PSG wamsajili kipa Gianluigi Donnarumma wa Italia bila ada yoyote

Na MASHIRIKA

PARIS Saint-Germain (PSG) wamemsajili kipa matata wa timu ya taifa ya Italia, Gianluigi Donnarumma, kwa mkataba wa miaka mitano.

Mlinda-lango huyo mwenye umri wa miaka 22 alisalia mchezaji huru baada ya mkataba wake na AC Milan ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu wa 2020-21.

Anaingia katika sajili rasmi ya PSG baada ya kuibuka Mchezaji Bora wa kipute cha Euro kilichotawaliwa na Italia baada ya kuzamisha Uingereza 3-2 kwenye fainali iliyochezewa katika uwanja wa Wembley jijini London mnamo Julai 11, 2021.

Donnarumma alipangua penalti mbili za Uingereza kwenye fainali hiyo.

Kufikia sasa, Donnarumma amechezea timu ya taifa ya Italia mara 33 na amekuwa kipa chaguo la kwanza la kikosi hicho ambacho kwa sasa kinanolewa na kocha Roberto Mancini.

Hadi mkataba wake na AC Milan ulipotamatika, Donnarumma alikuwa amewajibishwa na kikosi hicho katika mechi 251 kwenye mashindano yote. Alichezeshwa na AC Milan kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 16.

Alichezeshwa na AC Milan katika mechi zote isipokuwa moja kwenye kampeni za Serie A mnamo 2020-21 na kusaidia kikosi hicho kurejea katika soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa mara ya kwanza tangu 2014 baada ya kukamilisha kampeni za Serie A katika nafasi ya pili.

AC Milan tayari wamemsajili kipa Mike Maignan ambaye ni raia wa Ufaransa kujaza pengo la Donnarumma. Maignan alisaidia Lille kukomesha ukiritimba wa PSG kwa kunyakua taji la Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) mnamo 2020-21.

Chini ya kocha wa zamani wa Tottenham Hotspur, Mauricio Pochettino, PSG walibanduliwa na Manchester City kwenye nusu-fainali ya UEFA mnamo 2020-21. Kikosi hicho kilizidiwa maarifa na Bayern Munich kwa kichapo cha 1-0 kwenye fainali ya 2019-20 jijini Lisbon, Ureno.

Donnarumma anakuwa mchezaji wa nne kusajiliwa na PSG muhula huu baada ya kiungo mahiri raia wa Uholanzi, Georginio Wijnaldum, 30, kujiunga nao kutoka Liverpool na beki Sergio Ramos, 35, kusajiliwa baada ya mkataba wake na Real Madrid kutamatika.

PSG wamemsajili pia beki raia wa Morocco, Achraf Hakimi, 22, kutoka Inter Milan kwa mkataba wa miaka mitano.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

Kipa Gianluigi Donnarumma wa Italia atawazwa Mchezaji Bora wa Uefa Euro 2020

Na MASHIRIKA

KIPA Gianluigi Donnarumma wa Italia alitawazwa Mchezaji Bora wa kipute cha Euro 2020, mashindano yaliyokamilika rasmi Julai 11, 2021.

Mlinda-lango lango huyo mwenye umri wa miaka 22 anatarajiwa kuingia katika sajili rasmi ya Paris Saint-Germain (PSG) muhula huu baada ya mkataba wake na AC Milan ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu wa 2020-21.

Donnarumma alipangua mikwaju miwili ya penalti katika fainali ya Euro iliyoshuhudia Italia ikizamisha chombo cha Uingereza baada ya kuambulia sare ya 1-1 mwishoni mwa muda wa kawaida na wa ziada.

Mlinda-lango wa Italia Gianluigi Donnarumma (kati-kushoto) amkumbatia mlinda-lango wa Italia Salvatore Sirigu (kati-kulia) mara baada ya ushindi kwenye fainali kali ya Uefa Euro 2020 iliyokutanisha Italia na Uingereza uwanjani Wembley jijini London, Julai 11, 2021. Picha/ AFP

Ufanisi huo wa Italia uliwavunia taji la kwanza la Euro tangu 1968.

Donnarumma ambaye hakufungwa katika mechi tatu za kampeni za Euro mwaka huu, aliwazidi ujanja Jadon Sancho na Bukayo Saka walioaminiwa fursa za kuchanja penalti za mwisho za Uingereza.

Ndiye kipa wa pili katika historia kuwahi kujizolea tuzo hiyo kwenye Euro baada ya aliyekuwa ‘nyani’ wa Denmark, Peter Schmeichel mnamo 1992.

Donnarumma aliwajibishwa na Italia kwa kipindi cha dakika 719 kwenye fainali za Euro mwaka huu na akawa mchezaji wa pekee aliyechezeshwa na kocha Roberto Mancini katika kila mojawapo ya mechi kwenye kipute hicho.

“Tulijituma vilivyo bila ya kukata tama. Tulianza vyema kampeni hizi kwa kuweka wazi malengo yetu. Ingawa hatukutarajia ufanisi huu, hili ni taji ambalo nahisi kwamba tulistahili kulitwaa,” akasema Donnarumma.

Gonzalez ‘Pedri’ Lopez wa Uhispania alitawazwa Chipukizi Bora wa kipute cha Euro 2020, mashindano yaliyocheleweshwa kwa sababu ya janga la Covid-19.

Pedri mwenye umri wa miaka 18 alikosa kuwajibikia Uhispania kwa dakika moja pekee kwenye Euro baada ya kuondolewa uwanjani katika sekunde za mwisho za muda wa ziada wakati wa robo-fainali dhidi ya Uswisi. Kabla ya kuwakilisha Uhispania kwenye Euro mwaka huu, alikuwa amevalia jezi za kikosi hicho mara nne pekee katika mapambano ya timu ya watu wazima.

“Hakuna mwanasoka yeyote katika historia ya Euro ambaye amefanya kitu ambacho Pedri amekifanya kwenye kipute hicho mwaka huu. Ana umri wa miaka 18 pekee na dalili zote zinaashiria kwamba anafuata nyayo za nguli Andres Iniesta. Ana kipaji adhimu na anaridhisha sana,” akasema kocha wa Uhispania, Luis Enrique.

Cristiano Ronaldo wa Ureno alitawazwa Mfungaji Bora wa Euro mwaka huu. Ingawa idadi ya mabao aliyofunga yaliwiana na yale yaliyopachikwa wavuni na Patrik Schick wa Jamhuri ya Czech, Ronaldo aliibuka kileleni kwa sababu alichangia goli jingine katika mechi ya Kundi F dhidi ya Ujerumani.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

Italia kukutana na Uhispania kwenye nusu-fainali za Euro baada ya kuipiga Ubelgiji 2-1

Na MASHIRIKA

ITALIA waliwakomoa Ubelgiji 2-1 mnamo Ijumaa usiku jijini Munich, Ujerumani na kufuzu kwa nusu-fainali ya Euro itakayowakutanisha na Uhispania mnamo Julai 6, 2021.

Ingawa mchuano huo haukushuhudia idadi kubwa ya mabao yakifumwa wavuni, kila upande ulijituma vilivyo na mashambulizi yakatamalaki mchezo hadi mwisho.

Italia wanaopigiwa upatu wa kutwaa taji la Euro, walijibwaga uwanjani wakipania kuendeleza ubabe wao huku Ubelgiji wakiwa pia na azma ya kusadikisha mashabiki kwamba wanastahili kuorodheshwa katika nafasi ya kwanza kimataifa kwa mujibu wa viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Ushindi wa Italia ulikuwa wao wa 13 mfululizo huku wakiwa sasa wamesakata jumla ya mechi 32 bila kupoteza.

Chini ya kocha Roberto Mancini, Italia walifungua ukurasa wa mabao kupitia Nicolo Barella aliyeshirikiana na Marco Verratti katika dakika ya 31 kabla ya Lorenzo Insigne kufuma wavuni goli la pili dakika 13 baadaye.

Ubelgiji walirejea mchezoni mwishoni mwa kipindi cha kwanza baada ya Romelu Lukaku kufunga penalti iliyochangiwa na hatua ya Jeremy Doku kuchezewa visivyo na Giovanni de Lorenzo katika dakika ya 45.

Kila kikosi kilipoteza nafasi maridhawa za kufunga mabao katika kipindi cha pili kilichotamalakiwa na shambulizi baada ya jingine.

Pigo la pekee kwa Italia ni kwamba watavaana sasa na Uhispania kwenye nusu-fainali uwanjani Wembley, Uingereza bila ya kujivunia huduma za beki wa kushoto Leonardo Spinazzola aliyepata jeraha la kifundo cha mguu katika kipindi cha pili.

Italia walikamilisha kampeni za Kundi A bila ya kupoteza mechi yoyote katika uwanja wao wa nyumbani wa Olimpico, Roma. Waliwapepeta Uturuki 3-0, wakachapa Uswisi 3-0 na kupokeza Wales kichapo cha 1-0. Ufanisi huo uliwakatia tiketi ya hatua ya 16-bora iliyowashuhudia wakipepeta Austria 2-1 katika muda wa ziada uwanjani Wembley.

Hata hivyo, matokeo dhidi ya Ubelgiji nchini Ujerumani huenda ndiyo bora na muhimu zaidi kwa Italia kuwahi kushuhudia katika kipindi cha takriban miaka mitatu bila ya kushindwa.

Italia walianza mechi kwa matao ya juu huku bao la Leonardo Bonucci katika dakika ya 23 likikataliwa na refa baada ya teknolojia ya VAR kubaini kwamba alicheka na nyavu akiwa ameotea.

Kipa Gianluigi Donnarumma wa Italia naye alijitahidi vilivyo na kupangua makombora mazito aliyoelekezewa na wavamizi wa Ubelgiji.

Licha ya kuwa kikosi bora kwa sasa duniani, Ubelgiji ambao pia wanajivunia idadi kubwa ya wanasoka wa haiba kubwa, walikamilisha kampeni za Kombe la Dunia katika nafasi ya tatu mnamo 2018 nchini Urusi. Fainali ya mwisho ya Euro ambayo kikosi hicho kimewahi kunogesha ni ya 1980 ambapo walizidiwa ujanja na iliyokuwa Ujerumani Magharibi.

Mabeki wote watatu wa Ubelgiji walikuwa na umri wastani wa miaka 33 huku wanasoka wawili pekee katika kikosi chao cha kwanza cha 11-bora wakiwa na umri wa chini ya miaka 28.

Mbali na Doku, wanasoka wengine wa Ubelgiji ambao walitatiza pakubwa mabeki wa Italia ni Kevin de Bruyne na Lukaku ambaye sasa amefungia kikosi hicho jumla ya mabao 24 kutokana na mechi 23 zilizopita.

Ingawa imesalia miezi 18 pekee kabla ya fainali zijazo za Kombe la Dunia kuandaliwa nchini Qatar mnamo 2022, kinachosubiriwa ni iwapo Ubelgiji bado watakuwa chini ya mkufunzi wao wa sasa, Roberto Martinez.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO