bw Odinga katika ODM, kuhusu ikiwa huenda Rais Kenyatta na waandani wake wanamfunga macho kisiasa kupitia handisheki.

Hofu hiyo iliibuliwa na Seneta wa Siaya, Bw James Orengo mwezi uliopita, alipodai kwamba baadhi ya washirika wa Rais Kenyatta walikuwa wakijaribu kumzima kisiasa Bw Odinga, kwa kupanga kisiri kuhusu mchakato wa urithi wake.

“Inasikitisha wakati Rais Kenyatta na Bw Odinga wanaendelea na mikakati ya kuipigia debe ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI), kuna kundi la maafisa wakuu serikalini wanaopanga kuhusu namna Kenya itatawaliwa baada ya rais kung’atuka,” akasema Bw Orengo.

Kauli hiyo ilifuatwa na uvumi kuhusu uwezekano wa Bw Odinga na Dkt Ruto kubuni muungano wa kisiasa, hali inayotajwa kuzua wasiwasi wa kisiasa katika kambi ya Rais Kenyatta.

Hayo yanatajwa pia kuchangiwa na madai kuwa Rais Kenyatta anaupendelea muungano wa OKA kuliko ushirikiano uliopo baina yake na Bw Odinga.

Ni hali iliyowafanya washirika wa Rais Kenyatta kufanya msururu wa mikutano, kumhakikishia Bw Odinga kwamba handisheki ingali thabiti.

Hata hivyo, Bw Murathe alisisitiza kuwa kando na umaarufu wake, Bw Odinga ndiye anayefaa zaidi kuwa rais, kwani ameonyesha uzalendo na uvumilivu mkubwa hata baada ya tofauti za kisiasa kuibuka kati yake na Rais Kenyatta na Rais Mstaafu Mwai Kibaki.

“Bw Odinga ni mwanasiasa ambaye ameonyesha uzalendo wa kweli. Alikubali kubuni serikali ya muungano na Bw Kibaki ili kuleta uthabiti wa kisiasa nchini baada ya ghasia za 2007. Vile vile, alikubali kubuni handisheki na Rais Kenyatta 2018 baada ya utata uliokumba uchaguzi wa 2017 ili kurejesha amani nchini,” akasema.

Wakati huo huo, alieleza mchakato wa vyama vya Jubilee na United Democratic Alliance (UDA) kutengana rasmi kisiasa utafanyika wiki hii.

UDA ilikuwa miongoni mwa vyama washirika vya Jubilee kama Party for Reforms and Development (PDR), lakini ikabadilishwa jina na waandani wa Dkt Ruto.

Murathe asema njama ipo ya kusaidia Raila kutwaa urais wa awamu moja pekee

Na MWANGI MUIRURI

MWANDANI wa kutegemewa wa Rais Uhuru Kenyatta, alisema Jumapili kuwa Wakenya wanafaa wajiandae kumkumbatia kiongozi wa ODM Raila Odinga kama Rais wa Tano mara utakapoandaliwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Bw David Murathe akiwa ndiye pia Naibu Mwenyekiti wa Chama tawala cha Jubilee alisema hayo na huenda yakawa na mashiko kwa sababu matamshi yake ya kisiasa mara nyingi huhusishwa na msimamo wa Ikulu na serikali na huishia “kulenga ndipo”.

Wengi hushikilia kuwa ndiye kipaza sauti cha yaliyo moyoni mwa Rais Kenyatta.

“Hao wengine wanaomezea mate urais katika uchaguzi mkuu wa 2022 kwa sasa waweke nje kwa kuwa Bw Odinga ndiye aliye guu mbele katika urithi huo,” akasema Bw Murathe.

Alisema mwanawe aliyekuwa Rais wa Pili nchini Hayati Daniel Toroitich Arap Moi hana yale makali ya kufanya kampeni ya msisimko unaohitajika kumpeleka Ikulu.

 “Mtu kama Seneta wa Baringo Gideon Moi hana yale makali ya kumenyana na aibuke Rais hivyo afanya uamuzi wa busara ajiunge na merikebu ya ushindi ya Bw Odinga.” akasema.

Alihimiza Bw Moi na wengine kama kiongozi wa ANC Bw Musalia Mudavadi pamoja na kiongozi wa Wiper Bw Kalonzo Musyoka na wengine wajiunge pamoja wagawane nyadhifa nyingine ambazo zitaibuka iwapo mswada wa marekebisho ya Katiba kupitia mchakato wa maridhiano (BBI) utapitishwa kupitia referenda.

“Hawa kwa urais, wako nje ya mchezo,” akasema.

Bw Murathe akiwa katika kipindi cha runinga ya Inooro kinachofahamika kama Kiririmbi (Moto), alisema kuwa Bw Odinga ana uwezo wa kufanikisha nia ya wengi walio na imani na Rais na serikali yake.

“Nia hiyo ni kuhakikisha kuwa Naibu Rais Dkt William Ruto hafanikiwi kurithi urais. Hilo ni suala ambalo wengi ndani ya utawala huu tumeafikiana na tukaamua ni Bw Odinga ndiye aliye na makali muafaka ya kumzima,” akasema.

Bw Murathe alisema miungano yote inayoibuka kwa sasa ina lengo moja tu la kumzima Dkt Ruto na katika kipindi cha lala salama debeni Bw Odinga ambaye ana uungwaji mkono wa wapigakura wengi, ataunganishiwa kura za wafuasi wa Rais Kenyatta na kwa pamoja iwe ni mteremko kwake hadi Ikulu.

Bw Murathe alisema kuwa “Dkt Ruto amepoteza uungwaji mkono wa wengi ndani ya utawala wa sasa kutokana na mienendo na matamshi yake na kwingine tukimshuku kupungukiwa na maadili.”

Bw Murathe alithubutu kusema kuwa eneo la Mlima Kenya linamuona Dkt Ruto kama mwenye chuki na hivyo lengo lake kuu kuingia Ikulu “halina manufaa yoyote kwa wenyeji wa ukanda huo.”

Mnamo Ijumaa wiki jana, Dkt Ruto alikuwa katika runinga ya Citizen ambapo alidai kuwa “Bw Murathe na washirika wake wamezindua mrengo wa kunizima nisiwanie urais lakini namwambia pamoja na hao watu wake wajipange kwa kuwa huo ni mkondo ambao hauzuiliki.”

Dkt Ruto alikiri njama ipo ya kumsambaratisha huku akihujumiwa waziwazi na watu wengi.

“Ninasisitiza iwapo nitatwaa huu urais, singependa kumwona naibu wangu akidharauliwa jinsi ninavyoonyeshwa madharau ya wazi,” alisema Dkt Ruto.

Bw Murathe alisema kuwa Bw Odinga anafaa kuanza kupokelewa na Wakenya kama aliye mfaafu zaidi “na akipata, ahudumu kwa kipindi kimoja tu cha miaka mitano sawa na jinsi shujaa wa Afrika Kusini marehemu Nelson Mandela alivyotawala.”

Mandela aliingia uongozini mwaka 1994 akiwa na umri miaka 75 na ambapo aliingia katika historia ya kuwa Rais wa Kwanza Mweusi na mkongwe zaidi wa taifa hilo na ambapo alitawala kwa miaka mitano pekee na akastaafu.

Aliaga dunia Desemba 5, 2013, akiwa na umri wa miaka 95.

Ikiwa ‘utabiri’ wa Bw Murathe utaishia kuwa ni ukweli, basi Bw Odinga atawania urais mwaka 2022 akiwa na umri wa miaka 78 na akifanikiwa atawale hadi 2027 ambapo atastaafu akiwa na umri wa miaka 83.

Murathe sasa akiri kauli ya Kang’ata ni kweli kuhusu BBI kususiwa

Na WANDERI KAMAU

NAIBU Mwenyekiti wa Chama cha Jubilee, David Murathe, Alhamisi alimtetea Seneta Irungu Kang’ata wa Murang’a, akisema alieleza ukweli kuhusu hali ilivyo katika Mlima Kenya kuhusu ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI).

Majuma matatu yaliyopita, Seneta Kang’ata alimwandikia barua Rais Uhuru Kenyatta akimwambia kuchukua hatua za haraka kutatua changamoto zinazowaathiri wenyeji wa Mlima Kenya, kwani wengi wao hawaungi mkono ripoti hiyo.

Licha ya Dkt Kang’ata kukosolewa vikali na baadhi ya wanasiasa wanaomuunga mkono Rais Kenyatta, Bw Murathe alisema kuwa seneta huyo hapaswi kukosolewa kwani alisema ukweli, lakini alitumia njia isiyofaa.

Kwenye barua hiyo ambayo ilizua hisia kali za kisiasa katika ukanda huo, Dkt Kang’ata alionya kuwa huenda juhudi za Rais Kenyatta kuwarai wenyeji kuunga mkono BBI zikakosa kuzaa matunda, ikiwa serikali haitaeleza mikakati ya kuboresha hali ya uchumi na kufufua upya sekta ya kilimo.

Akionekana kukubali kulikuwa na tatizo kuhusu jinsi mikakati ya kuipigia debe ripoti hiyo Mlima Kenya ilikuwa ikiendeshwa, Bw Murathe aliwakosoa viongozi waliotwikwa jukumu hilo kwa kuwalazimishia wananchi kukubali BBI.

“Huwezi kuwalazimishia wenyeji jambo bila kuwaelezea au kuwafafanulia ukweli. Hilo ndilo tatizo kuu lililokuwepo. Hata hivyo, tunalenga kulainisha shughuli za kuipigia debe BBI baada ya mkutano wa viongozi wa eneo hilo utakaofanyika kesho Sagana,” akasema.

Wakati huo huo, Bw Murathe alifichua kwamba Rais Kenyatta ndiye aliyewazuia kuwachukulia hatua za kinidhamu maseneta maalum waasi chamani kama Isaac Mwaura, Millicent Omanga na Mary Seneta.

Alisema usimamizi mkuu wa chama ulikuwa tayari umeanza mchakato wa kuwafukuza chamani lakini Rais akawarai kusitisha.

Wandani wa Ruto sasa wamuonya Murathe

SHABAN MAKOKHA na CHARLES WASONGA

WANDANI wa Naibu Rais William Ruto wamemwonya Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe dhidi ya kuingiza jina la naibu huyo wa rais katika sakata inayozonga Mamlaka ya Usambazaji Dawa Nchini (Kemsa).

Bw Murathe Ijumaa alihojiwa na maafisa wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) jijini Nairobi kuhusu uhusiano wake na kampuni ya Kiling Limited iliyopewa zabuni ya kuisambazia Kemsa vifaa 450,000 vya kujikinga dhidi ya Covid-19 (PPEs) na ikalipwa Sh4 bilioni.

Hii ni baada ya madai kuibuka kwamba yeye ni mmoja wa wasimamizi wa akaunti za kampuni hiyo inayomilikiwa na kakake mwanahabari Tony Gachoka, Wilbroad Gachoka na mwanamume mmoja mwa jina Zhu.

Lakini badala yake Bw Murathe alidai Dkt Ruto alinunua hisa katika Kilig Limited na akawataka maafisa wa EACC na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kumhoji naibu huyo wa rais kuhusiana na sakata hiyo.

Vile vile, aliwataka wapelelezi kuwaamuru maseneta wa zamani Boni Khalwale (Kakamega) na Johnstone Muthama (Machakos) kufika mbele ya waelezee wanachofahamu kuhusiana na sakata hiyo.

Akiongea na wanahabari baada ya kuhojiwa kwa zaidi ya saa mbili na maafisa wa EACC katika afisi za tume hiyo zilizoko jumba la Madison, Nairobi, Murathe alidai aliitwa kama shahidi wala sio mshukiwa wa sakata hiyo.

Lakini Jumamosi Dkt Khalwale, Muthama na Mbunge wa Mumias Mashariki Benjamini Washiali walimwonya Bw Murathe dhidi ya kuchezea jina la Dkt Ruto.

“Inasikitisha kuwa Bw Murathe anacheza na jina la Naibu Rais na kuitumia kama mwanasesere. Anapaswa kuheshimu afisi ambayo Dkt Ruto anashikilia kwa sababu ndiyo ya pili kimamlaka nchini. Ingawa ni wazi kuwa hamheshimu kama mtu binafsi hana budi kuheshimu afisi anayoshikilia kama Naibu Rais,” Bw Washiali. 

Mbunge huyo alimtaka Bw Murathe ajiuzulu wadhifa wake katika chama cha Jubilee akisema mienendo na matamshi yake yanaiharibia sifa chama hicho kinachoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.

“Bw Murathe asipojiuzulu aondolewe kwa nguvu. Chama tawala chenye wajumbe wenye katika mabunge yote hakipasi kusimamiwa na naibu mwenyekiti mfisadi,” Bw Washiali akaeleza.

Dkt Khalwale alipuuzilia mbali kauli ya Murathe kwamba yeye na Muthama wakife mbele ya EACC akisema hawajahitajika kufanya hivyo.

“Atuambie anataka tujitetee kuhusu nini katika EACC kwa sababu sisi sio kama yeye aliyeitwa kujitetea baada ya kutajwa katika sakata ya Kemsa. Hatuna makosa ya kujitetea kwayo,” akasema.

Hata hivyo, Dkt Khalwale alisema wako tayari kufika mbele ya tume hiyo kama mashahidi endapo wataitwa.

‘Tangatanga’ Mlima Kenya wamtaka Murathe akome ‘kuaibisha’ Rais

Na MWANGI MUIRURI

WASHIRIKA wa Naibu Rais Dkt William Ruto eneo la Mlima Kenya, wamemtaka Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe akome kumwangazia Rais Uhuru Kenyatta kama asiyeaminika wala kujielewa kisiasa.

Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua, Ndindi Nyoro wa Kiharu na Alice Wahome wa Kandara walisema Jumapili kuwa Rais Kenyatta kutokana na matamshi ya mara kwa mara ya Bw Murathe, ameibuka machoni mwa umma kama asiye na msimamo wa kisiasa, asiyeaminika kuweka ahadi na ambaye ‘amechanganyikiwa’ kuhusu 2022.

Walisema kuwa Bw Murathe huenda akafikiria kuwa anamsaidia Rais kudhibiti siasa za Mlima Kenya na zile za urithi wa 2022 “lakini kwa hakika anamwaibisha Rais, anamkosesha heshima na kuzidisha kero ya wenyeji dhidi ya utawala wa Jubilee na siasa zake kuhusu uchaguzi wa 2022.”

Wakiongea katika mkahawa mmoja mjini Murang’a, watatu hao walisema kuwa Rais Kenyatta kama mtu binafsi ni “muungwana, wa kuaminika na asiyependa fitina ndogondogo.”

Rigathi alisema ameshawahi kuhudumu kama msaidizi wa Kenyatta “na ninaweza nikakuambia waziwazi bila hofu ya kujikanganya kuwa Bw Murathe hajatumwa na Rais kuyaanika ayasemayo kila mahali na kuishia kukanganya watu.”

Alisema kuwa Murathe amemewangazia Rais kama “aliyehadaa na anayeshirikisha aibu kwa Dkt Ruto kisiasa, ametangaza kuwa Rais atamuunga mkono kinara wa ANC Musalia Mudavadi, akabadilisha ngoma na kutangaza kuwa angemuunga mkono Raila Odinga kabla ya kubadili mawazo na kutangaza kuwa Rais alikuwa kwa Peter Kenneth au Waziri wa Kilimo, Peter Munya.”

Hata hivyo, Bw Murathe alipuuzilia mito hiyo akisema kuwa “mimi siko kwa Tangatanga na masuala ambayo tunapanga huko mbele kuhusu umoja na ustawi wa taifa hili hayataniwezesha kujibizana nao.”

Mbunge wa Gatanga Bw Nduati Ngugi alisema kuwa “mrengo wa Tangatanga Mlima Kenya unafaa uelewe kuwa isipokuwa ni jina la rais walitumia wakiwania vyeo vyao 2013 na 2017, hawangechaguliwa na ndio sababu wanafaa kuheshimu rais na washirika wake.”

“Ikiwa jina la Rais ndilo lilitufanya tuchaguliwe, basi linafaa kubakia la kuheshimiwa wala sio la kurejelewa kila wakati watu wanataka kutisha wengine kisiasa au kujihakikishia zawadi kutoka kwa wanasiasa wengine kwa msingi wa kuwaahidi kura za Mlima Kenya,” akasema Bw Rigathi.

Alimtaka Murathe kwanza awanie hata ikiwa ni uenyekiti wa Jubilee hata ikiwa ni katika ngazi ya wadi ndipo awe akiongea akiwa na uhalali wa kuwakilisha watu wanaojulikana.

Nyoro alisema mienendo na matamshi ya Bw Murathe, vinaashiria udalali wa hali ya juu kuhusu siasa na “amezingatia tu kulitumia jina la Rais kutafuta umaarufu eneo la Mlima Kenya.”

“Ikiwa Murathe humwakilisha Rais katika matamshi yake ya mara kwa mara, basi anafaa pia kuwa akiingia katika mitaa mbalimbali ya Mlima Kenya na katika mikutano atangaze hayo ambayo huyatangaza akiwa katika ngome za wapinzani wa siasa za eneo hili na pia katika vyombo vya habari,” akasema Nyoro.

Bi Wahome alisema ikiwa Murathe huongea kwa niaba ya Rais na anajua kuwa misimamo hiyo yake hutambulika mashinani eneo la Mlima Kenya, basi hafai kuwa na hofu ya kuandaa kikao katika uwanja wowote wa Mlima Kenya na akizingatia masharti ya Kiafya kuhusu Covid-19, aongee nao moja kwa moja, uso kwa uso.

“Mimi ni jirani wa Murathe ambaye ni mwanasiasa wa eneobunge la Gatanga na ninaweza nikakwambia waziwazi kuwa ikiwa kuna mtu ambaye hawakilishi sauti ya wenyeji kuhusu siasa, basi ni huyu Murathe,” akasema mbunge huyo wa Kandara.

JAMVI: Kauli za Murathe zaacha wengi njia panda

Na BENSON MATHEKA

NAIBU mwenyekiti wa chama cha Jubilee David Murathe amewakanganya Wakenya kwa kubadilisha msimamo wake kuhusu siasa za urithi wa Rais Uhuru Kenyatta.

Ingawa amekuwa akikariri kwamba Rais Kenyatta hana nia ya kumwachia hatamu za uongozi Naibu Wake William Ruto anayemlaumu kwa kudharau kiongozi wa nchi, Bw Murathe amekuwa akitetereka kuhusu ni nani ambaye anafaa kuongoza nchi mwaka wa 2022.

Mnamo Desemba 2019 wakati kampeni za Mpango wa Maridhiano (BBI) zilikuwa kileleni, Bw Murathe alinukuliwa akisema kwamba Rais Kenyatta hatastaafu siasa, kauli iliyochukuliwa na wandani wa Dkt Ruto kwamba kiongozi wa nchi anaweza kushikilia wadhifa wa juu serikalini Katiba ikibadilishwa.

Wakati huo, duru zilisema kwamba Rais Kenyatta alikuwa akimezea mate kiti cha waziri mkuu mwenye mamlaka.

Mchakato wa maridhiano unaendelea na ni ripoti ya mwisho inayotarajiwa wakati wowote itakayotoa mwelekeo wa iwapo Rais Kenyatta atabaki kuwa msemaji wa eneo la Mlima Kenya kwa kuwa serikalini.

Tangu alipoashiria kuwa huenda Rais Kenyatta akaendelea kuwakilisha Mlima Kenya katika siasa za kitaifa baada ya 2022, Bw Murathe amenukuliwa mara kadhaa akitambua wanasiasa anaowekea upatu kumrithi Rais Kenyatta 2022.

“Kauli yake ya hivi punde ilikuwa ya kudai kuwa Waziri wa Kilimo Peter Munya ameiva kuwa msemaji wa Mlima Kenya. Ni kauli iliyotafsiriwa na wengi kwamba kuna minong’ono ya kumfanya gavana huyo wa kwanza wa Kaunti ya Meru kuwa mrithi wa Rais. Hii ilijiri siku chache baada ya Bw Murathe kutoa kauli iliyozua mdahalo mkali mtandaoni akiwataka wakazi wa Mlima Kenya kujiandaa kwa urais wa kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga,” anasema mdadisi wa siasa Geff Kamwanah.

Kabla ya kutoa kauli iliyochukuliwa kama kumtawaza Bw Odinga kuwa chaguo la Rais Kenyatta kuwa mrithi wake 2022, Bw Murathe aliungana na aliyekuwa mbunge wa Gatanga Peter Kenneth, Bw Odinga na Seneta wa Siaya James Orengo nyumbani kwa Katibu Mkuu wa Muungano wa vyama vya wafanyakazi Francis Atwoli ambapo alisema walijadili siasa miongoni mwa masuala mengine.

Wadadisi walisema kwamba hii iliashiria kuwa Bw Murathe anamuandaa Kenneth au alituma ishara kwamba waziri msaidizi huyo wa wizara ya fedha anaweza kutoshea viatu vya Rais Kenyatta.

“Murathe ni mwanasiasa mwerevu sana. Anajua kupanga na kupangua siasa na analotamka huwa lina lengo fulani. Kila kauli anayotoa inafaa kuchukuliwa kwa uzito unaostahili. Ole wao wanaolichukulia kwa mzaha. Kwa hivyo, anapotambua kiongozi fulani, anamaanisha amekuwa mtiifu kwa rais au amefuata mkondo wa rais. Ukisikia sauti yake kuhusu suala fulani, fuatilia utaona yatakayotokea,” asema mdadisi wa siasa, Bonny Kasuki.

Anasema kwa wakati huu, Bw Odinga anafuata mkondo wa Rais Kenyatta, Bw Kenneth amesema kwamba Mlima Kenya watafuata mwelekeo wa kisiasa ambao eneo hilo litapatiwa na Rais Kenyatta, Munya pia ni waziri mtiifu wa serikali ya Rais Kenyatta.

“Katika siasa, hauaniki mbinu zako sote hadharani. Unacheza na akili za watu na kuacha wapinzani wako wakifaruka huku ukijipanga. Hivi ndivyo Murathe anavyofanya kwa niaba ya Mlima Kenya ikizingatiwa kwamba kipindi cha pili cha utawala cha Rais Kenyatta kinaelekea ukingoni,” asema Bw Kasuki.

Kulingana na Bw Kamwanah, Murathe anacheza kamari ya kisiasa kuhakikisha kuwa serikali ijayo italinda maslahi ya wakazi wa eneo la Mlima Kenya.

“Kwa sasa, muhimu kwa wakazi wa Mlima Kenya ni utawala utakaolinda maslahi yao utakuwa katika BBI ikiwa itafaulu au katika muungano wa kisiasa utakaohusisha viongozi anaotaja miongoni mwa wengine,” asema Bw Kamwanah.

Mdadisi huyo anakumbuka kwamba mnamo 2018, Bw Murathe alifanya mazungumzo na kiongozi wa chama cha Amani National Congress Musalia Mudavadi nyumbani kwake Gatanga.

“Wakati huo minong’ono ilikuwa walikuwa wakisuka masuala ya kisiasa. Ingawa Mudavadi anaonekana kufuata mwelekeo tofauti, kumbuka amesema anaunga ajenda za Rais Kenyatta. Murathe pia alikuwa kwenye karamu ya kukaribisha mwaka ya viongozi wa Ukambani nyumbani kwa kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka ambaye pia anaunga rais. Anafanya hayo yote kwa maslahi ya Mlima Kenya baada ya 2022,” alisema.

Wadadisi wa siasa wanakubaliana kuwa kauli za Bw Murathe sio za kupuuzwa ikizingatiwa ukuruba na utiifu wake kwa Rais Kenyatta kwa miaka mingi.

Raila asukumwa awe Rais

Na WAANDISHI WETU

SHINIKIZO za kumtaka kiongozi wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga awanie urais zimeongezeka licha ya kigogo huyo wa siasa nchini kusalia kimya kuhusu malengo yake ya 2022.

Mjadala kuhusu hatima yake kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao ulitokota Jumapili, baada ya Naibu Mwenyekiti wa Chama cha Jubilee, Bw David Murathe, kudokeza kuwa kuna mipango serikalini ya kumkweza Bw Odinga hadi Ikulu ili aongoze kwa miaka mitano kuanzia 2022.

Katika mahojiano kwenye runinga, Bw Murathe ambaye ni mmoja wa wandani wakubwa wa Rais Uhuru Kenyatta alitaja mipango hiyo kuwa sawa na ilivyofanyika Afrika Kusini wakati marehemu Nelson Mandela alitunukiwa nafasi ya kuongoza ili atoe mwelekeo wa uongozi bora.

“Tunaamini wakati umefika kwa Wakenya kumtuza Raila Amollo Odinga kwa kujitolea kwake kwa miaka mingi. Wakenya wana deni lake. Ni kama vile Mandela. Lakini tungependa kumwambia awe rais wa mpito ambaye atawezesha vijana kuingia uongozini ifikapo 2027,” akaeleza.

Ingawa Bw Odinga hukataa kuelezea iwapo anapanga kuwania urais, Bw Murathe alisisitiza ni wazi atakuwepo kwenye kinyang’anyiro hicho.

Matamshi yake yaliibua hisia mseto kutoka kwa viongozi na wafuasi wa Bw Odinga.

Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi nchini (COTU), Bw Francis Atwoli, aliunga mkono kauli ya Bw Murathe.

Akizungumza nyumbani kwake Kajiado ambapo alitarajiwa kukutana na viongozi mbalimbali akiwemo Seneta wa Siaya, Bw James Orengo, katibu huyo alisema Bw Odinga ndiye anastahili zaidi kumrithi Rais Kenyatta.

Suala kuhusu urithi wa Rais Kenyatta ifikapo 2022 limekuwa likiibua msisimko katika ulingo wa kisiasa, hasa ikizingatiwa kwamba uhusiano wake na naibu wake, Dkt William Ruto umesambaratika ikilinganishwa na wakati walipoingia mamlakani 2013.

Wakati huo, iliaminika Rais angemsaidia Dkt Ruto kuingia Ikulu baada ya kuongoza kwa mihula miwili.

Bw Atwoli alieleza kwamba, ingawa kuna wanasiasa wengi ambao wana uwezo wa kuongoza nchi, 2022 inastahili kuachiwa Bw Odinga ili asafishe mandhari ya kisiasa na kiuchumi.

Alisisitiza kuwa balozi huyo wa miundomsingi katika Muungano wa Afrika (AU) anaweza kushinda urais mapema asubuhi kama atakubali kuwania kiti hicho.

Wiki chache zilizopita, Mbunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bw Oburu Oginga ambaye ni kakake Bw Odinga, alikuwa amedai atasaidiwa na watu wenye ushawishi serikalini kuingia mamlakani.

Kulingana naye, kikundi hicho cha watu almaarufu kama ‘system’ ndicho kilikuwa kikwazo kwa Bw Odinga kuingia katika Ikulu miaka iliyopita, lakini sasa amepata baraka zao kwa kushirikiana na Rais Kenyatta.

Hata hivyo, Muungano wa jamii za Gikuyu, Embu na Ameru (Gema) kupitia mwenyekiti wake Askofu Mstaafu Lawi Imathiu ulisema wananchi ndio wataamua atakayekuwa rais.

“Uwanja uko wazi kwa wote na kazi yetu ni kuwasikiza na kuwafuatilia na hatimaye tutafanya uamuzi wetu wa kibinafsi kama wapiga kura,” akasema.

Aliyekuwa mbunge wa Gatanga Bw Peter Kenneth na ambaye anapendekezwa na baadhi ya wabunge wa Mlima Kenya arithi usemaji wa kijamii kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta alisema watasubiri tangazo kutoka kwa Rais Kenyatta kuhusu anayemtaka awe mrithi wake.

“Ikiwa Rais kwa busara yake ataonelea atuongoze kwa Bw Odinga, basi sisi tutatii,” akasema Kenneth.

Aliyekuwa mbunge wa Maragua Bw Elias Mbau alisisitiza kuwa matamshi ya Bw Murathe yanafaa kuchukuliwa kwa uzito.

Hata hivyo, Mbunge wa Kiharu Bw Ndindi Nyoro, aliye mwandani wa Dkt Ruto alipuuzilia mbali dhana kuwa Ikulu inamwandaa Bw Odinga kuwa rais.

Katika eneo la Nyanza ambayo ngome kuu ya kisiasa ya Bw Odinga, Mbunge wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma alisema Bw Odinga ndiye mwanasiasa wa kipekee nchini ambaye anaweza kuendeleza kazi iliyoanzishwa na Rais Kenyatta.

Lakini baadhi ya wakazi eneo hilo walimtaka Bw Odinga kujihadhari na ahadi kuhusu urais, kwani amewahi kuchezewa shere katika tawala zilizopita za marehemu Daniel arap Moi na Rais Mstaafu Mwai Kibaki.

Mwenyekiti wa vuguvugu la wakazi wa Kisumu, Bw Audi Ogada, alisema ni wazi Bw Odinga anastahili kutuzwa kwa jinsi alivyojitolea kuikomboa nchi lakini asiamini ahadi anazopewa hadi zitekelezwe.

 

Ripoti za Charles Wasonga, Valentine Obara, Mwangi Muiruri na George Odiwuor