• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 6:55 AM
Fulham waendeleza masaibu ya kocha Graham Potter kambini mwa Chelsea baada ya kuwapiga 2-1 katika EPL

Fulham waendeleza masaibu ya kocha Graham Potter kambini mwa Chelsea baada ya kuwapiga 2-1 katika EPL

Na MASHIRIKA

FULHAM waliendeleza masaibu ya kocha Graham Potter baada ya kupokeza Chelsea kichapo cha 2-1 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Alhamisi usiku ugani Craven Cottage.

Carlos Vinicius alifungia Fulham bao la ushindi kunako dakika ya 72 baada ya sajili mpya wa Chelsea, Joao Felix, kuonyeshwa kadi nyekundu matokeo yakiwa 1-1. Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Felix kusakatia Chelsea waliomsajili kwa mkopo wa miezi sita kutoka Atletico Madrid ya Uhispania.

Willian ambaye ni mchezaji wa zamani wa Chelsea na Arsenal, aliwaweka Fulham kifua mbele katika kipindi cha kwanza kabla ya beki Kalidou Koulibaly kusawazishia Chelsea. Matokeo hayo yalipaisha Fulham hadi nafasi ya sita kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 31, sita zaidi kuliko Chelsea ambao wana mchuano mmoja wa akiba.

Kichapo hicho kutoka kwa Fulham kinaweka Potter katika hatari ya kupigwa kalamu ikizingatiwa kwamba ameongoza Chelsea sasa kushinda mechi mbili pekee kati ya 10 zilizopita katika mashindano yote.

Alama 25 zinazojivuniwa na Chelsea kutokana na mechi 18 za ufunguzi wa EPL msimu huu ndizo chache zaidi kwa kikosi hicho kujizolea kufikia hatua kama hii kwenye kipute hicho tangu 2015-16. Huo ndio msimu wa pekee tangu 1996-97 ambapo Chelsea walikosa kufuzu kwa soka ya bara Ulaya.

Chelsea walichapwa na Fulham siku tano baada ya kuaga Kombe la FA katika raundi ya tatu kufuatia kichapo cha 4-0 kutoka kwa Manchester City mnamo Januari 8, 2023 ugani Etihad.

Chelsea, waliotandikwa na Man-City 1-0 katika EPL awali uwanjani Stamford Bridge, waling’olewa na masogora wa kocha Pep Guardiola kwenye makombe mawili tofauti msimu huu. Walibanduliwa nje ya Carabao Cup kwa kichapo cha 2-0 katika raundi ya tatu uwanjani Etihad mnamo Novemba 9, 2022.

Kadri wanavyosubiri kuendea Borussia Dortmund ya Ujerumani katika mkondo wa kwanza wa hatua ya 16-bora ya UEFA mwezi ujao, Chelsea wamekuwa wakisuasua pia katika EPL.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Barcelona kuvaana na Real Madrid kwenye fainali ya Spanish...

KWPL: Kisumu All Starlets kupimana nguvu na WADADIA Women

T L