• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Gladys Wanga aelezea jinsi Ida Odinga alivyomsaidia kujiunga na siasa

Gladys Wanga aelezea jinsi Ida Odinga alivyomsaidia kujiunga na siasa

Na MARY WANGARI

MWAKILISHI wa Wanawake wa Kaunti ya Homa Bay katika Bunge la Kitaifa, Gladys Wanga amefunguka kuhusu safari yake ya siasa akifichua nafasi muhimu aliyochangia mkewe Raila Odinga, Ida Odinga, katika kumfanya mwanasiasa mkakamavu jinsi alivyo leo hii.

Mbunge huyo aliyegonga vichwa vya habari mnamo 2017 katika mgogoro mbaya kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa (JKIA) polisi walipomzuia kumlaki kiongozi wa ODM, alisema kuwa urafiki wake na aliyekuwa waziri mkuu si chanzo cha umaarufu wake kisiasa.

“Kabla ya kujiunga na siasa mwaka 2013, sikujulikana na Raila Odinga. Kwa hakika ni Ida Odinga aliyenitambua, akanitia moyo na kunielekeza,” alisema mwanasiasa huyo katika mahojiano na kituo cha runinga humu nchini.

Mwanasiasa huyo aliyewahi kuwa kiongozi wa wanafunzi, alifutilia mnali dhana kwamba wanasiasa wa kike ni sharti wawe na mahusiano ya kimapenzi na wanaume ili kupanda ngazi kisiasa, akisisitiza kwamba safari yake ilikuwa tofauti maadamu alilazimika kutia juhudi ili kufika alipo sasa.

“Nilianza kufanya kampeni nikitumia gari dogo jeupe nililokuwa nimenunua pamoja na mume wangu kwa mkopo ambapo baadhi ya watu walinicheka wakisema ‘ni mwanasiasa gani huyu katika gari dogo’,” alisema.

Ugavana

Mfuasi sugu huyo wa ODM aliyepigiwa debe na chama cha upinzani 2013, pia alitangaza azma yake ya kuwania kiti cha ugavana Kaunti ya Homa Bay, akitegemea rekodi yake nzuri ya maendeleo, hatua ambayo bila shaka inatarajiwa kumtoa kijasho ikizingatiwa vigogo wengine wa kisiasa kaunti hiyo pia wameelezea nia yao ya kumng’atua Gavana Cyprian Awiti.

Mama huyo wa watoto wawili aliyegunduliwa na hatua ya nne ya saratani ya utumbo takriban miaka mitano iliyopita, vilevile alifafanua kuhusu mswada wa sheria aliopendekeza bungeni unaoshinikiza saratani kujumuishwa kama mojawapo wa kitengo cha kimsingi cha afya, ambapo daktari watahitajika kuwafanyia wagonjwa vipimo kuhusu dalili yoyote ya ugonjwa huo kila mara wanapoenda hospitalini.

You can share this post!

MUTUA: Kuna matunda tele Afrika Mashariki kushikamana

Nuksi zaandama Wanyama akirejea uwanjani, Spurs yalimwa na...

adminleo